Kenya inatarajiwa kuwa ni mwenyeji wa mkutano wa familia Kanda ya Afrika utakaofanyika kuanzia tarehe 22- 24 Septemba 2016. Hili litakuwa ni jukwaa kwa ajili ya kuadhimisha ukuu na utakatifu wa familia ya Kiafrika, ili kweli familia za Kiafrika ziendelee kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Hayo yamesemwa na Anne Kioko, Rais wa Shirika la kuratibu maadhimisho ya familia Barani Afrika katika mahojiano maalum na Radio Waumini.
Kati ya mambo ambayo kwa sasa yanaendelea kutishia ukuu na utakatifu wa ndoa na familia ni utamaduni wa kifo unaokumbatiwa katika sera za utoaji mimba na usawa wa kijinsia mambo ambayo yanayonekana kupigiwa debe na Mashirika ya Kimataifa, lakini athari zake ni kubwa kwa familia Barani Afrika! Mama Kioko anasikitika kusema kwamba, ikiwa Bara la Afrika halitakuwa makini, linaweza kujikuta kwamba, tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinapokwa na Mashirika ya Kimataifa kwa kisingizio cha misaada. Somo la jinsia shuleni bado lina utata mkubwa kwa tunu msingi za maisha ya kifamilia kwani linafumbata ndani mwake utamaduni wa kifo, hali inayoweza kuhatarisha kanuni maadili na utu wema miongoni mwa watoto na vijana kwa siku za usoni. Mkutano huu wa familia unafanyika pia kwa ushiriki mkubwa wa Baraza la Maaskofu katoliki Kenya. Serikali ya Kenya na Vyama vya familia kutoka Cameroon na Nigeria.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni