0
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya maadhimisho ya Jubilei ya Wafungwa Duniani kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Jumapili, tarehe 6 Novemba 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amelitafakari Fumbo la kifo na ufufuko wa wafu kama kielelezo cha mwendelezo wa mahusiano kati ya Mwenyezi Mungu na mwanadamu katika maisha ya uzima wa milele.
Yesu aliwaambia Masadukayo, wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala kuolewa. Mafundisho haya ya Yesu, yanawakumbusha waamini kwamba, hapa duniani ni wao ni wapita njia hawana makazi ya kudumu. Baada ya kifo, watakuwa na mahusiano mapya yaliyotukuzwa kadiri ya mpango wa Mungu. Ndoa ambayo ni alama ya upendo wa Mungu kwa binadamu itapyaishwa na kung’ara ili kufikia utimilifu wake katika maisha ya watakatifu walioko mbinguni!

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, wokovu na uzima wa milele si kwa ajili ya wateule wachache, bali ni mwaliko kwa watu wote. Maisha ya ufufuko wa wafu yatageuzwa kadiri ya mwanga wa Mungu na kwa kusimikwa katika furaha na amani ya milele. Maisha ya ufufuko wa wafu ni mwendelezo wa maisha safi na adili kutoka hapa duniani na kwamba, ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele ni kiini cha imani ya Kikristo kadiri ya ufunuo wa Maandiko Matakatifu. Imani katika ufufuo wa wafu ni muhimu sana kiasi kwamba, upendo wa Kikristo unamwagilia bustani ya Mungu itakayozaa matunda ya uzima wa milele.
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wafungwa duniani, amewataka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanaboresha maisha ya wafungwa gerezani, kwa kuheshimu utu wao kama binadamu. Adhabu inayotolewa kwa wavunja sheria iwapatie matumaini ya kuanza upya kuandika historia ya maisha yao kwa kurejea tena katika jamii wakiwa ni watu wapya zaidi. Kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, pale inapowezekana, wakuu wa nchi watoe msamaha kwa wafungwa wanaodhani kwamba, wanastahili msamaha huo!
Baba Mtakatifu amekumbusha kwamba, Itifaki ya Mkataba wa Paris, kuhusu mabadiliko ya tabianchi umeanza kutekelezwa na Jumuiya Kimataifa, changamoto na mwaliko kwa watu wote kushirikiana na kushikamana katika kulinda, kutetea na kutunza mazingira nyumba ya wote. Uchumi unapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu, ili kujenga na kudumisha haki na amani. Baba Mtakatifu amegusia pia mkutano kuhusu mabadiliko ya tabianchi unaoanza, Jumatatu huko Marrakec, Morocco unaopania pamoja na mambo mengine, kutekeleza itifaki ya Paris. Mchakato huu unapaswa kuongozwa na dhamiri ya uwajibikaji kwa ajili ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.
Baba Mtakatifu Francisko amegusia pia Wenyeheri wapya 38 kutoka Albania waliotangazwa kwenye Ibada ya Misa Takatifu, huko Albania. Hawa ni wale waliokumbana na pazia ya chuma kutoka kwenye Utawala wa Kikomunisti, lakini wakasimama kidete kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Ushuhuda wao ni nguvu inayowategemeza waamini katika shida na mahangaiko ya maisha sanjari na kuendelea kuambata wema, msamaha na amani.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top