Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya uhai, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Maisha ni zawadi kubwa ambayo binadamu amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu na kwamba, binadamu anapaswa kumrudishia kwa moyo wa shukrani, imani na mapendo!
Askofu Msonganzila ameyasema haya hivi karibuni wakati alipokuwa anaadhimisha Ibada ya Misa ya shukrani kwa kutimiza miaka 60 tangu alipozaliwa, mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kutokana na matendo yake makuu. Miaka 60 ya maisha ni baraka na neema inayomwingiza mtu kwenye kundi la heshima na hivyo kuwa ni kisima na chemchemi ya hekima, busara, neema na baraka.
Watanzania wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kudumisha mila, desturi na tamaduni njema zinazofumbatwa katika Injili ya uhai, huruma na mapendo. Tabia na mila zinazokumbatia utamaduni wa kifo zimepitwa na wakati na wala hazina nafasi tena katika maisha ya watanzania na wapenda amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Umefika wakati kwa waamini kuwa kweli ni vyombo vya haki, amani, upatanisho, msamaha na huruma inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu ili kuondokana na tabia za mauaji yanayoendelea kusikika mara kwa mara katika Ukanda wa Ziwa Victoria.
Watu wanapaswa kuheshimu utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mila za kukeketa wanawake zimepitwa na wakati kwani hizi ni chanzo cha majanga kwa wanawake wengi Mkoani Mara. Watanzania wajitahidi kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano, kama njia ya kujenga na kudumisha Ufalme wa Mungu duniani. Askofu Msonganzila amesema, ni dhamana na jukumu la viongozi wa Serikali na Kijamii kuhakikisha kwamba, wanatumia nafasi zao, ili kukuza umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.
Ukabila, udini na ubaguzi wa aina yoyote ule hauna tija wala mashiko kwa maendeleo ya watanzania. Umefika wakati kwa Serikali kuhakikisha kwamba, ahadi ya kutoa huduma bure ya matibabu kwa wazee inatekelezwa kwani uzee ni umri wenye changamoto nyingi za maisha. Ili kuhakikisha kwamba, Mapadre baada ya kulitumikia Kanisa kwa ari na moyo mkuu, wanaendelea kutunzwa na kuhudumiwa vyema wakati wa uzee wao, Jimbo Katoliki la Musoma, limeanzisha bima ya afya kwa ajili ya Mapadre wazee pamoja na kuwajengea mahali pazuri zaidi pa kuishi ili kufurahia Injili ya uhai, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Na Veronica Modest,
Jimbo Katoliki Musoma.
Chanzo cha habari ni http://sw.radiovaticana.va/news/2016/08/10/iweni_wahudumu_wa_injili_ya_uhai_dhidi_ya_utamaduni_wa_kifo!/1250525
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni