0
Ukweli ni uthibitisho wa kitu chochote au tukio lolote lile kadiri ya uhalisia wake. Kwa mfano ukweli kuhusiana na maji katika hali ya kimiminika ni kwamba yanapokutana na mteremko na hakuna kizuizi chochote basi yatatiririka kuelekea chini. Kwa maneno mengine ukweli unatupeleka katika kuutafakari ulimwengu huu kadiri ulivyopangwa na kuumbwa na Mwenyezi Mungu. Hivyo ukweli huo ambao huelezewa kwetu kwa njia ya neno lake unabaki daima kama ulivyo na kamwe hauwezi ukabadilika kama asemavyo Mungu kwa kinywa cha Nabii Isaya kwamba: “Majani yakauka, ua lanyauka; Bali neno la Mungu wetu litasimama milele” (Is 40:8).
Dhambi iliuondoa ukweli duniani. Katika hali ya dhambi mwanadamu anamuondoa Mwenyezi Mungu na hivyo kufiki na kutenda kadiri ya fikra zake ni si kadiri ya uhalisia wa jambo husika. Jamii ya mwanadamu leo inatuweka katika sura mbalimbali za ukweli juu ya jambo au kitu kimoja. Hii huonekana zaidi katika huria ya kimaadili. Jamii imekosa kielelezo na hivyo hakuna lengo wala moja mwisho mmoja. Matokeo yake ni mgawanyiko wa mawazo na kuzidi kumfifisha mwanadamu kuufikia ukweli unaomuusu yeye na ulimwengu unaomzunguka. Hali hii ya kutoambatana na ukweli inaendelea kufifisha uprndo kati ya binadamu na kati yao na Mwenyezi Mungu. Kila mmoja anajijengea ulimwengu wake na hivyo kuweka hali ya hatari katika mahusiano na kushirikiana kwa mwanadamu, tabia ambayo inapaswa kuwa ni asili ya ubinadamu wetu.
Utume wa Kristo ambao pia ndiyo utume wetu sisi unajengwa katika kuutangaza ukweli. Kristo anaonesha wazi kwamba utume huo ni sawa na kutupa moto. Moto ambao Kristo amekuja kuuwasha ni Roho Mtakatifu. Moto huo wa Roho Mtakatifu unapaswa kuwashwa ndani mwetu na kutufanya watangazaji wa matendo makuu ya Mungu kwa watu. Moto huo unapowashwa kwanza unakuwa ni ushahidi wa kazi za Mungu na hapo hapo unaleta mafarakano kwani ukinzani wa mkuu wa ulimwengu huu hautakubaliana na utendaji huu wa kazi za Mungu. Moto huo wa Roho Mtakatifu unatuelekeza katika njia moja na sote kuwa na kielelezo cha aina moja katika maisha yaani Kristo Bwana wetu aliye ufunuo wa ukweli wote. Ujio wake na kutupa moto kwake hapa ulimwenguni hakutatufanya kukaa kimya tu au kunyamaziana hasa katika uovu bali kutatufanya tugawanyike na hata kufarakana kwani hali ya upokeaji wa moto huo hutofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine.
Amani si ukimya tu na kutojishughulisha bali kukabiliana na changamoto za ulimwengu huu. Ndiyo maana Kristo anasema katika Injili kwamba sikuja kuleta amani. Ni utayari wa kukabiliana na changamoto zitakazotokana na uchocheaji wa moto uliowekwa na Kristo ndani mwetu. Mafundisho haya ya Kristo yanaweza yasieleweke. Maana mahali pengine anatuambia kwamba tujifunze kwake kwa kuwa Yeye ni mpole na mnyenyekevu wa moyo. Upole, unyenyekevu na amani ya Kristo si ule wa kutulia tu na kutofanya kitu. Upole wake haupatikani katika kutokutenda. Upole wake si katika kunyamazia ukweli wao kufifishwa bali unapaswa kuufunua ukweli kwa kutupa moto wa Roho Mtakatifu aliye kiongozi wetu na mwenye kutufunulia ukweli wote. Hivyo ufuasi wetu si katika kusawazisha na kuwa wakimya au kuunyamazia ukweli hata kama unayo nafasi ya kuukemea uovu huo.
Ustahimilivu hushinda katika ukweli. Mara nyingi tuutupapo moto huo wa Roho Mtakatifu ili kuupata ukweli huwa tunazusha migawanyiko na mafarakano. Ni nini sasa linapswa kuwa jibu la mfuasi wa Kristo? Ni kubaki katika ukweli ambao tumefunuliwa na tunauamini. “Tupige mbio kwa saburi tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu”. Nabii Yeremia anakuwa mfano mzuri kwetu kwa kuufunua ukweli na kustahimili katika ukweli huo kiasi kwamba anatupwa katika bwawa la matope ili aangamie lakini mwishoni wanatokea wa kumsaidia kwa maana Neno la Mungu linatuambia kwamba atakayevumilia hata mwisho huyo ataokoka.
Mahali pengine ambapo tunapata changamoto katika ukristo wetu ni katika kuusimamia ukweli kutokana na nafasi zetu mbalimbali za kijamii. Hii inaonekana katika nafasi iwe ni upande wa uongozi wa kijamii au upande wa wanaoongozwa. Msemo katika lugha ya Kiingereza unasema “call spade a spade” hutuamasisha katika kusimamia ukweli hata kama itahatarisha nafasi zetu au urafiki wetu na wengine. Mara ngapi tunakuwa wazito kusimama katika ukweli sababu tu ya kuogopa kupoteza ajira? Mara ngapi tunashabikia hata vitendo vya rushwa ambavyo hupindisha ukweli bila kujali athari inayoweza kutokea katika ubinadamu? Watu wengi wanafarakana katika ngazi za familia na hata katika jamii pengine kwa kunyamazia kwetu ukweli au kwa kuupindisha ukweli. Ufuasi wetu kwa Kristo unapata changamoto.
Moto wa Roho Mtakatifu umekwisha kuwashwa ndani mwetu kupitia Masakramenti na Neno la Mungu. Ni jukumu letu kama wafuasi kuchochea moto huo ili kutupeleka katika ukweli. Tuziamshe karama mbalimbali tulizojaliwa na Mungu kusudi utendaji wetu uendelee kuustawisha ukweli ulimwenguni. Ufuasi wetu unapaswa kustahimili katika ukweli kwa kuwa “ukweli ndiyo utatuweka katika uhuru wa kweli”, uhuru ambao unaturudishia hadhi yetu na kutufanya kutenda kadiri mpango wa mwenyezi Mungu.
Kutoka studio za Radio Vatican mimi ni Padre Joseph Peter Mosha
.Chanzo caha habari ni Radio Vatican.
Usiste kutembelea 
Kwa habari za kidini.  http://sw.radiovaticana.va/
                                             

Chapisha Maoni

 
Top