0
aba Mtakatifu Francisko kabla ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani, Jumapili tarehe 31 Julai 2016 alibariki na kuzindua nyumba mbili ambazo zimejengwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Poland kwa ajili ya wazee na maskini, kama kumbu kumbu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake ametafakari juu ya vikwazo vinavyoweza kuwakwamisha vijana na hivyo kushindwa kumwona Yesu kama ilivyokuwa kwa Zakayo mtoza ushuru.


Nia ya Yesu ni kutaka kumkaribia na kukutana na kila mtu katika safari ya maisha yake, ili maisha na Yesu na yale ya wafuasi wake yaweze kukutana na kuambatana! Zakayo alikuwa ni kiongozi wa watoza ushuru, mtu ambaye alikuwa anachukiwa sana na watu kutokana na kazi yake, hali ambayo ilimfanya ashindwe kumkaribia Yesu, lakini akaonesha ujasiri kwa kuvukwa vikwazo vyote na hatimaye, akafanikiwa kumwona na kumkaribisha Yesu nyumbani kwake, tukio ambalo lilileta mageuzi makubwa katika maisha yake.
Baba Mtakatifu anasema, Zakayo alikuwa ni mfupi kwa kimo, hali ambayo hata leo hii inaweza kuwafanya baadhi ya waamini kujiona kana kwamba, hawana sifa wala kustahili kuonana na Yesu, kishawishi kikubwa katika imani, kwani katika imani, waamini wanatambua kwamba wao ni watoto wapendwa wa Mungu, walioumbwa kwa sura na mfano wake na kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Yesu ameutwaa ubinadamu na Roho Mtakatifu anapenda kufanya makazi katika nyoyo za watu ili kuwakirimia furaha ya uzima wa milele.
Hapa Baba Mtakatifu anawataka vijana kujitambua, kujikubali na kutafuta mbinu za kuweza kupambana na vikwazo katika maisha pasi na kukata tamaa, ili kurutubisha ndoto ambayo Mwenyezi Mungu ameweka katika maisha ya kila kijana. Mwenyezi Mungu anawapenda watu wake jinsi walivyo na Yesu anawahakikishia watu wote kwamba ni watu wa maana, wenye thamani kubwa na kwamba, Mungu ana mpango nao.
Vijana wanapojisikia kukata tamaa na kushindwa kuangalia mbele kwa matumaini, watambue kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwaminifu katika upendo wake, atawasaidia vijana kujipenda kwani ana waamini kuliko hata vijana wenyewe wanavyojiamini; anawasubiri kwa matumaini hata pale wanapojifungia katika masikito na makosa waliyotenda siku za nyuma; mambo ambayo hayapaswi kupewa uzito mkubwa katika maisha ya kiroho, kwani hali hii ni sawa na kirusi kinachokwamisha mambo yote na hivyo kushindwa kuanza tena upya. Mwenyezi Mungu anapenda kuwaona vijana wakiwa wamesheheni furaha kwani anawapenda, kumbe, vijana wawe na ujasiri wa kumshukuru Mungu daima kwamba, anawapenda na kuwajali jinsi walivyo! Hiki ni kipindi cha kupenda ili kuweza kupendwa zaidi!
Baba Mtakatifu anasema Zakayo alishindwa kumwona Yesu kutokana na aibu iliyo mkata maini, lakini akapiga moyo konde, akaamua kupanda mtini ili kumwona Yesu. Alitambua cheo chake, lakini hakuona kuwa ni mali kitu, akashinda kishawishi hiki na kufanikiwa kumwona Yesu. Zakayo alivutwa na upendo wa Yesu moyoni mwake, licha ya dhambi na mapungufu yake ya kibinadamu, akafanikiwa kupata zawadi kubwa ya kukutana uso kwa uso na Yesu, kiasi hata cha kumkaribisha nyumbani kwake. Hii ndiyo siri ya moyo anasema Baba Mtakatifu kwa kuwataka vijana kutozima ndani mwao kipaji cha udadisi, Yesu anataka majibu ya uhakika katika maisha ya ujana!
Baba Mtakatifu anawaka vijana kujiaminisha kwa Kristo Yesu katika shida na mahangaiko yao kwa kukimbilia huruma na upendo wake unaofumbatwa katika Sakramenti za Kanisa, lakini kwa namna ya pekee kabisa, Sakramenti ya Upatanisho ambamo wataonja msamaha na amani ya ndani. Vijana wajiwekee lengo la kuwa na upendo kamili unaohitaji sadaka na majitoleo na kamwe wasitafute njia za mkato katika maisha kwa kutumbukia katika matumizi haramu ya dawa za kulevya.
Kizingiti cha tatu anasema Baba Mtakatifu ni minong’ono kuhusu maisha ya Zakayo mtoza ushuru, kiasi kwamba, watu waliona kwamba, Yesu alikuwa hastahili hata kidogo kuingia na kula kwenye nyumba ya mdhambi kama Zakayo! Wakasahau kuwa Yesu alikuwa ni ufunuo na chemchemi ya huruma ya Mungu inayowaangazia wema na wabaya katika hija ya maisha yao. Hii ni changamoto na mwaliko wa kuwa na nguvu ya kutenda mema zaidi badala ya kutumbukia katika ubaya.
Vijana wajitahidi kujivika fadhila ya upole, unyenyekavu na huruma. Kamwe wasikubali kutumbukizwa katika vita, chuki na uhasama; wasiwe ni watetezi wa ubinafsi na utaifa usiokuwa na mashiko, bali wawe kweli ni majembe ya matumaini na baraka kwa familia ya binadamu, kama inavyojionesha katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani!
Zakayo alidharauriwa na kubweza na watu, akainuliwa juu na Kristo Yesu kama “mlingoti wa bendera”, kwa kuona utu, ustawi na matarajio yake kwa siku za usoni. Vijana wajitahidi kuwa ni wajenzi wa umoja na mshikamano; wajitahidi kutafuta ustawi na maendeleo yao; wawe na moyo safi, waaminifu na watenda haki; wazame katika mambo msingi ya maisha badala ya kuendekeza liturujia zinazowatumbukiza katika malimwengu. Vijana wawe ni chemchemi ya wema na utakatifu wa maisha. Wawe ni vyombo vya furaha wanayosubiri watu wengi duniani!
Baba Mtakatifu anasema, Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yanaendelea katika maisha ya ujana, kwani bado Yesu anataka kukutana na kuambatana na vijana katika hija ya maisha yao: wakati wa masomo, kazi, urafiki, mikakati na ndoto ya maisha. Vijana watoe kipaumbele cha kwanza katika sala, tafakari ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa, ili kuweza kumshirikisha Yesu hija ya maisha ya ujana wao. Watambue kwamba, Yesu anawaita kila mmoja wao kwa jina lake! Vijana wajitahidi kujiaminisha kwa Mungu, kwani ni mwema na mwingi wa huruma na mapendo. Vijana watunze ndani mwao kumbu kumbu nzuri ya uaminifu na mema mengi ambayo wamefanikiwa kupata wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top