Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba mkutano mkuu wa Pili wa Mtandao wa Mashirika ya Kitawa Barani Ulaya dhidi ya biashara haramu ya binadamu na unyonyaji, RENATE kuanzia tarehe 7 – 11 Novemba 2016 itakuwa ni fursa ya kusali, kutafakari na kufanya upembuzi yakinifu, utakaozaa matunda kwa wakati wake. Huu ni mkutano unaofanyika mjini Roma, wakati huu, Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kipindi cha neema na mwaliko wa kuzama katika huruma ya Mungu, kama Wasamaria wema, ili kuganga na kuponya madonda ya mwanadamu katika ulimwengu mamboleo kwa mafuta ya huruma ya Mungu.
Baba Mtakatifu ameyasema haya, Jumatatu, tarehe 7 Novemba 2016 alipokutana na wajumbe wa mkutano mkuu wa RENATE uliofunguliwa rasmi mjini Roma. Biashara haramu ya binadamu ni kati ya mifumo ya utumwa mamboleo inayoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Vitendo hivi ni nyanyaso na dhuluma dhidi ya utu wa binadamu. Kumekuwepo na maendeleo makubwa katika ufahamu wa madhara yanayosababishwa na biashara haramu ya binadamu pamoja na kuwa na msimamo wa jumla utakaosaidia kuratibu nguvu za pamoja katika mapambano haya lakini bado kuna safari ndefu inayopaswa kutekelezwa. Ushirikiano wa dhati kutoka kwa Serikali, vyombo vya mahakama, watunga sera na sheria pamoja na wafanyakazi katika huduma za kijamii, wanapaswa kushirikiana na kushikamana kwa dhati ili kukomesha biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo duniani. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ni kazi ambayo inahitaji uragibishaji, elimu na uratibu makini, ili kuweza kukabiliana kikamilifu na tabia ya baadhi ya watu kutojali pamoja na unyeti wa biashara hii katika ujumla wake. Kutokana na mafao ya kiuchumi, mitandao ya kihalifu imeendelea kushamiri duniani. Kutokana na hali kama hii, Baba Mtakatifu anasema, anapenda kuwashukuru wajumbe katika mapambano haya ili kusaidia mchakato wa uragibishaji wa kijamii ili kupambana na janga hili katika maisha ya binadamu, linalowaathiri kwa namna ya pekee, wanawake na watoto.
Baba Mtakatifu anawashukuru kwa ushuhuda wao kama vyombo vya huruma ya Mungu, kwa kuwasaidia na kuwajengea uwezo waathirika ili kuanza tena kuandika ukurasa mpya wa maisha yao kwa matumaini zaidi. Shughuli hizi katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo zinawakumbusha wengi kazi na wajibu nyeti unaoendelea kutekelezwa na mashirika ya kitawa, hawa wanawake ili kuwarejeshea tena utu na heshima wale waliopokwa na wajanja wachache. Anawashukuru kwa kuwasaidia wanawake na watoto katika kuponya madonda ya maisha yao na kuwaingiza tena katika maisha na mfumo wa kijamii. Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa kusema kwamba, ana imani na matumaini makubwa katika ushirikishaji wa mwono na mang’amuzi yao; uelewa na ustawi; mambo ambayo yatasaidia mchakato wa ushuhuda wa Injili kwa watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii mamboleo. Wajumbe wote hawa wamewekwa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu pamoja na kuwahakikishia sala na sadaka yake katika huduma kwa maskini na wote wanaonyanyasika na kusukumizwa pembezoni mwa jamii.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Related Posts
- MAPADRI HESHIMUNI SADAKA ZA WAAMINI12 Jan 2018Maoni
PAROKO wa Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Kalmeli jimboni Morogoro Padri Vivian Menezes, amewaasa mapadri nchini kushika njia ya utakatifu na kutham...Read more »
- Kardinali Pengo: Jitahidini kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha12 Jan 2018Maoni
Yamekuwa ni mapokeo kwa Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam kutoa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi wa ...Read more »
- WAZAZI WAWE MAKINI NA VIPINDI VYA LUNINGA KWA WATOTO12 Jan 2018Maoni
Na Angela Kibwana, Morogoro ASKOFU wa Jimbo Katoliki Morogoro Mhashamu Telesphor Mkude amewaonya baadhi ya wazazi wenye tabia ya kuwaacha watoto ...Read more »
- Maaskofu watoa ujumbe wa Kwaresima 20111 Feb 2018Maoni
MAASKOFU 35 wanaounda Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania wametoa ujumbe wa Kwaresima kwa 2018, huku wakiwataka waamini wakatoliki wote kuuitik...Read more »
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni