Kiitikio hicho tunakifahamu sisi sote; tunaitikia mara nyingi lakini je, tunaelewa umuhimu wake? Binafsi nikichunguza wakati wa maadhimisho mbalimbali ya Liturujia hasa Adhimisho la Ekaristi, ni baadhi tu ya waamini wanaoitikia Aminasehemu mbalimbali wakati wa Misa. Waamini wengine huitikia kwa sauti ya kuungama dhambi na wengine hawaitikii kabisa.
Asili yake
Kwa asili Amina ni neno la kiebrania na maana yake ni: ni kweli kabisa. Neno hilo lililotumika kukubali au kuthibitisha ukweli wa maneno au jambo lililokuwa limesemwa. Kwa hiyo mtu aliyesema Amina alitakiwa kusikia nini kilichosemwa na ndipo akubalie: Amina.
Neno hilo limetumika katika Agano la Kale hasa katika Zaburi. Katika Agano Jipya Bwana Yesu alilitumia mara nyingi alipotaka kusisitiza siyo tu ukweli wa lile alilolisema bali pia uzito wake. Kwa namna hiyo Bwana Yesu alidhihirisha pia mamlaka yake katika lile alilosema.
Katika kitabu cha Ufunuo Yesu mwenyewe anaitwa Amina, kwani yeye ni mwaminifu kabisa katika maneno yake na kwamba yale anayosema kwa uhakika yatatimia. Tunasoma hivi: “Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina. Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli...” (Ufu 3:14). Yesu mwenyewe anajiita “njia, na ukweli na uzima” (Yn 14:6).
Katika Liturujia
Katika Liturujia yetu Amina ni kiitikio muhimu sana. Tunapoanza Sala zetu na kuhitimisha tunafanya Ishara ya Msalaba na kuitikia Amina.Tunaposema Aminatunasisitiza umuhimu wa kuanza Sala au Liturujia tunayoadhimisha kwa jina la Utatu Mtakatifu. Kwa Sala hiyo msingi tunautukuza Utatu Mtakatifu na kuomba utuongoze katika Liturujia yetu tunayoadhimisha au Sala yetu tunayoitoa. Kwa kupiga Ishara ya Msalaba tunajiweka mikononi mwa Utatu Mtakatifu tunapoanza Sala zetu au kuadhimisha Liturujia, na tunapomaliza tunapiga tena Ishara ya Msalaba na kusema Amina. Katika Adhimisho la Liturujia kwa kawaida kuhani huhitimisha kwa Baraka ndipo waamini hujiandika Ishara ya Msalaba.
Hata hivi katika Adhimisho moja la Liturujia kuna Sala mbalimbali ambazo kuhani au atazitamka kwa sauti peke yake kama mwongoza Adhimisho ili waamini wasikie na hatimaye waitikie Amina lakini kuna Sala ambazo kuhani hutakiwa kusali pamoja na waamini na wote watazihitimisha kwa pamoja kwa kiitikio hichohicho Amina. Tufuatane kuangalia Amina katika Adhimisho la Ekaristi, yaani Misa.
Mwanzo wa Misa
Mwanzoni kuhani huanza: Kwa Jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu. Kama tulivyosema hapo juu hii ni Sala ya msingi ambayo inatuweka mikononi mwa Utatu Mtakatifu tunapoanza kuadhimisha Liturujia yetu. Kuhani akishasema vile Wakristo wote wanatakiwa kuitikia Amina. Wale wasioitikia wanafanya kosa kubwa la kutokukiri imani kwamba tunajiweka mikononi mwa Utatu Mtakatifu. Wanatakiwa kujiuliza wamefika kanisani kufanya nini?
Kuhani huwasalimu waamini na kisha hutualika kukiri dhambi zetu. Hapo kuna namna mbalimbali za kukiri dhambi, lakini zote huishia na Sala anayotamka kuhani: Mungu mwenyezi atuhurumie, atusamehe dhambi zetu, atufikishe kwenye uzima wa milele. Waamini wote hutakiwa kuitikia Amina. Kwa nini wengine basi hawaitikii?
Hata hivi tukumbuke tendo hilo ni la kukiri dhambi na kuomba msamaha wa jumla katika kujiweka tayari kuadhimisha mafumbo matakatifu kama mwaliko wa kuhani unavyosema. Hiyo siyo nafasi ya Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho. Mkristo mwenye dhambi kubwa lazima aende kuungama kwa kuhani yaani padri au Askofu.
Baada ya tendo la kukiri dhambi na kuomba msamaha hufuata Utenzi wa Utukufu ambao huimbwa au kusemwa siyo na kwaya peke yao bali na waamini wote pamoja na kuhani. Utenzi huishia na Amina. Waamini wote pamoja na kuhani hukiri kwamba walivyoimba au kusali ni ukweli kabisa.
Sehemu ya Mwanzo wa Misa huhitimishwa na Sala iitwayo Kolekta, kutokana na neno la kilatini lenye maana ya kukusanya. Kuhani akishasema: Tuombe,inampasa kunyamaa kitambo ili kila Mkristo na kuhani mwenyewe wasali kimya ndipo kuhani ahitimishe maombi yao kwa sala iliyomo katika kitabu cha Misa. Sala anayosali kuhani ni kama inakusanya na kuhitimisha maombi ya Wakristo wote wanaoshiriki Misa hiyo. Mwishoni mwa Kolekta hiyo wote hutakiwa kuitikia Amina. Asiyeitikia huwaza nini moyoni mwake?
Liturujia ya Neno
Wakati wa Liturujia ya Neno, kabla ya Injili, kuhani hujiandaa kwa Sala fupi ili kutangaza Injili. Iwapo Misa huongozwa na Askofu, shemasi au padri iwapo shemasi hayuko huomba Baraka kwa Askofu. Anapopata Baraka hupiga ishara ya Msalaba na kutikia Amina.
Baada ya mahubiri, siku za Dominika na Sherehe hufuata Kanuni ya Imaniambayo, kama utenzi wa Utukufu kwa Mungu juu, huimbwa au husemwa na Wakristo wote, na mwishoni wote humaliza kwa Amina.
Tunapomaliza sehemu ya Liturujia ya Neno kuhani huwaalika waamini kusali: Salini ndugu, ili sadaka yangu na yenu ikubalike kwa Mungu Baba mwenyezi. Wakristo wakishasali hawasemi Amina kwa sababu kuhani huendelea mara na Sala iitwayo Sala juu ya Vipaji (oratio super oblata) ambayo ni ya kuombea dhabihu. Baada ya Sala hiyo ndipo Wakristo wote huitikia Amina.Tujibidishe kufanya vile.
Sala Kuu ya Ekaristi
Sala ya kuombea vipaji huhitimisha sehemu ya kuandaa vipaji. Hufuata Sala Kuu ya Ekaristi inayoanza na dayalojia: Bwana awe nanyi,... Inueni mioyo .. Mwishoni mwa Sala Kuu ya Ekaristi hufuata kiitikio cha Amina, ambayo huitwa Amina Kuu. Waamini wote hutakiwa kuitikia kwa nguvu Amina hiyo Kuu. Katika Sherehe waamini wote siyo kwaya peke yao, waimbe Amina mara tatu. Wanamuziki wazingatie hilo wakitunga muziki.
Baada ya Amina kuu hufuata sehemu ya kujiandaa kwa Komunyo Takatifu, inayoanza na Sala ya Bwana: Baba yetu uliye mbinguni. Baada ya sala hiyo hatuitikii Amina kwa sababu kuhani huendelea`mara :Ee Bwana, tunakuomba utuopoe ...hatimaye wote huitikia: Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu...
Hufuata mara Sala ya kuomba Amani ambayo kuhani husali na mwishoni wote huitikia Amina. Wakati wa kupokea Ekaristi kila Mkristo hutakiwa kuitikia Aminakabla ya kupokea Mwili wa Bwana. Ni tendo la kukiri imani kwamba unasadiki huo ni Mwili wa Kristo. Wote huitikia Amina mwishoni mwa Sala baada ya Komunyo.
Hatima
Mwishoni mwa Misa wakati kuhani anapowabariki waamini ndipo wote wakiinamisha vichwa vyao, hupiga Ishara ya Msalaba na kuitikia Amina ya mwisho.Wito kwa Wakristo wote: Tuitikie AMINA wakati wa Liturujia, bila kusita.Kwa kufanya vile tunashiriki na kusali na kuhani tena tunakiri imani yetu kwamba alivyotamka kuhani ninakubali, ni kweli kabisa na Sala hiyo huwa Sala yetu pia.
chanzo cha habari ni http://tec1956.blogspot.com/2016/09/amina-amina-amina-kiitikio-muhimu-sana.html
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni