Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, kunako mwaka 2015 limeadhimisha Jubilei ya miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Shirika hili kwa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa sadaka na majitoleo makubwa yalioshuhudiwa na Wamissionari hawa katika nchi mbali mbali duniani. Mwaka 2015 umekuwa ni mwaka wa neema na baraka kwa Tanzania, kwani katika maadhimisho haya, Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania likawa ni Kanda mpya chini ya Padre Chesco Peter Msaga.
Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Wamissionari wa damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania wanaadhimisha pia Jubilei ya miaka 50 ya uwepo na utume wao nchini Tanzania. Kutoka Manyoni, Jimbo Katoliki Singida, wamissionari hawa wakaenea Jimboni: Dodoma, Morogoro, Dar es Salaam, Mahenge na Ifakara. Baadhi yao wanafanya utume nchini Marekani, Guinea Bissau na Italia.
Kwa muda wa miaka 50 ya uwepo na utume wao nchini Tanzania, Wamissionari hawa wamekuwa kweli ni mashuhuda wa upatanisho unaobubujika kutoka katika tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo Yesu, dhamana wanayoitekeleza kwa njia maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa na huduma makini kwa familia ya Mungu nchini Tanzania hususan katika sekta elimu, afya, mawasiliano, maji na huduma kwa maskini. Wamissionari wanapenda kuandika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya uwepo na utume wao nchini Tanzania kwa wino wa machozi ya furaha na shukrani, hapo tarehe 18 Agosti 2016.
Miaka 50 si haba kama kiatu cha raba kama wanavyosema waswahili! Imekuwa na mafanikio pamoja na changamoto nyingi katika ukuaji na utoaji wa huduma kwa familia ya Mungu nchini Tanzania na kwamba, ndoto ya Mtakatifu Gaspar bado inaendelea! Kati ya matunda ya Miaka 50 ya Uwepo wa Wamissionari wa Damu Azizi nchini Tanzania ni Mapadre wazalendo: Felix Mushobozi na Pd. Onesphory Kayombo wanaoadhimisha Jubilei ya miaka 25 tangu walipopewa Daraja Takatifu la Upadre ili kuwamegea watu huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Neno, Sakramenti na huduma mbali mbali za kichungaji. Hawa walifungua mlango wa Wamissionari wazalendo kutoka Tanzania, leo hii, Shirika linajivunia matunda ya miito ya Upadre na Ubruda ndani ya Shirika, matendo makuu ya Mungu.
Padre Felix Mushobozi, C.PP.S. katika maisha na utume wake kama Padre ameihudumia familia ya Mungu ndani na nje ya Tanzania kama Paroko, Mkurugenzi wa miito, Jaalim, Katibu mkuu wa Vikarieti, Katibu mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu na hii ilikuwa ni mara ya kwanza katika historia ya Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu kuwa na kuwa Katibu mkuu wa kwanza kutoka Barani Afrika. Padre Felix bado anaendelea kulihudumia Kanisa la Kristo katika Tume ya haki na amani ya Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume nchini Italia.
Padre Onesphory Kayombo ni tunda la kwanza kabisa la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu kutoka Manyoni, Singida. Shirika linapoadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya uwepo na utume wake nchini Tanzania linamwangalia Padre Kayombo, maarufu kama Kalikenye kwa jicho la pekee. Na kutoka Manyoni, Shirika linaendelea kupata miito ya kimissionari, kielelezo cha ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Katika maisha na utume wake, amekuwa ni Paroko na Jaalim Seminari kuu ya Peramiho, Jimbo kuu la Songea.
Shirika linapowapongeza Mapadre hawa linapenda pia kumkaribisha Shemasi Marco Loth katika huduma ya kimissionari kama Padre kwani yeye naye atakuwa ni mwendelezo wa ndoto ya Mtakatifu Gaspar kwa familia ya Mungu nchini Tanzania. Sherehe hizi zinahudhuriwa pia na baadhi ya viongozi wa Shirika kutoka Kanda ya Italia na Wamissionari waliojisadaka kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita na leo hii, Shirika hili limekuwa kama lilivyo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni