Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu amejiwekea utaratibu wa kufanya walau tendo la huruma katika “Ijumaa ya huruma ya Mungu! Wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Wakleri sanjari na Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu na Siku ya kuombea Utakatifu wa Mapadre, baadhi ya Wakleri walishindwa kuhudhuria kutokana na afya zao kuwa tete pamoja na uzee.
kwa Wakleri wazee na wagonjwa, ambao daima anawaweka mbele ya macho yake wakati wa sala na adhimisho la Ekaristi takatifu kwa kuwatembelea Wakleri hao kwenye Jumuiya ya “Monte Tabor” iliyoko hapa mjini Roma. Umekuwa ni muda wa Wakleri kukutana na kushirikishana furaha ya maisha na utume wa Kipadre; sala na tafakari. Hii ni jumuiya inayotoa huduma kwa Mapadre wanane kutoka katika Majimbo mbali mbali ya Kanisa Katoliki nchini Italia.
Baba Mtakatifu katika hija hii ya ”Ijumaa ya huruma ya Mungu” alikuwa ameambatana na Shemasi wa kudumu Ermes Luparia, ambaye aliwahi kuwa ni Kanali wa Jeshi la Anga, akaamua kuacha yote na sasa anaendelea na majiundo yake ya kiroho ili kuwasindikiza watu katika safari ya maisha ya kiroho chini ya uongozi wa Mapadre Wasalvatoriani. Baba Mtakatifu amekutana na kusali na Wakleri hawa kwenye Kikanisa chao.
Baadaye, Baba Mtakatifu Francisko alitembelea tena Jumuiya ya Wakleri wazee wa Jimbo kuu la Roma katika nyumba yao inayojulikana kama “Casa san Gaetano” inayowahudumia Mapadre 21 kwa sasa, wengi wao ni wagonjwa sana. Hawa ni Wakleri ambao baada ya kusadaka maisha yao kwa ajili ya huduma ya Neno na Sakramenti za Kanisa, sasa wamerejea Jangwani, hata pengine wamesahauliwa na wale waliokuwa wanawahudumia wakati walipokuwa wazima, wanachakarika usiku na mchana! Hawa ndio ambao Baba Mtakatifu Francisko amependa kuwakumbuka na kusali pamoja nao, ili kuwatia moyo na kuwafariji katika shida na mahangaiko yao ya ndani, kielelezo cha umwilishaji wa huruma ya Mungu kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni