Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo mitume, tarehe 29 Juni 2016, Majira ya saa 3:30 asubuhi kwa saa za Ulaya anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu na kutoa Pallio Takatifu kwa Maaskofu wakuu wapya walioteuliwa katika kipindi cha mwaka 2015- 2016. Palio hizi takatifu watavishwa kwenye Majimbo yao makuu ya Mabalozi wa Vatican kwa wakati muafaka.
Wakati huo huo, Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma katika barua yake kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma anakumbusha kwamba, hapo tarehe 29 Juni 2016, Mama Kanisa ataadhimisha Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani, siku maalum ambayo imetengwa na Kanisa ili kuonesha moyo wa upendo na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kuchangia, ili kusaidia utekelezaji wa Injili ya upendo inayomwilishwa katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Kwa Makanisa mengine duniani, ili kuweza kuwashirikisha waamini wengi zaidi katika mchakato wa huduma ya upendo hasa mwaka huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, mchango huu unafanywa tarehe 26 Juni 2016. Kwa kuongozwa na changamoto inayoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa kulitaka Kanisa kuonesha huruma, upendo na ukarimu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, waamini wanahamasishwa kuchangia kwa hali na mali.
Lengo ni kufanikisha jitihada hizi za huruma ya Mungu ambazo kimsingi zinafumbatwa katika Sakramenti za Kanisa na kumwilishwa katika huduma ya ukarimu na upendo kwa watu wanaokumbwa na umaskini, ujinga na maradhi; kwa wakimbizi na wahamiaji; kwa watu wanaokumbwa na maafa mbali mbali kwa sasa. Mchango huu unamwezesha Khalifa wa Mtakatifu Petro kuwa ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.
Viongozi wa Kanisa wanatakiwa kuwahamasisha waamini kutambua umuhimu wa kuchangia huduma ya upendo na ukarimu inayotolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa watu sehemu mbali mbali za dunia. Jimbo kuu la Roma, linadhamana kubwa zaidi, kwani linahamasishwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Askofu wake mkuu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu duniani. Kardinali Vallini anawahimiza wadau mbali mbali kuonesha moyo wa upendo na ukarimu na kwamba, anawatakia wote heri na baraka katika huduma ya mshikamano.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni