0
Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Agosti anaadhimisha Sherehe ya Kung’ara kwa Bwana, kielelezo cha utimilifu wa Sheria na Unabii unaofumbatwa katika Kashfa ya Fumbo la Msalaba, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Kung’ara kwa Bwana ni tukio ambalo Kristo Yesu alilitumia ili kuweza kuwaimaarisha mitume wake, ili waweze kukabiliana na Kaskfa ya Msalaba, kielelezo makini cha: hekima ya Mungu, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu.

Mama Kanisa katika maadhimisho haya anaungama kwa dhati kabisa Ubinadamu na Umungu wa Kristo; Kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu na Mkombozi wa dunia sanjari na kuzaliwa kwa Kanisa Sakramenti ya wokovu kwa binadamu! Sherehe hii inagusa kwa namna ya pekee, umuhimu wa Kanisa kusimama kidete kulinda na kutunza kazi ya Uumbaji kama anavyokaza kusema Mtakatifu Damascene.
Yesu anaufunua Umungu wake kwa njia ya mwili uliotukuka, ndiyo maana Kanisa linamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa utukufu kwani ukuu una Yeye milele hata na milele! Ni ufunuo wa mwanga utakaozima giza la Kashfa ya Fumbo la Msalaba, tayari kutoa nafasi kwa binadamu kumwabudu, kumsifu, kumtukuza na kumwomba Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kabisa kuisikiliza sauti yake na kutekeleza mapenzi yake katika uhalisia wa maisha yake, kwani Neno la Mungu ni dira na mwongozo wa maisha.
Neno la Mungu ni Ufunuo wa utambulisho wa Mwana wa Mungu kama siku ile ya Ijumaa kuu atakavyosema yuke Akida kwamba, “kwa hakika huyu alikuwa ni Mwana wa Mungu”. Sherehe ya Kung’ara Bwana ni mwendelezo wa Siku kuu ya Ubatizo na Ukuu wa Fumbo la Msalaba na Mwanga unaong’ara katika maisha na utume wa Kanisa. Huu ni mwanga utakaojionesha kwa namna ya pekee, Siku ile Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho!
Kusikiliza ni sanaa inayohitaji majiundo makini na endelevu, mwaliko kwa waamini kumwomba Roho Mtakatifu ili awasaidie kuwa wasikivu wema na wazuri, tayari kumwilisha kile wanachokisikia kutoka katika dhamiri zao nyofu! Yesu kama ilivyokuwa kwa mitume wake wa karibu yaani: Petro, Yakobo na Yohane, Wakristo pia wanahamasishwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.
Huruma ya Mungu imefunuliwa kwa njia ya Maandiko Matakatifu katika Sheria na Unabii na kupata utimilifu wake katika Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipotwaa mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu na kuzaliwa kwake Bikira Maria. Wakristo wanatumwa kumshuhudia Kristo aliye teswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko kwa kutambua kwamba, daima Mwenyezi Mungu anaandama nao katika hija ya maisha yao. Sherehe ya kung’ara kwa Bwana ni chachu ya mabadiliko katika maisha kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu katika maisha!
Katika maadhimisho ya Sherehe ya Kung’ara Bwana, Kanisa  kwa mwaka huu, linafanya kumbu kumbu ya miaka 38 tangu Mwenyeheri Paulo VI alipofariki dunia akiwa kwenye Ikulu ndogo ya Castel Gandolf, nje kidogo ya mji wa Roma. Itakumbukwa kwamba, alitangazwa kuwa Mwenyeheri hapo tarehe 19 Oktoba 2014 na Baba Mtakatifu Francisko. Kanisa pia linakumbuka miaka XXIII tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wa kitume “Mng’ao wa Ukweli” “Veritatis Splendor” uliochapishwa kunako tarehe 6 Agosti 1993. Ni Waraka unaojikita katika mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu maadili na utu wema.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top