ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema kuwa, kufunga Yubilei ya Huruma ya Mungu ni kufungua upya Huruma ya Mungu kwa wanadamu.
Mwadhama ameeleza hayo hivi karibuni wakati wa Misa Takatifu ya kufunga Yubilei ya Huruma ya Mungu katika Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu.
“Tumefunga mwaka wa Huruma ya Mungu, ikiwa ni kufungua upya mahusiano yetu na Mungu. Ni kufungua milango ya Huruma ya Mungu kwetu sisi wanadamu na mahusiano kati ya mwanadamu na mwanadamu. Kujitambua kwamba sisi ni wakosefu na kwamba tunahitaji Huruma ya Mungu kwa unyenyekevu, "amesema Kardinali Pengo.
Aidha Kardinali Pengo amewaasa waamini kuwa, Yubilei ya Huruma ya Mungu kilikuwa kipindi cha kujifunga, kutafakari Huruma ya Mungu. Hivyo kufunga mwaka huo Mtakatifu haimaanishi kutupilia mbali Huruma ya Mungu, bali kuiishi kwa matendo yanayoonyesha kuwa wanatambua Huruma hiyo.
“Injili ya Luka inaonesha mfano wa watu wawili, mfarisayo na mtoza ushuru. Mfarisayo alijiona hahitaji Huruma ya Mungu hivyo ana mastahili zaidi kuliko mtoza ushuru. Akajigamba akisema anamshukuru Mungu kwani hayuko kama mtoza ushuru . Anasali, anafunga kuliko wenzake, mwishowe akarudi nyumbani akiwa hana haki mbele ya Mungu.
Mtoza ushuru alijiona mnyonge asiye na mastahili mbele ya Mungu hivyo akamuendea Mungu akijiona hana sifa ya kukaa mbele ya Mungu akaomba Mungu amsamehe dhambi zake. Yesu anasema aliondoka akiwa na haki mbele za Mungu zaidi kuliko mfarisayo.
Hiyo ndiyo maana ya Yubilei ya Huruma ya Mungu. Kujiona kuwa hatuna mastahili mbele ya Mungu. Tunahitaji kuomba Huruma ya Mungu na wanadamu wenzetu. Kuwa tayari kuomba msamaha na kutoa msamaha. Kuipa thamani Sakramenti ya kitubio.
Milango ya msamaha inafunguliwa upya katika Kanisa kwa ajili ya maisha yetu yote.
Kuja mbele ya Mungu na kusema, Ee Mungu unihurumie mimi ni mwenye dhambi. Anayejiona kinyume na hilo ni mfarisayo na anaishi kinyume bila neema ya Mungu,"ameeleza Kardinali Pengo.
Amewaasa waamini kuwa na huruma ya kuwasamehe wengine hasa wale waliowakosea vikubwa zaidi. Amesema kuwa kusamehe kunampa mwanadamu nafasi ya kuona kuwa hata yeye anahitaji kuhurumiwa na Mungu na wengine.
Amewaasa mapadri kuwa tayari kutoa Sakramenti ya kitubio kila siku na kwa muda wowote kwani milango ya Huruma ya Mungu imefunguliwa upya kwa wanadamu.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni