0
Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania kuanzia tarehe 25 Septemba hadi tarehe 1 Oktoba 2016 liliendesha Kongamano la Huruma ya Mungu lililowashirikisha waamini kutoka katika Majimbo Katoliki yanayounda Jimbo kuu la Mwanza. Hiki kilikuwa ni kipindi muafaka cha kutafakari, kusali na kumwilisha huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha ya waamini huko Majimboni, Parokiani, kwenye Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, lakini zaidi katika maisha ya kifamilia! Leo Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inapenda kukushirikisha tafakari ya kina iliyotolewa na PadreWojciech Adam Koscielniak, moja ya wamissionari wa huruma ya Mungu walioteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Leo anachambua umuhimu wa kuabudu Ekaristi Takatifu kama njia muafaka ya kukumbatia na kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya mwamini!


Ndugu Mahujaji wenzangu,
hivi punde tutapiga magoti na kukiri imani thabiti ya Kanisa, imani ya karne zote, katika uwepo halisi wa Yesu Kristo Mteswa na Mfufuka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu ndani ya Hostia nyeupe itakayowekwa ndani ya jua hili la mwonyesho.
Baba Mtakatifu Benedikto wa XVI alisema kwamba neno ‘kuabudu’ - kwa Kigiriki proskynesis - maana yake ni tendo la kujinyenyekeza mbele ya Mungu, ni tendo la kumtambua Mungu kama Mungu na Bwana wetu ambaye tunataka kumfuata katika maisha yetu. Uhuru wa kweli wa binadamu ni kuishi ndani yake Mungu huyo katika ukweli na wema wake kusudi nasi tuweze kuwa wakweli na wema. Tendo la kupiga magoti mbele ya Yesu wa Ekaristi katika ibada hii ni muhimu sana katika nia yetu hii ya kumfuata Mungu katika uhuru kamili.
Lakini ipo maana nyingine ya neno ‘kuabudu’. Neno ‘kuabudu’ kwa lugha ya kilatini ni adoratio. Neno hili maana yake ni busu, kumbatio, upendo. Tendo la kujinyenyekeza kwetu mbele ya Bwana katika Ekaristi Takatifu linajibiwa kwa tendo la Yesu wa Ekaristi anayetunyanyua na kutubusu na kutukumbatia kwa upendo kamili katika Fumbo hili la Ekaristi Takatifu. Tunapomsujudia Bwana na kujinyenyekeza mbele yake na kubusu miguu yake kwa moyo wa toba, uchaji na upendo, Yeye anatunyanyua ili atubusu mdomoni kama ishara ya kututambua sisi kuwa marafiki zake wapendwa na si watumishi au watumwa! Ndivyo, maana Yule tunayemwabudu ni Upendo na Huruma yenyewe, ni Yesu anayetuweka huru kabisa kwa maana yake halisi, katika Fumbo hili la Upendo wa ajabu katika Ekaristi Takatifu.
Ndugu Mahujaji, kama nilivyokwishadokeza - Ibada hii ni tendo letu la hadhara la kukiri kwa imani thabiti ya karne zote ya Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume - Uwepo halisi wa Bwana wetu Yesu katika Ekaristi.
Na Bwana mwenyewe anatusaidia kuimarisha imani hiyo kwa njia ya matukio mengi ya kimiujiza yanayohusu Fumbo la Ekaristi. Nidyo matukio ambapo Hostia Takatifu zilivuja damu ama kugeuka kuwa mwili wa kibinadamu. Muujiza wa kwanza kabisa uliothibitishwa na watalaam na mamlaka ya Kanisa ulitokea katika mji wa Lanciano, nchi ya Italia ya sasa, katikati ya karne ya nane. Tangu tukio lile hadi sasa matukio karibia 140 yalithibitishwa na Kanisa na watalaam na wanasayansi mbalimbali kuwa ni miujiza halisi ya kiekaristia.
Matukio mawili ya mwisho yalitukia hivi karibuni nchini Poland ninakotoka mimi - katika mji ndogo wa Sokółka kaskazini-mashariki mwa Poland; na katika mji wa Legnica magharibi kusini mwa Poland. Na juzi nilipoenda nyumbani kwa matibabu, nilifanya hija ya kwenda mji wa Sokółka ambapo korporale yenye Hostia Takatifu ambayo nusu yake ilivuja damu na kugeuka kuwa mwili wa kibinadamu - imewekwa hadharani ndani ya monstransia maalum juu ya tabernakulo.
Uchunguzi na utafiti wa watalaam katika matukio yote haya karibia 140 umebaini  vitu viwili vinavyofanana katika kila tukio - kwanza: mwili huo ni sehemu ya msuli wa moyo wa mwanaume mwenye umri wa miaka 30-33, tena msuli huo uko katika hali ya kupigania roho, katika hali ya kufa. Kwa kiingereza - this heart muscle is in the state of agony. Na pili: katika matukio yote ya miujiza ya kiekaristia, damu hiyo ni daima ya aina ya AB. Fikirini, utafiti na uchunguzi wa watu mbalimbali wa nyakati mbalimbali tangu karne ya nane hadi wakati wetu huu - lakini majibu yote yanafanana kabisa! Utadhani wamekubaliana kutoa majibu ya aina moja! Wakati sivyo.
Habari hii ituweke sawa katika ibada yetu hii ya kumwabudu Yesu wa Ekaristi na kuimarisha imani yetu. Hostia hii nyeupe nitakayoiweka altareni sasa kwa kweli ni pazia tu, kama lile pazia la Hekalu la Yerusalemu lililoficha Patakatifu pa Patakatifu mbele ya macho ya wasiohusika. Hostia hii ni alama ya Mungu Hai Aliye hapa kweli miongoni mwetu. Ndiye Mungu aliyejifunua kwa Musa katika alama ya kichaka kiwakacho mlimani Horebu kwanza. Ndiye Mungu anayetuambia - Mimi Niko Ambaye Niko. Niko pamoja nanyi hata ukamilifu wa dahari.
Hostia hii kwa karne ishirini sasa inatuambia daima - ‘Niko pamoja nawe. Na daima nitakuwa pamoja nawe, haijalishi kama wewe utakuwa pamoja nami au la’. Hujaji mwenzangu, katika ibada hii uikaribie kwa imani Hostia hii nyeupe na ufunue pazia na uuone Moyo Mtakatifu wa Yesu. Moyo huo unapigania roho kwa ajili ya upendo wake kwako na katika hali ya kujitoa sadaka kwa ajili ya wokovu wako na wa dunia nzima. Tafakari kwa kina katika Ibada hii maneno ya kiitikizano tunayotamka mwishoni mwa Litania ya Moyo Mtakatifu wa Yesu - “Ee Yesu, mwenye Moyo mpole na mnyenyekevu, uifanye mioyo yetu ifanane na Moyo wako!”
Jiulize kama kweli unamaanisha maneno haya wakati ukiyatamka ama unayatamka kwa mazoea tu na hayatikisi tena dhamiri zako na hisia zako za ndani kabisa. Jihoji kama kweli unataka moyo wako ufanane na Moyo Mtakatifu wa Bwana uliomo ndani ya Hostia hii nyeupe. Na uwe na hali iyo hiyo uliyo nayo Moyo wa Yesu? Jihoji kama uko tayari kuteseka na kupigania roho yako hadi kufa kwa ajili ya upendo wako kwa Mungu na kwa nia ya kujitoa sadaka kwa ajili ya wokovu wa watu na wa dunia nzima? Hasa wokovu wa wale wanaokuzunguka, maadui zako na watu wasio na shukrani kwa wema wako unaowatendea katika familia yako, katika jumuiya unamoishi, katika mazingira ya masomo na kazi?
Jihoji kama kweli unataka kuteseka kimya kimya kama Yesu anavyoendelea kuteseka ndani ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa ajili ya watu hao wote wanaokuzunguka wasio na shukrani kwako na wasiojali hata wakiambiwa kwamba unateseka kwa ajili yao?
Uutazame Moyo wa Mwokozi na tafakari…
Tumkaribishe sasa miongoni mwetu Yesu Mfufuka katika Ekaristi Takatifu, Yesu - Umwilisho wa Huruma ya Mungu. Tuimbe wimbo wa Ekaristi, kisha ya kufukiza Hostia Takatifu - wimbo wa kuabudu.
Ndugu waamini wenzangu, tukiwa bado mwanzoni mwa Kongamano letu la Huruma ya Mungu katika Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu hapa Kawekamo, tukiwa katika mazingira haya ya Fumbo la Uwepo halisi wa Bwana wetu Yesu Kristo, Mteswa na Mfufuka katika Ekaristi na katika kusanyiko hili takatifu, tukiwa katika Ibada hii ya Saa Takatifu, Neno la Mungu linatujia kwa kusudi maalum la kutuandaa vema kushiriki Kongamano hili kwa makini tangu mwanzo mpaka mwisho wake na muda wote huo tukiwa na msimamo wa mwanafunzi na shahidi wa Yesu Mfufuka na Mfalme wa Huruma.
Neno hili linakuja kwetu katika Masomo manne. Masomo haya manne ni kama miguu minne imara ya meza thabiti ambayo juu yake tutajenga hatua kwa hatua mafundisho yote katika Kongamano letu siku kwa siku. Nasi tulipokee, kulitafakari na kulifanyia kazi kwa dhati katika maisha yetu.
Neno la kwanza la Mungu mwenye Huruma latoka katika Injili ya Mt. Mathayo.
Mt 26:30-44:
Nao walipokwisha kuimba, wakatoka nje kwenda mlima wa Mizeituni. Ndipo Yesu akawaambia, Ninyi nyote mtachukizwa kwa ajili yangu usiku huu kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika. Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya. Petro akajibu, akamwambia, Wajapochukizwa wote kwa ajili yako, mimi sitachukizwa kamwe. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, usiku huu kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu. Petro akamwambia, Ijaponipasa kufa nawe, sitakukana kamwe. Na wanafunzi wote wakasema vivyo hivyo. Kisha Yesu akaenda pamoja nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, hata niende kule nikaombe.Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka. Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe. Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu. Akaenda tena mara ya pili, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe. Akaja tena, akawakuta wamelala; maana macho yao yamekuwa mazito. Akawaacha tena, akaenda, akaomba mara ya tatu, akisema maneno yale yale.”
Yesu hakuuawa. Yesu alitoa uhai wake kwa hiari yake kamili. Ndivyo ilivyo - maana ndivyo Neno la Mungu linavyotueleza katika Maandiko Matakatifu, kwa mfano katika Kitabu cha Nabii Isaya, sura ya 53, aya ya 1 hadi ya 12:
Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani? Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani. Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote. Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake. Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeyasimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu. Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake. Lakini Bwana aliridhika kumchubua; Amemhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi, Na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake; Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki Atawafanya wengi kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu yao. Kwa hiyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu, Naye atagawanya nyara pamoja nao walio hodari; Kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa, Akahesabiwa pamoja na hao wakosao. Walakini alichukua dhambi za watu wengi, Na kuwaombea wakosaji.”
Neno hili la Mungu lapaswa kutimia ndani ya nafsi ya Yesu. Si kwamba Neno hilo ni kama shuruti inayotoka nje, bali ni hitaji la ndani la Bwana wetu linalomsukuma kwa hiari yake mwenyewe ili Neno hilo la Mungu lipate kutimia ndani yake. Yesu anatoa uhai wake, hakuna mtu anayemnyang’anya uhai huo!
Yesu amejitoa kafara kwa hiari yake kamili kwa ajili yetu. Jiulize, mwenzangu, wewe ni kafara kwa ajili ya nani katika maisha yako? Umemtolea nani uhai wako na maisha yako? Ikiwa wewe ni mtu wa ndoa, je, kweli umemtolea mwenzio wa ndoa uhai wako, maisha yako na vipaji vyako? Ukiwa padre au mtawa, je, umemtolea Yesu uhai wako, maisha yako na karama zako zote katika Kanisa lake takatifu?
Katika Bustani ya Gethsemane Mitume hawakufaulu mtihani wa urafiki wao na Yesu wakati wa majaribu na hatari. Walikimbia na kumwacha Yesu peke yake. Kwa nini? Kwa sababu hawakusali. Wao walikuwa wanapenda sana kujisifu mbele yake, eti, watafanya mambo mengi makuu kwa ajili ya Yesu, hata kutoa uhai wao kwa ajili yake, lakini ukweli ukawa tofauti kabisa. Walikimbia kwa sababu hawakuwa tayari kukaa na kusali pamoja na Yesu hata saa moja. Yesu hakudai kitu chochote kutoka kwao zaidi ya muda wa saa moja tu wa kukaa pamoja naye katika sala. Lakini hawakuwa tayari. Yesu akabaki mwenyewe kabisa.
Ndugu zangu, Mt. Yohane Paulo II hakuacha kuabudu Ekaristi Takatifu katika Ibada ya Saa Takatifu Alhamisi saa 2.00 hadi saa 3.00 usiku kila wiki katika maisha yake yote. Hakuacha hata mara moja. Ilikuwa haiwezekani kabisa afanye kitu kingine muda huo. Haiwezekani. Muda ulipokuwa unafika alikuwa anaenda kanisani na kukaa na Yesu kwa muda wa saa nzima.
Mungu anataka tuwe pamoja naye katika sala. Kutokana na namna tutakavyoenzi  ama kupuuza muda huo wa sala tutakuwa tunaishi kwa namna moja au nyingine. What we do and how we behave in our lives depends on time we dedicate to prayer. Petro asingelilala na badala yake angelisali pamoja na Yesu asingelihangaika na upanga wake, na wenzake wangelisali badala ya kulala, wasingelitoroka.
Sijui mnaweza kutenga muda gani kwa ajili ya sala kwa siku? Saa moja? Zaidi? Lakini kwa vyovyote vile ni lazima tutafute muda wa kutosha ambapo tutakuwa na Yesu tu na hatutafanya kitu kingine wakati huo. Tukiwa na Yesu peke yake.
Lakini tuseme ukweli - sisi kwa ujumla wetu tunapuuza sala, tunaidharau, tunafikiri tunapoteza muda kusali. Tunafiri muda huo hauna maana sana. Tena, tungeutumia muda huo kwa kufanya kazi na matendo mazuri ya kufaidi watu - tungefanya jambo la maana zaidi.
Martha anawahangaikia wageni nyumbani kwake na bado anamlaumu Mariamu kwamba hataki kumsaidia. Mariamu amechagua sehemu iliyo bora akiwa amekaa miguuni pake Yesu na kumsikiliza. Yesu anamwambia Martha kwamba kitu kimoja tu ni cha lazima - na Mariamu alikichagua. Kitu hicho ni kuwa na Yesu, kumsikiliza na kusali kwake.
Sisi hatuamini kwamba sala ni muhimu kabisa, tena ni nambari wani katika maisha yetu.
Tunaona yatokanayo na msimamo wetu huo wa kupuuza thamani ya sala katika maisha yetu na ya wenzetu. Mfano - fratera aliyesali kwa kufuata ratiba ya seminari kuu kwa miaka sita na zaidi, mara baada ya upadrisho wake anaacha upesi meditation na adoration, anaacha kusali breviari na kujitumbukiza katika shughuli, shughuli, shughuli tu. Badala ya kusali asubuhi, anasikiliza taarifa ya habari. Badala ya kusali Masifu ya Jioni au kufanya Lectio Divina  - taarifa ya habari kwenye runinga. Hilo haliachi hata kidogo. Tunakutana sisi Mapadre wakati wa mafungo, tunapewa vitabu vya breviari na Katibu wa Askofu maana Mapadre wenyewe hawajui hata waliweka breviari zao wapi. Ukiwatazama Mapadre, wengi hata hawana habari wapi watafute sala za siku hiyo. Wanahangaika kugeuzageuza kurasa au kutazama wengine. Picha hii inasikitisha sana. Lakini wakati huo huo kila mmoja wao ni mtalaam wa maswala ya kisiasa na matukio yanayojiri kila siku katika taarifa ya habari. Lakini habari za breviari waliyoapa kusali kwa uaminifu kila siku - hawana!
Masista wako tayari hata kurekebisha ratiba ya siku konventini endapo saa za kurusha tamthilia wanazozipenda zimebadilikakatika runinga. Wakiwa wanatazama wako makini sana, hawasinzii, wako focused kabisa, utafikiri wako katika ecstasy au contemplation ya hali ya juu. Lakini wakati wa sala, meditation, kuabudu - visingizio vingi vya kazi, kazi, kazi na kukosa vipindi vya sala kimoja, baadaye vingine na kadhalika. Na kukosa vipindi vya sala ya pamoja katika jumuiya zao. Mwisho ni anguko kubwa au neo-paganism.
Viongozi wangapi wa Utume wa Walei wana mazoea kushiriki Misa Takatifu kila siku parokiani, kuabudu Ekaristi, kusali Rozari, kujiunga na vyama vya kuchochea imani yetu? Wangapi? Makatekista wangapi ni wapenzi wa Misa za kila siku, ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu? Wangapi wanapenda kusali Rozari, kusoma na kutafakari Neno la Mungu (Lectio Divina)? Wangapi wanajiendeleza kwa kupenda kwao tu katika elimu dini na imani yao hai?
Majibu mnayo ninyi wenyewe. Majibu tunayo sisi wenyewe.
Na Yesu anatuambia jambo hili - kitu kimoja tu ni cha lazima katika maisha yetu - yaani kukaa naye kwa muda wa saa moja katika sala kila siku.
Matokeo ya kupuuza tamko hili la Yesu ni wazi. Unaongea na padre aliyeacha upadre, unaongea na mtawa aliyeacha utawa, unaongea na mlei aliyepotea katika Ukristo wake au katekista aliyeacha utume ama kugeuka kuwa katekista-kwazo, katekista-kituko. Na unaona kwamba ni watu ambao hawasali kwa namna hii anayotuambia Yesu - ya kukaa pamoja naye, kukesha pamoja naye, kusali pamoja naye kwa saa moja kila siku. Walikiacha kitu kile cha lazima na matokeo yake ni kubomoka kabisa na kupotea.
Tukitilia maanani maneno haya ya Yesu - “Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.” - hatutapotea kamwe katika maisha yetu na katika wito wetu. Hatutamsaliti Yesu wala hatutafanya mambo ya kijinga. 
Kuanzia sasa amua na umwombe Yesu akujalie neema ya kudumu katika sala miguuni pake kwa muda wa saa moja kila siku. Kongamano hili ni shule bora ya kutuweka katika njia mpya ya uhusiano wa karibu na Yesu Mfufuka katika maisha hai ya sala. Tusipoteze fursa hii ya kuanza upya kwa Kristo maisha yetu makini ya kiroho.

Neno la pili kutoka kwa Mungu wa Huruma linatujia kutoka Injili ya Mt. Yohane.
Yn 12:1-5:
Basi, siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alifika Bethania, alipokuwapo Lazaro, yeye ambaye Yesu alimfufua katika wafu. Basi wakamwandalia karamu huko; naye Martha akatumikia; na Lazaro alikuwa mmojawapo wa wale walioketi chakulani pamoja naye. Basi Mariamu akatwaa ratli ya marhamu ya nardo safi yenye thamani nyingi, akampaka Yesu miguu, akamfuta miguu kwa nywele zake. Nayo nyumba pia ikajaa harufu ya marhamu. Basi Yuda Iskariote, mmojawapo wa wanafunzi wake, ambaye ndiye atakaye kumsaliti, akasema, Mbona marhamu hii haikuuzwa kwa dinari mia tatu, wakapewa maskini?
Marhamu ya dinari mia tatu ni marashi yenye thamani ya mshahara wa mfanyakazi wa mwaka mzima. Ni nani kati yenu akina mama na akina dada mliopo hapa aliye na marashi ya gharama kama hiyo nyumbani kwake? Hakuna hata mmoja! Watalaam wa Maandiko Matakatifu wanasema kwamba tangu mwanzo wa Kanisa, marhamu hiyo ni ishara ya sala ya kikristo. Sala inayopaka miguu ya Yesu na kujaza mbingu kwa harufu nzuri na tamu.
Mariamu hakujali thamani ya marhamu hiyo. Alitumia yote kwa sababu alimpenda Yesu mno.
Yuda Iskariote na criticism yake ni sauti ya wengi wetu tunaoona muda tunaotumia kwa sala ni muda tunaopoteza bure, muda unaoharibika. Marhamu iuzwe na maskini wapewe fedha. Badala ya kuabudu Ekaristi tufanye mambo mengine yenye tija na manufaa kwetu. Badala ya sala, Misa ya Dominika, Misa za kila siku, ibada ya JNNK, sala za pamoja katika familia, breviari yetu sisi Mapadre na Watawa kwa namna ya pekee - tusikilize taarifa ya habari asubuhi na jioni. Breviari imejaa vumbi kwenye maktaba. Wanakwaya kufanya mazoezi wakati Misa ya jioni inaendelea Kanisani, wao wanaona ni kupoteza muda maana wanajiandaa kwa kurekodi au kwa sherehe muhimu.

Wengi wetu ni Yuda Iskariote wanaoona kutenga muda wa sala ni kuharibu muda, ni kupoteza muda… Wengi wetu tunawadharau Mapadre na Watawa na kusema - hawana kazi, wamekaa tu, hawajishughulishi na kazi za maendeleo. Eti, ni kusali tu. Bure kabisa hao! Lakini siku mtoto wako, mke wako, mume wako, ndugu yako akijaa mashetani na majini, ghafula unamwona Padre huyo uliyemdharau kwamba hana kazi, anakula tu na kulala — eti, ana faida, ni muhimu!
Ndugu yangu, unaanza kuwa mfuasi wa Bwana, unapoanza kuharibu na kupoteza muda wako kwa hiari, kwa makusudi, kwa moyo radhi na kwa upendo mkubwa kwa Bwana kwa ajili ya sala na ibada.  Kama unampenda Yesu kweli, utapenda na kukaa pamoja naye katika sala. Kama unampenda Yesu, muda wote wa wiki nzima wa Kongamano letu utaona kama sekunde iliyopita kasi na utasikitika kuwa muda umefika wa kurejea nyumbani. Kama humpendi Yesu, unamwona ni mzigo tu na maisha yako ya sala ni kavu na butu, kesho hutarudi tena hapa maana ukiwa hapa unaboreka na unapoteza muda, sivyo?
Naamini sisi sote tumefika hapa kwa kusudi la kuharibu na kupoteza muda wote wa wiki nzima kwa ajili ya Bwana - kwa furaha, kwa moyo radhi na kwa nia thabiti ya kukaa miguuni pake Yesu na kumsikiliza kwa makini ili Neno lake Hai lilete mapinduzi katika maisha yetu na utume wetu, tuweze kudhihirisha Uso wa Huruma wa Baba katika maisha yetu.
Neno la tatu la Mungu latoka katika Kitabu cha Nabii Mika.
Mi 7,14-15.18-20:
Walishe watu wako kwa fimbo yako, kundi la urithi wako, wakaao peke yao, mwituni katikati ya Karmeli; na walishe katika Bashani na Gileadi, kama siku za kale. Kama katika siku zile za kutoka kwako katika nchi ya Misri nitamwonyesha mambo ya ajabu. Mataifa wataona, na kuzitahayarikia nguvu zao zote; wataweka mikono yao juu ya vinywa vyao, masikio yao yatakuwa na uziwi (…) Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe uovu, na kuliachilia kosa la watu wa urithi wake waliosalia? Hashiki hasira yake milele, kwa maana yeye hufurahia rehema. Atarejea na kutuhurumia; atayakanyaga maovu yetu; nawe utazitupa dhambi zao zote katika vilindi vya bahari. Wewe utamtimilizia Yakobo kweli yako, na Ibrahimu rehema zako, ulizowaapia baba zetu tangu siku za kale.
Katika Neno hili la Mungu imefichwa Ahadi ya ajabu ya Mungu wa Huruma, ambaye anazitupa dhambi zetu katika vilindi vya bahari. Tena si bahari ama ziwa la kawaida, bali ni Bahari ya Huruma ya Mungu isiyo na mipaka. Tujaribu kuona kwa macho ya imani muujiza huu - tunamkabidhi Baba wa Huruma dhambi zetu naye hazitunzi wala haziandiki popote pale kwa ajili ya kumbukumbu za baadaye, bali anazitumbukiza zilivyo katika vilindi vya Bahari ya Huruma yake kama vile sisi tunavyotupa mawe baharini. Mawe ya dhambi zetu hayataibuka kamwe, yanabaki ndani ya vilindi vya Bahari ya Huruma ya Baba daima.
Ndivyo Baba wa Huruma anavyotusamehe dhambi zetu. Hakuna hata dhambi moja tulizotenda itakayomsababishia Baba yetu kwikwi ama kiungulio! Huu ndio utofauti wa msamaha wa Mungu na misamaha tunayotoa sisi. Maana sisi tunatunza kumbukumbu za makosa ya wengine juujuu - chini ya ngozi. Wakati wowote tunaziibua na kuwakumbushia waliotukosea. Kumbe, kamwe hatusahau na wakati mwingine hata msamaha wetu ni wa mdomo tu na si wa moyo. Baba wa Huruma anatumbukiza dhambi zetu ndani ya vilindi vya Bahari ya Huruma ya Mungu forever. Na haziwezi kujitokeza  tena kamwe. Game is over. 
Neno la nne la Mungu latoka katika Injili ya Mt. Mathayo 12,46-50:
Alipokuwa katika kusema na makutano, tazama, mama yake na ndugu zake walikuwa wakisimama nje, wataka kusema naye. Mtu mmoja akamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kusema nawe. Akajibu, akamwambia yule aliyempasha habari, Mama yangu ni nani? Na ndugu zangu ni akina nani? Akawanyoshea mkono wanafunzi wake, akasema, Tazama, Mama yangu na ndugu zangu! Kwa maana ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni, huyu ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.
Katika Somo hili tunafundishwa jinsi Yesu anavyogeuza umati wa wasikilizaji wasiofahamiana kuwa familia yake. Kwa tendo hili Yesu hamaanishi kwamba anamdharau Mamaye na ndugu zake wa damu. Hapana! Yesu anawakaribisha wasikae nje wakijali kundi lao na ukoo wao tu bali wajiunge na familia pana na mpya ya Yesu ya wapokeaji na watendaji wa Neno lake. Yesu anatufundisha hapo kwamba unaweza kuwa Mkristo mbatizwa, unaweza kumbeba Yesu mikononi mwako na moyoni mwako unapompokea katika Komunyo Takatifu, unaweza kudai kwamba unamjua, unaweza kuongea mengi na kuhubiri juu yake, lakini yote haya hayatakuwa na maana na hayatakubadilisha kwa ndani na kukufanya mwanafamilia wa Yesu endapo Neno lake Yesu halitatwaa mwili ndani mwako na kuzaa matunda. Wengi walimsikiliza Yesu, wangapi wakawa wafuasi wake na watendaji wa Neno lake?
Familia ya Mungu ni zaidi ya jumuiya ya watu. Familia ya kweli ya Mungu ni watu wanaojitambua kuwa kaka na dada wa Yesu. Sisi tuliopo hapa hatupaswi kujitambua kama umati tu uliokusanyika kwa ajili ya jambo fulani. Tujitazame hapa. Tunatoka katika mataifa na makabila mbalimbali. Tunafanana na watu waliokuwa wanajenga mnara Babeli. Tukitaka kugeuka kuwa familia ya Mungu katika Kongamano letu hili tunahitaji kukubali kuongozwa na Roho Mtakatifu - ambaye ni zawadi ya pekee ya Yesu Mfufuka kwa wafuasi wake. Katika Roho Mtakatifu pekee tunaweza kuwa familia moja ya Mungu. Hivyo tunahitaji sana kumtii Roho Mtakatifu siku zote.
Njoo Roho Mtakatifu, uifanye upya sura ya maisha yetu, mawazo yetu, maamuzi yetu, matendo yetu na mahusiano yetu! Ni Yeye tu mwenye uwezo wa kuondoa tofauti zetu na kutufanya kuwa kitu kimoja katika Kristo! Tukumbuke sote, ndugu zangu, kwamba Kanisa la Yesu ndilo linalosali kwanza, kisha linainjilisha. Si mtu mmoja mmoja anavyojisikia na anavyodhani kuwa anasukumwa na Roho wa Bwana. Hapana. Ukitaka kuwa mwinjilishaji kadiri ya Mapenzi na Maongozi ya Mungu, hauna budi kuwa kwanza mwanakanisa hai anayesali na kupenda kuharibu muda wake mwingi (kama dunia inavyodhani) kwa ajili ya sala, yaani kukaa miguuni pake Yesu Aliye Hai. Hauna budi kuwa ndani ya familia ya Yesu inayosikiliza na kutenda Neno lake - kwa kufaidiana na kwa pamoja.
Ndiyo maana tumekusanyika hapa pamoja kwa idhini ya Askofu wetu Mahalia ili Roho Mtakatifu atusaidie kutambua upya hadhi yetu, hulka yetu na fumbo letu la kuwa familia ya Mungu na Kanisa, yaani Mwili wa Kifumbo wa Bwana wetu Yesu Kristo. Na Roho huyo wa Huruma atufanye sote kuwa kweli wamoja kama familia ya Mungu na Kanisa la Kristo.
Baada ya kumaliza Kongamano letu, hatutaondoka hapa kama kundi la watu wanaotawanyika, kila mtu akienda zake na kufanya atakavyo. Hapana. Uinjilishaji si biashara binafsi ya mtu yeyote. Ni utume wa Kanisa zima. Kwa hiyo tutaondoka hapa kama Kanisa hai, tukidumu katika sala miguuni pake Yesu pamoja na Mama Bikira Maria na kufanya kazi ya Bwana ya uinjilishaji kwa pamoja kama Kanisa mahalia tukiongozwa na Maaskofu wa Majimbo yetu wanaomwakilisha Yesu Kristo Mfufuka katika familia yetu ya Mungu.
Tusali sana ili Mungu Roho Mtakatifu wa Huruma atushukie na atufanye kuwa familia hai ya Mungu wa Huruma. Tumwombe Yesu anyoshe mkono wake juu yetu na kutujalia amani na kutuvuvia Roho Mtakatifu, tupate kujawa Nguvu na Mwanga ule waliopewa wanafunzi wa Bwana siku ya Pentekoste.
Njoo, Roho Mtakatifu! Uifanye upya sura ya kila mmoja wetu, uifanye upya sura ya uinjilishaji katika Kanisa letu mahalia, uifanye upya sura ya Kanisa la Tanzania!
Kama muda unatosha - ukimya mtakatifu wa kitambo kidogo..
Tumwombe sasa Bwana wetu Yesu Kristo katika Fumbo la Ekaristi atujalie tunu bora ya amani yake na amtie Roho Mtakatifu rohoni mwetu ili awe mwalimu wetu wa ndani na kutufundisha kushika yote atakayotufundisha Yesu kupitia kwa watumishi wake wote wakati wa Kongamano letu na kuyatenda katika maisha yetu ya kila siku.

Sakramenti kubwa hiyo…

Chapisha Maoni

 
Top