Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 5 Novemba 2016 ameipongeza familia ya Asburg iliyokuwa inafanya hija ya kiroho mjini Roma, kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu amefafanua kuhusu dhana ya familia katika mapana yake, kwa kugusia utajiri, tofauti na tunu msingi za maisha ya kifamilia ambazo, watu wanapaswa kuzigundua na kuzisimamia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu!
Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na kumbu kumbu ya Jubilei ya miaka 100 tangu Mwenyeheri Carlo wa Austria alipotawazwa kuwa Mfalme wa Austria. Uwepo wake wa kiroho miongoni mwao ni mwaliko wa kuyatazama yaliyopita kwa ari na moyo mkuu, ili kuweza kukabiliana na changamoto na mahitaji ya nyakati. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza baadhi ya wanafamilia hawa ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kujenga na kudumisha mshikamano na maendeleo ya binadamu kiutu na kitamaduni pamoja na kuendelea kusimama kidete kudumisha mradi wa Ulaya unaojikita katika tunu msingi za kiutu na Kikristo!
Baba Mtakatifu anawapongeza vijana wa kizazi kipya katika familia hii ya kifalme, ambamo kumeibuka pia miito mitakatifu ya kipadre na maisha ya kitawa. Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu kwa kuiwezesha familia kuwa ni kitalu cha kwanza cha miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Maisha ya ndoa ni wito mtakatifu unaopaswa kuendelezwa na kudumishwa. Mfalme Carlo wa Austria alikuwa ni Baba mwema wa familia, mtunzaji bora wa Injili ya uhai na amani. Ni kiongozi aliyeonja adha ya vita, alipopigana vita kama Askari wa kawaida, mwanzoni mwa Vita kuu ya kwanza ya dunia.
Kunako mwaka 1916, akiwa makini kwa Sauti ya Kinabii kutoka kwa Papa Benedikto wa kumi na tano, Mfalme Carlo, akasimama kidete kulinda na kutetea amani hata kama aligundua mwishoni kwamba, watu wengi hawakumwelewa na hivyo wakamdhihaki, lakini bado anaendelea kuwa ni mfano bora wa kuigwa na mwombezi mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya amani duniani. Mwishoni, Baba Mtakatifu ameishukuru familia hii kwa kuihakikishia sala na sadaka yake katika safari ya maisha ya familia yao.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni