Jumuiya ya Domenico Tardini maarufu kama Jumuiya ya Nazareth katika maadhimisho ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwake, ilipata nafasi ya uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatfu Francisko, Jumamosi tarehe 18 Juni 2016. Ulikuwa ni muda muafaka wa kukazia umuhimu wa ushuhuda wa Injili ya upendo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Akapata nafasi ya kujibu maswali saba kutoka kwa wanajumuiya wa Domenico Tardini, maarufu kama Jumuiya ya Nazareth. Baada ya tafakari ya Neno la Mungu mintarafu Mfano wa Msamaria mwema, Baba Mtakatifu alijibu maswali saba, alama ya ukamilifu katika Maandiko Matakatifu.
Baba Mtakatifu amewataka vijana kuwa mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma; kuthubutu katika maisha yao badala ya kubweteka na kujikatia tamaa ya maisha. Katika maisha kuna changamoto na fursa ambazo kila mwanadamu anapaswa kuzichangamkia na kuzifanyia kazi katika masuala ya elimu na upendo. Kwa mtu ambaye hawezi kuthubutu, huyo atakwama na hii ni hatari kubwa inayowakabili vijana wengi kiasi cha kushindwa kuthubutu katika maisha. Baba Mtakatifu anasema, inasikitisha kuona watu wametekelezwa pembezoni mwa jamii kama “daladala” iliyokatika usukani, hao wanafanana na majumba ya makumbusho!
Baba Mtakatifu anakaza kusema kifodini ni ujasiri na ushuhuda wa imani kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka ni ushuhuda endelevu wa Kanisa hata katika nyakati hizi, kama ilivyojionesha kwa Wakristo wa Kanisa la Kikoptiki kutoka Misri waliouwawa huko Libya huku wakiikiri imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Baba Mtakatifu anasema, haya si mauaji ya kimbari dhidi ya Wakristo kama inavyojitokeza pia huko Mashariki ya Kati. Mwelekeo wa namna hii ni kutaka kupindisha ukweli kwamba, huko Mashariki ya Kati, Wakristo wanadhulumiwa na kuuwawa kikatili kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Huu ndio ukweli wa kiimani yaani ushuhuda wa Wakristo.
Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Wakristo wanapaswa kumwilisha ushuhuda wao hata katika maisha ya kila siku si tu kwa kumwaga damu yao kutokana na chuki za kiimani. Kuna mashahidi wa ukweli na uaminifu wanaoendelea kujisadaka kila siku dhidi ya rushwa na ufisadi; uchu wa mali na madaraka mambo ambayo yanaendelea kuwakoroga na kuwavuruga watu. Waamini wawe na ujasiri wa kushuhudia ukweli, uaminifu pamoja na kudumisha uvumilivu katika maisha yao dhidi ya dhambi jamii zinazoendelea kujitokeza katika uso wa dunia na kuwa kama ni jambo la kawaida. Wazazi na walezi wawe ni mashuhuda wa imani katika malezi kwa watoto wao na uaminifu katika maisha ya ndoa na familia.
Baba Mtakatifu anasema ni wajibu kwa Wakristo kutambua kwamba, wao ni watenda dhambi: kwa mawazo, kwa maneno na kwa kutotimiza wajibu, kumbe, wanayo dhamana na wajibu wa kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu katika maisha yao kwa njia ya toba na wongofu wa ndani. Kwa Mkristo anayedhani kwamba, tayari ni mtakatifu na wala hana tena doa la dhambi, huyu anapungukiwa busara. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, tangu katika maisha ya ujana wake, kama Padre, Askofu na hata kama Khalifa wa Mtakatifu Petro amekumbana na changamoto za maisha ya kiroho, akapambana nazo kwa kupiga moyo konde na kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi. Kwa mwamini asiyetikiswa katika imani, huyo pengine tayari amekwishakumezwa na malimwengu.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga utamaduni wa kujisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa jirani zao hasa katika ulimwengu mamboleo ambamo mambo mengi yanapimwa kutokana na umuhimu wake kwa kujikita katika falsafa ya kula na kulipa eti ndio mtindo wa kisasa “do ut des”. Huu ni mtindo wa maisha unaojikita katika ubinafsi na kupenda raha kupita kiasi mambo ambayo yanaendelea kusababisha majanga kwa watu wengi duniani. Hapa kuna haja ya kuwatambua waamini ambao kweli ni watakatifu katika maisha yao na wale “watakatifu feki” wanaojivika mavazi ya kondoo kumbe ni mbwa mwitu wakali tena wa hatari.
Uchu wa mali, utajiri wa haraka haraka na madaraka ni mambo ambayo yanaendelea kuwatumbukiza watu wengi katika utumwa mamboleo na matokeo yake ni ukosefu wa haki pamoja na kumong’onyoka kwa maadili na utu wema. Watu wapimwe na kuheshimiwa kutokana na utu wao kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na wala si kwa wingi wa mali na utajiri wanaomiliki. Kanisa lioneshe kuwa ni Mama mpendelevu, mwenye malango yake wazi, tayari kuwapokea wote wanaobisha hodi ili kuambata huruma na upendo wa Mungu. Kanisa lijenge na kudumisha utamaduni wa ukarimu na mapendo.
Baba Mtakatifu anawaambia vijana kutothubutu kufunga ndoa ikiwa kama hawatambui umuhimu wa maisha ya ndoa na familia mintarafu mafundisho ya Kanisa. Watambue kwamba, Sakramenti ya Ndoa inajikita katika udumifu hadi pale kifo kitakapowatenga, uaminifu katika upendo usiogawanyika, malezi kwa watoto ambao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, ndoa ni mfano wa upendo wa Kristo kwa Kanisa lake.
Kwa wanandoa ambao bado hawajajiandaa kikamilifu kubeba wajibu na dhamana yao ndani ya Kanisa na katika jamii, kamwe wasithubutu kufanya mchezo wa kuigiza mbele ya Kanisa kwani matokeo yake ni kuvunjika kwa ndoa. Wanandoa waoneshane upendo wa dhati, wawe tayari kusamehe na kuanza upya, wachukuliane na kusaidiana katika mchakato wa kuwa watakatifu, huku wakiendelea kuimarishana katika tunu msingi za maisha ya Kikristo! Na kwa mwaliko huu, Baba Mtakatifu Francisko alikuwa anahitimisha hija ya upendo, mshikamano na ushuhuda wa maisha ya Kikristo yanayojikita katika ukarimu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni