0
Na Joseph Sabinus
 “SALOME, binti wa Herodia aliingia ukumbini walimokaa, akaanza kucheza ngoma mbele yao.
Herode akapendezwa sana na wazee wote waliokuwamo humo ukumbini; akaapa kwa kiapo kumpa kitu chochote atakachotaka Salome, hata kama ni nusu ya Ufalme wake,” inasema sehemu ya masimulizi ya kisa cha kukatwa kichwa kwa Yohani Mbatizaji.
Masimulizi hayo yapo katika kitabu cha MAISHA YA WATAKATIFU, Uk. 300 kikifananua kuwa, zamani za Bwana Wetu Yesu Kristo, Herode aliyekuwa Mfalme wa Galilaya, alitoa amri ya kumkamata Yohani Mbatizaji, na kumfunga gerezani kwa shauri la Herodia.

 Inaelezwa kuwa, sababu ya kutolewa amri hiyo ni kwamba Yohani hakuogopa kumkaripia Herode na kumwambia, “Huna ruhusa kukaa na mke wa ndugu yako.” Kitabu hicho kilichopigwa chapa TMP mwaka 1996 kinasema, mwanamke huyo ndiye Herodia. Masimulizi mbalimbali kuhusu watakatifu yanabainisha kuwa, Herode hakuthubutu kumwua kwa kuwa Yohani Mbatizaji aliheshimiwa na watu wote kwa ajili ya utakatifu wake. Inaelezwa kuwa, ilipofika (birthday) siku ya kuzaliwa kwake, Herode aliitukuza na kuwaita wazee wa Ikulu ambao aliwafanyia karamu.
 Ndipo Salome binti wa Herodia alipoingia ukumbini walimokaa na kuanza kucheza mbele yao. Ndipo hapo alipopendezwa sana pamoja na wazee aliokuwa nao chumbani humo hata kumtaka Salome ataje kitu chochote anachokitaka; kwamba hata kama ni nusu ya ufalme wake; kwamba Herode alikuwa tayari kumpa. Chapisho hilo la Kanisa linasema, “Msichana (Salome) alitoka akamwambia mama yake, ‘Nitaomba nini?’.
Chapisho hilo linasema Herodia alimwambia, “Kichwa cha Yohani Mbatizaji.” Ndipo Salome aliporudi harakaharaka mezani na kunena, “Unipe sasa hivi katika sahani hii kichwa cha Yohani Mbtizaji.” Ndio mtihani mgumu uliomkumba Mfalme ghafla. Akasikitika sana rohoni.
Hata hivyo, angefanyaje wakati ni yeye mwenyewe aliyeapa kwa kiapo kumpa chochote alichotaka; hata kama ni nusu ya ufalme wake. Basi, kwa kuwa alikuwa ameapa mbele ya wageni wake, Mfalme akaogopa kukataa. Ikawa hivyo; Herode hakuwa na namna nyingine. Akamtuma mmoja wa askari wake kumkata kichwa Yohani Mbatizaji. Askari akafanya kama alivyoagizwa. Akatekeleza mauaji yale. Akamkata Yohani Mbatizaji kichwa na kukileta katika sinia. Wakaja wafuasi wa Yohani Mbatizaji wakauzika mwili wa Shahidi Mtakatifu huyu kwa heshima. Kitabu hicho kinasema, “Hatimaye, Mungu aliwaadhibu Herode na Herodia. Warumi waliwahamishia Ufaransa na hapo ndipo walipofariki dunia, mbali na nchi yao wenyewe.” Kimsingi, ukweli ndio uliomuua Yohani.
 Hii ni changamoto kwetu Wakristo kusimamia ukweli na haki hata pale ukweli huo unapobidi kutugharimu maisha kama ilivyokuwa kwa Yohani mbatizaji Katika siku hii ya kumbukumbu ya kukatwa kichwa kwa Yohani Mbatizaji Agosti 29, anakumbukwa pia Mwenyeheri Antoni wa Rivoli aliyekuwa Mfiadini wa Tunisia.
WATAKATIFU WA WIKI AGOSTI 23: Mtakatifu Rosa wa Lima na Mtakatifu Filipo Beniti aliyekuwa Padri. Mtakatifu mwingine wa Afrika anayekumbukwa katika siku hii ni Mtakatifu Teonas aliyekuwa Askofu wa Misri na Mtakatifu Viktori aliyekuwa Askofu wa Tunisia. AGOSTI 24: Mtakatifu Bartolomayo aliyekuwa Mtume.
 AGOSTI 25: Mtakatifu Ludoviko (Lui) wa Ufaransa pamoja na Mtakatifu Yosefu Kalasanzi aliyekuwa Padri na Mwanzilishi wa Shirika. AGOSTI 26: Mtakatifu Elizabeth Bishiye, Mwanzilishi wa Shirika pamoja na Mtakatifu wa Afrika Titoes aliyekuwa mwanamke Mtawa wa Misri. AGOSTI 27: Mtakatifu Monika pamoja na Mtakatifu Pastori aliyekuwa Abati wa Misri. AGOSTI 28: Mtakatifu Augustino aliyekuwa Askofu na Mwalimu wa Kanisa pamoja na Watakatifu wa Afrika akina Polienus, Serapion na Justilus waliokuwa Wafiadini pamoja na Mose wa Ethiopia aliyekuwa Mtawa wa Misri. AGOSTI 29: Kukatwa kichwa kwa Yohani Mbatizaji pamoja na kumbukumbu ya Mwenyeheri Antoni wa Rivoli aliyekuwa Mfiadini wa Tunisia.

Chanzo cha habari Gazeti la Kiongozi

Chapisha Maoni

 
Top