0
Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, anaendelea na ziara yake nchini Malawi, akimwakilisha Baba Mtakatifu Francisko, katika tukio takatifu na la kihistoria kwa Kanisa nchini humo, la kutabaruku Kanisa Kuu jipya la Jimbo la Karonga. Siku ya jumamosi, 5 Novemba 2016, amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki wa Malawi, na ameeleza kwamba, anatambua waamini nchini humo wanazo changamoto nyingi za maisha, ikiwa ni pamoja na uhaba wa chakula unaosababishwa na ukame upande wa kaskazini na mafuriko upande wa kusini, myumbo wa uchumi, umaskini unaogusa wengi, huduma hafifu za jamii, majanga kama magonjwa ikiwemo Ukimwi. Pamoja na hayo, ameguswa sana na bidii na huduma zinazotolewa na Kanisa kwa upande wa elimu, afya na huduma za jamii, ili kupambana na changamoto hizo. Hii ni ishara njema na ya wazi ya Kanisa lililo hai na linalokuwa vizuri nchini Malawi.
Amewatia moyo maaskofu kuendelea na utume na huduma hizo, wakitambua kwamba ni katika huduma na utume huo, hasa kwa kujikita katika utume wa familia, wakiwa mababa na wachungaji, ndipo kila mmoja ataionja furaha ya Injili, kama anavyofafanua Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake ya Kitume Evangelii Gaudium, yaani Furaha ya Injili. Furaha hii inapatikana kutokana na kukutana na Kristo katika maisha, na kujenga mahusiano binafsi naye, furaha ambayo kiasilia humsukuma mkristo kuishiriki na wengine, ili wao pia waonje furaha hiyo ndani ya Kristo, na wote wakibaki katika umoja unaoponya, unaojenga na kukuza mahusiano kati ya watu. Hivyo ni muhimu kuzilinda familia, kuzitia nguvu, kwa kuhakikisha mahitaji, uhalisia na thamani yake vinapewa kipaumbele.
Akiwapongeza na kuwatia moyo katika utume, kahimiza waendeleze udugu, umoja,  mshikamano, uthabiti na ujasiri walio nao. Mambo ambayo yamewawezesha mpaka sasa kutetea haki za raia, kuboresha jamii yao na kukemea mambo yasiyofaa hata dhidi ya serikali. Katika kuendeleza haya yote, watapaswa kuzingatia ushirikiano mzuri pamoja na mapadri, watawa wa kike na wa kiume, na walei wote, ili kwa pamoja wawe na mtazamo na utendaji ulio sambamba. Zaidi sana kasisitiza waongeze nguvu katika kuwalea vema waseminari, ili kupata mapadri bora, walioandaliwa vizuri kitaaluma, kiutu, kiroho na kichungaji.
Na Padre Celestine Nyanda
Idhaa ya Kiswahili, Radio vatican

    Chapisha Maoni

     
    Top