Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kuanzia tarehe 15 - 18 Septemba 2016 linaadhimisha Kongamano la XXVI la Ekaristi Takatifu Kitaifa, Jimbo kuu la Genova, Kaskazini mwa Italia kwa kuongozwa na kauli mbiu “Ekaristi Takatifu chemchemi ya utume: Kwa njia ya huruma yako, umekutana na wote”. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya amemteuwa Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kuwa mwakilishi wake maalum, wakati familia ya Mungu nchini Italia itakapokuwa inatafakari juu ya ukuu wa Fumbo la Ekaristi Takatifu kama kiini cha utume na maisha ya Kanisa.
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika ujumbe wake kwa maadhimisho haya linasema, hii ni nafasi muhimu sana kwa familia ya Mungu nchini Italia kufanya mang’amuzi juu ya Mwenyezi Mungu anayetoka ili kuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kwa njia ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Mwenyezi Mungu anajitoa sadaka na kuwa ni mkate unaomegwa kwa ajili ya maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko kwa waamini kujimega bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani kwa njia ya huduma makini, upendo na mshikamano wa dhati.
Kwa njia hii, waamini wataweza kuwa ni mashuhuda na vyombo vya upendo wa Mungu kwa jirani zao, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Maadhimisho ya Kongamano la XXVI la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia yanajikita katika hatua kuu nne za hija ambazo waamini wanatakiwa kuzitekeleza kama sehemu ya mchakato wa tafakari ya kina ili hatimaye, waweze kumwilisha kikamilifu maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa katika maisha yao ya kila siku.
Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika maadhimisho ya Kongamano la XXVI la Ekaristi Takatifu Kitaifa unajikita katika Sala ya Ekaristi ya Nne, sehemu muhimu sana na hitimisho la adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu. Ibada ya Misa Takatifu inawawezesha waamini kuonja uwepo endelevu wa Fumbo la Pasaka katika maisha ya waamini, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo; ufunuo wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Hii ni dhamana ya kutangaza na kushuhudia huruma hii katika maisha ya watu kwa njia ya Kanisa na kwamba, kila mwamini anapaswa kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimissionari katika maisha yake. Huruma ya Mungu iwe ni kikolezo cha utakatifu wa maisha!
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linakaza kusema, katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, waamini kwa namna ya pekee, wanaalikwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya furaha inayofumbata na kuambata huruma ya Mungu katika maisha yao, ili kupyaisha maisha na utume wa Kanisa nchini Italia. Lengo ni kuziwezesha Jumuiya za Kikristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Uinjilishaji mpya.
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema bila kusahau Jumuiya za Kikristo kuhakikisha kwamba, Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yanakuwa ni chachu inayopyaisha maisha ya mwamini binafsi na Jumuiya katika ujumla wake.
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kwa namna ya pekee, linawaalika waamini kutafakari kwa kina na mapana juu ya Ekaristi Takatifu na Utakatifu wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Waamini watafakari kuhusu Ekaristi Takatifu na utume wa Mwana wa Mungu ambaye kwa njia ya Fumbo la Pasaka kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ufunuo wa huruma ya Mungu amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, mwaliko kwa waamini kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa jirani zao na kama sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya Fumbo la Pasaka.
Wakristo wanatafakari pia Ekaristi Takatifu na Utume wa Roho Mtakatifu, tayari kupokea na kumwilisha karama na upendo wa Roho Mtakatifu katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho hizi ni Sakramenti za huruma ya Mungu. Kumbe, maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia ni nafasi ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwani kwa njia ya huruma yake, ameweza kukutana na wote.
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linawaalika waamini kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuwagusa kwa njia ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa kwa kutambua kwamba, mhusika mkuu katika Liturujia ya Kanisa ni Kristo, Kuhani mkuu na kwamba, waamini wanashiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Sakramenti za Kanisa linawawezesha waamini kwa njia ya imani kuweza kukutana na Mungu kwa njia ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.
Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa hayana budi kugusa na kutakatifuza maisha ya waamini, tayari kumshuhudia Kristo Yesu katika maisha yao ya kila siku ambao unapaswa kuwa kweli ni utenzi wa sifa na shukrani kwa utukufu wa Mungu. Ushiriki mkamilifu wa waamini katika Ibada ya Misa Takatifu, iwe ni fursa ya kumfuasa Kristo kiaminifu katika maisha, kama: Kiongozi, Mwalimu na Bwana. Ekaristi Takatifu isaidie kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimissionari ndani ya Kanisa, ili kuendeleza mchakatowa upyaisho. Neno la Mungu ni muhimu sana katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.
Hapa Wakleri wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanajiandaa kikamilifu ili kuwamegea watu wa Mungu utamu unaofumbatwa katika Neno la Mungu, tayari kulimwilisha katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama sehemu ya ujenzi wa ufalme wa Mungu. Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu yajenge na kukuza umoja, udugu na mshikamano miongoni mwa waamini ili kujenga Jumuiya inayoamini na kushuhudia utukufu wa Mungu katika maisha ya mwanadamu, ili kuweza kukutana na kushikamana na wote.
Hapa mkazo ni huduma makini ya upendo inayojikita katika ukarimu ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ekaristi Takatifu isaidie kuimarisha umoja na upendo wa familia kwa kujikita pia katika elimu, malezi na majiundo ya vijana wa kizazi kipya, ili wao pia waweze kuonja tunu msingi za Kiinjili. Ni changamoto pia ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote pamoja na kuthamini kazi kama utimilifu wa utu na heshima ya binadamu.
Familia ya Mungu nchini Italia inapojiandaa kuadhimisha Kongamano la XXVI la Ekaristi Takatifu Kitaifa huko Genova, Kasikazini mwa Italia inahamasishwa kutweka hadi kilindini, ili kuonja na hatimaye, kushuhudia huruma ya Mungu katika maisha yao, tayati hata wao kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu. Bikira Mari nyota ya bahari awaongoze waamini katika hija ya maisha huku wakiaadhimisha Mafumbo ya Kanisa, ili siku moja waweze kufika na kulakiwa nyumbani kw Baba wenye huruma.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni