araza la Maaskofu Katoliki Ufilippini baada ya kuhitimisha mkutano wake wa mwaka, linasema, litaendelea kusimama kidete: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu nchini humo. Maaskofu wataendelea pia kutekeleza dhamana na wajibu wao waliokabidhiwa na Kristo Yesu kwa kufundisha mambo ambayo ni haki na kuonya yale ambayo ni potofu katika maisha ya mwanadamu. Lengo si kushinda, bali ni kuendelea kusimama imara katika imani, maadili na utu wema, licha ya mawimbi magumu ya mashambulizi kutoka kila upande.
Hii ni changamoto iliyotolewa na Askofu mkuu Socrates B. Villegas, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini wakati alipokuwa anatoa hotuba elekezi kwenye mkutano mkuu wa 113 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini uliokuwa unafanyika Jimbo kuu la Manila. Maaskofu wamejiwekea mikakati ya shughuli za kichungaji kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia sasa pamoja kuanza maandalizi ya maadhimisho ya Kongamano la tatu la huruma ya Mungu kimataifa litakaloadhimishwa nchini humo kuanzia tarehe 16 – 20 Januari 2017.
Maaskofu wamejadiliana kwa kina na mapana hali ya kisiasa, kijamii na kiuchumi nchini humo baada ya ushindi na hatimaye kuanza kushika madaraka Rais Rodrigo Durtete kwa kusimika rasmi hapo tarehe 30 Juni 2016. Tangu mwanzo wa ushindi wake, Rais Durtete alianza kwa kutupa makombora ya shutuma dhidi ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini kiasi cha kutaka kurejesha tena nchini humo sheria ya hukumu ya kifo; udhibiti wa uzazi pamoja na kuwakata mikono watu watakaopatikana na hatia ya kujihusisha na biashara pamoja na matumizi ya dawa za kulevya.
Mambo haya yalipingwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini kwamba, yangelitumbukiza taifa katika utamaduni wa kifo usiothamini utu na heshima ya binadamu! Maaskofu hawakujibu shutuma zilizoelekezwa kwao na Rais Durtete na badala yake waliwaomba waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuwaombea viongozi wapya waliokabidhiwa dhamana na majukumu ya kuwaongoza wananchi wa Ufilippini baada ya uchaguzi mkuu.
Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo hata kama watawala watashindwa kulisikiliza kama ilivyojitokeza hata katika historia ya nchi, lakini ikumbukwe kwamba, wanao wajibu wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu mambo ambayo wanayatekeleza bila makunyanzi. Sheria ya uzazi salama inakumbatia utamaduni wa kifo unaofumbatwa na sera za utoaji mimba, jambo ambalo ni kinyume kabisa cha Injili ya uhai, utu na heshima ya binadamu!
Kanisa nchini Ufilippini litaendelea kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea maskini, wanyonge na watu wasiokuwa na sauti nchini Ufilippini bila woga wowote, hata kama utafika wakati ambapo watu watashindwa kusikiliza ukweli, lakini wao lazima wautangaze na kuushuhudia kwa nguvu zote. Hii itakuwa ni fursa makini kwa familia ya Mungu nchini humo kuweza kujitakasa na kujikita katika sala wakati inapopita kwenye Jangwa la mmong’onyoko wa maadili na utu wema; pale ambapo utamaduni wa kifo unakumbatiwa na kupigiwa debe la ushindi!
Huu ni wakati kwa familia ya Mungu nchini Ufilippini kuwa imara katika imani, pasi na kuyumbushwa hata kidogo na kwamba, waamini wanapaswa kurejea katika misingi ya imani na mafundisho ya Kanisa. Askofu mkuu Socrates B. Villegas anasema kwa misingi ya: Imani, Maadili na Utu wema, wako tayari kuandika historia ya nchi yao kwa wino wa damu, yaani hawana mchezo wako tayari kufa kifo dini kwa ajili ya ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Maaskofu Katoliki Ufilippini wataendelea kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa wakati unaofaa na wakati usiofaa! Wataendelea kuwaimarisha ndugu zao katika imani, matumaini na mapendo kwa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni