Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni nafasi ya kutekeleza kwa dhati mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, waliotamani kuliona Kanisa kuwa ni Mama mpendelevu, mvumilivu na anayewaka moto wa mapendo kwa watoto wake waliojitenga na Msamaria mwema kwa watu wanaoteseka kiroho na kimwili! Kwa mwanga wa Roho Mtakatifu, Kanisa liwasaidie waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuona Uso wa huruma wa Baba wa milele!
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, huruma ya Mungu imeweza kuwafikia watu wengi zaidi kama ishara ya Ufalme wa Mungu ambao uko kati ya watu wake! Katika maadhimisho haya, Kanisa limeonesha kuwa ni Mama mvumilivu na mwingi wa huruma na mapendo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu: kiroho na kimwili, ili kuwaonesha watu hawa ushuhuda kwamba, Mungu kweli ni upendo na huruma ni jina na utambulisho wake. Hii ndiyo huruma inayojionesha katika mifano ya huruma ya Mungu katika Maandiko Matakatifu, ili waamini wajifunze kusamehe na kupokea msamaha kama vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu.
Hii inatokana na ukweli kwamba, huruma ni msingi thabiti wa uhai, maisha na utume wa Kanisa. Huruma ya Mungu ni kiini cha Uinjilishaji wa kina unaofumbatwa katika ushuhuda na upendo, kwani hii ndiyo changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo! Waamini wanakumbushwa kuwa na huruma kama Baba wa mbinguni alivyo na huruma!
Baba Mtakatifu Francisko katika mkesha wa kufunga rasmi Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Sherehe ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu, tukio ambalo linatanguliwa kwa Ibada ya kuwasimika Makardinali wapya walioteuliwa hivi karibuni kutoka sehemu mbali mbali za dunia anasema, Mwaka wa huruma ya Mungu ni utekelezaji wa mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanaokazia umuhimu wa huruma na majadiliano ya kiekumene, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, hadi miisho ya dunia, kama kielelezo cha imani tendaji!
Baba Mtakatifu ameyasema haya wakati wa mahojiano maalum na Gazeti la kila siku la “L’ Avvenire” linalomilikiwa na kuendeshwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Anakaza kusema, amemwachia Roho Mtakatifu afanye kazi ndani mwake kwani Kanisa ni shuhuda na chombo cha Habari Njema ya Wokovu na wala si mawazo yanayoelea kwenye ombwe! Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, anasamehe na kusahau, mambo makuu katika mafundisho ya Kanisa. Hii inatokana na ukweli kwamba, Neno wa Mungu amefanyika Huruma ya Mungu ili kuufunua Uso wa huruma ya Baba wa milele, changamoto ya kufanya mang’amuzi ya dhati katika maisha badala ya kumezwa na mapungufu peke yake.
Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, pale ambapo dhana ya ukosoaji inajikita katika ukweli na uwazi, inasaidia kuleta mabadiliko katika maisha ya watu, lakini ukosoaji usiokuwa na tija wala mashiko ni hatari kwa maisha na utume wa Kanisa kama inavyojitokeza katika Waraka wa furaha ya Upendo ndani ya familia, “Amoris laetitia”. Hali hii inaonesha kwamba, kuna baadhi ya watu ambao hawajaridhika na wala hawapendi kuona huruma na upendo wa Mungu unamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!
Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa linatumwa kuwa ni chombo na shuhuda wa huduma ya mapendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani maskini ni amana, hazina na utajiri wa Kanisa. Maskini, kimsingi ndio walengwa wa Habari Njema ya Wokovu dhamana inayopaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko anasema, maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani huko Lund nchini Sweden, kimsingi haya si matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, bali mwendelezo wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ulioanzishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili, takribani, miaka 50 iliyopita. Hija hii ya kiekumene, inakwenda “mwendo mdundo” na wala hakuna haraka, kwani mambo mazuri hayataki haraka!
Umoja wa Wakristo unafumbatwa katika mambo makuu matatu: kwa kutembea na kutekeleza kwa pamoja matendo ya huruma kwa maskini; kwa kusali na kuambata mambo msingi ya imani kama vile: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma. Hapa hakuna wongofu wa shuruti, bali watu wanavutwa kumwongokea Kristo na Kanisa lake kutokana na ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko na wala si vinginevyo! Baba Mtakatifu anasikitika kusema, utukufu wa Makanisa ni saratani mbaya, lakini kama ilivyokuwa kwa Martin Luther, Kanisa linapaswa kutenda kwa njia ya ushuhuda na huduma kwa maskini ili waweze kuona neema na baraka kutoka kwa Kristo Yesu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni