Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni muda muafaka wa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha ya watu. Huruma ni mtindo wa maisha na wala si maneno yanayoelea kwenye ombwe, bali yanapaswa kuwa ni muhtasari wa Injili ya huruma. Imani bila matendo hiyo anasema Mtume Yakobo hiyo imekufa ndani mwake. Huruma inapaswa kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii: kiroho na kimwili. Huruma ni jicho linalomsaidia mwamini kuona; ni sikio linalosikiliza kilio cha maskini na kukipatia jibu kwa wakati muafaka.
Hii ni sehemu ya Katekesi ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 30 Juni 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anakaza kusema, matendo ya huruma yanamwezesha mwamini kuwasaidia ndugu na jirani zake wanaogelea katika hali ngumu ya maisha, bila kuwageuzia kisogo kana kwamba hakuna kitu kinachowashtua katika maisha, kielelezo cha ukavu wa maisha ya kiroho.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna vielelezo vingi vya huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu na kwa mwamini ambaye ameguswa na huruma ya Mungu kamwe hawezi kuwa na moyo mgumu kama jiwe kiasi cha kushindwa kuona mateso na mahangaiko ya jirani zake. Mafundisho ya Yesu hayatoi mwanya wa kukwepa majukumu bali kuhakikisha kwamba, wanamwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha ya watu. Matendo ya huruma ni ushuhuda wa maisha.
Baba Mtakatifu anasikitika kusema, kutokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, umaskini wa maisha ya kiroho na kimwili umeongezeka maradufu katika ulimwengu mamboleo, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kusaidia mchakato wa kupambana na umaskini wa hali na kipato duniani. Mwelekeo wa maisha ya Kikristo unapaswa kuwa macho ili kusikiliza na kujibu kilio cha maskini wa nyakati hizi, daima, waamini wakiwa makini kuangalia yale mambo ya msingi katika maisha.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, amechukua fursa hii kumshukuru Mungu aliyemwezesha kutembelea Armenia, nchi ambayo iliupokea na kuukumbatia Ukristo kama dini rasmi kwa ajili ya watu wake. Familia ya Mungu nchini humu katika historia na maisha yake imeguswa na kutikiswa sana, lakini daima imekuwa imara kama shuhuda wa imani. Baba Mtakatifu anawashukuru viongozi wa Serikali na Makanisa na wananchi wote wa Armenia waliompokea na kumkaribisha kama hujaji wa udugu na amani.
Baba Mtakatifu anasema kwamba, Mwezi Septemba, anatarajia kufanya hija ya kichungaji nchini Georgia na Azebaigian ili kutambua na kuimarisha mizizi ya Ukristo unaojikita katika majadiliano ya kidini na kitamaduni pamoja na kukoleza mchakato wa amani unaohitaji uvumilivu na udumifu kwa kujikita katika utamaduni wa kukutana na watu wengine, ili kila mtu aweze kuchangia katika upatanisho. Waamini wanahamasishwa kuimarisha umoja na udugu ili kushuhudia Injili ya Kristo, chachu ya ujenzi wa jamii inayojikita katika haki na mshikamano.
Baba Mtakatifu anamshukuru Patriaki Karekin II kwa ukarimu uliomwezesha kukaa katika makao yake makuu wakati wote wa hija yake ya kitume nchini Armenia. Baba Mtakatifu anachukua nafasi hii kuishukuru familia ya Mungu nchini Armenia pamoja na kuiweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria ili aweze kuwaimarisha katika utamaduni wa kukutana na watu; imani na ukarimu unaomwilishwa kwenye matendo ya huruma. Matendo ya huruma anasema Baba Mtakatifu ni kiini cha imani katika matendo.
Baba Mtakatifu anawatakia vijana maandalizi mema kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 huko Cracovia, Poland, daima waendelee kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu. Anawataka waamini kuendeleza na kuthamini utamaduni wa kazi unaojikita katika utu na heshima ya binadamu, mafao, ustawi wa wengi pamoja na kuendeleza tunu msingi za maisha ya kifamilia. Mateso na mahangaiko ya familia ni matokeo ya sera mbaya za kazi na ajira.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni