0
Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kufanya hija ya kitume nchini Georgia na Azerbaigian kuanzia tarehe 30 Septemba hadi tarehe 2 Oktoba 2016. Lengo la hija hii ya kitume anasema, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ni kuendelea kuhamasisha na kuimarisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa mataifa!



Kardinali Parolin katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano pamoja na mambo mengine anagusia: majadiliano ya kiekumene, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo huko Mashariki ya Kati; dhamana na wajibu wa dini katika mchakato wa ujenzi wa amani na utulivu; kinzani za Nagorino Karabakh bila kusahau changamoto ambayo imejitokeza kwa Jumuiya ya Ulaya baada ya Uingereza kujitenga na Umoja huo.
Kardinali Parolin anasema hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Armenia kuanzia tarehe 24- 26 Juni 2016 ilikuwa ni awamu ya kwanza ya hija ya kitume ambayo Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kuifanya katika eneo la Caucus ili kukoleza moyo wa majadiliano ya kidini na kiekumene. Baba Mtakatifu anataka kupandikiza mbegu ya amani katika nyoyo za watu itakayo zaa matunda kwa wakati kwa kutambua kwamba, eneo hili lina matatizo na changamoto zake ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi kwa njia ya ushirikiano na wote sanjari na kuonesha utashi wa kisiasa ili kuweza kupata ufumbuzi wa kudumu wa changamoto hizi.
Baba Mtakatifu anatembelea eneo la Caucus kwa unyenyekevu mkuu, akipania kusikiliza kwa makini, ili kufahamu na hatimaye kukoleza juhudi za majadiliano katika ukweli na uwazi pamoja na kujenga utamaduni wa kuthaminiana. Akiwa nchini Armenia, Baba Mtakatifu aliwataka wadau mbali mbali wanaohusika kwenye mgogoro wa Nagorno Karabakh kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, mgogoro huu unamalizwa kwa njia ya amani. Kikundi cha Minsk kilichoundwa na Shirikisho la OSCE, kimekuwa kikiendeleza majadiliano ili kufikia muafaka na hatimaye, amani kujerea tena katika eneo hili. Ni matumaini ya Kardinali Parolin kwamba, majadiliano haya yataweza kuzaa matunda yanayokusudiwa.
Kuhusu mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Karekin II, Kardinali Parolin anasema, Baba Mtakatifu kwa sasa anapenda kudumisha uekumene wa sala, huduma na ushuhuda wa maisha ya Kikristo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini wa kawaida kabisa. Baadaye, majadiliano haya yanaweza kukuzwa na kudumishwa na viongozi wa Makanisa.
Kumbe, majadiliano ya kiekumene ni mchakato unaopaswa kushika kasi kuanzia katika maisha ya waamini wa kawaida na baadaye kudumishwa katika majadiliano ya kitaalimungu ili viongozi wa Makanisa waweze kujikita zaidi katika mambo yale yanayowaunganisha Wakristo kuliko kuendeleza mipasuko ya kihistoria na kitaalimungu ambayo pengine imepitwa na wakati.
Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini Armenia alizungumzia kuhusu mauaji ya kimbari, kuonesha jinsi alivyoguswa na athari za utamaduni wa kifo na kwamba, hii iwe ni changamoto ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya uhai, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu anapenda kuwa ni chombo cha haki na amani; msamaha na upatanisho. Juhudi hizi zinaweza kuzaa matunda yanayokusudiwa kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; daima kwa kutafuta mafao ya wengi, ili kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.
Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo huko Mashariki ya Kati ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa anasema, Kardinali Parolin katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano. Wanasiasa wanapaswa kuonesha utashi wa kisiasa kwa kushirikiana katika majadiliano, ili kweli muafaka uweze kufikiwa. Viongozi wa kidini wana dhamana ya kuendeleza mchakato wa upatanisho, haki na msamaha, ili kujenga jamii inayosimikwa katika haki, amani na udugu kati ya watu.Waamini wajenge utamaduni wa kuheshimiana hata katika tofauti zao za kidini na kiimani, ili waamini wote kadiri ya dini na imani zao waweze kushiriki katika mchakato wa maendeleo endelevu: kiroho na kimwili. Wakristo huko Mashariki ya Kati wanateseka na kuuwawa; wanadhulumiwa na kunyanyaswa kana kwamba, wao ni raia wa daraja la pili huko Mashariki ya kati au wanatambulikana kama watu wa kuja! Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kushika hatamu ili haki, amani, utulivu, ustawi na maendeleo ya wengi yaanze kushika mkondo wake.
Kardinali Pietro Parolin anakaza kusema, leo hii Jumuiya ya Ulaya inapaswa kufanya upembuzi yakinifu ili kuonesha mshikamano wa karibu na wananchi wa Umoja wa Ulaya pamoja na kutafuta ufumbuzi wa kero zinazowasibu wananchi wake. Kipindi hiki cha mpasuko wa Umoja wa Ulaya kisaidie kukuza mchakato wa upatanisho kwa kuthamini umoja unaofumbatwa katika tofauti. Bara la Ulaya lijifunze kujenga utamaduni wa majadiliano pamoja na madaraja yanayowakutanisha watu na wala si kuta zinazowatenganisha na kuwanyanyasa watu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top