0
Mama Carmen Hernàndez, muasisi mwenza wa Chama cha Kitume cha Ukatekumeni mpya pamoja na Bwana Kiko Arguello, aliyefariki dunia Jumanne tarehe 19 Julai 2016 amezikwa Alhamisi, tarehe 21 Julai 2016 huko Madrid, Hispania katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu mkuu Carlos Osoro Sierra wa Jimbo Kuu la Madrid, Hispania.Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye maziko haya yaliyokuwa yanatangazwa moja kwa moja na Kituo cha Televisheni TV2000 kinachomilikiwa na kuendeshwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anasema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Mama Carmen Hernàndez, “mwanamke wa shoka” ambaye alikita maisha yake katika upendo kwa Kristo Yesu, akawa na ari na mwamko mkuu wa kimissionari.


Baba Mtakatifu anaendelea kueleza kwamba, wakati huu wa maombolezo anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa ndugu, jamaa na wanajumuiya wote wa Chama cha Kitume cha Ukatekumeni Mpya pamoja na wale wote walioguswa kwa namna mbali mbali na utume wake. Mi mwanamke aliyegundua na kuonesha umuhimu wa Sakramenti ya Ubatizo na majiundo endelevu ya waamini katika masuala ya imani.
Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa ushuhuda uliotolewa na Mama Hernàndez wakati wa uhai wake kwa kumpenda Kristo na Kanisa na kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu katika medani mbali mbali za maisha bila kuwasahau maskini na watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii!
Baba Mtakatifu anapenda kuiweka roho ya marehemu Mama Hernàndez chini ya wema na huruma ya Mungu, ili aweze kuipokea katika furaha ya Fumbo la Pasaka ya milele na anaendelea kuwatia shime wale wote waliobahatika kukutana na Mama Hernandes katika hija ya maisha yao pamoja na wanachama wote wa Ukatekumeni mpya kuendelea kuwa imara na thabiti katika ari na mwamko wa Uinjilishaji.
Baba Mtakatifu anawataka kujenga umoja na Maaskofu mahalia pamoja na Mapadre; huku wakionesha daima uvumilivu na huruma kwa wote. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaombea ulinzi na tunza ya Bikira Maria watu wote walioshiriki katika ibada ya mazishi ya Mama Carmen Hernàndez muasisi mwenza wa Chama cha Kitume cha Ukatekumeni mpya.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top