0
Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na Kituo cha Televisheni cha Tv2000 na Radio Inblu, vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anasema, ni vigumu sana kuweza kutoa tathmini ya jumla ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, uliofungwa rasmi kwa Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu, tukio ambalo limetanguliwa na kusimikwa kwa Makardinali wapya 17, “Majembe” ya Jubilei ya huruma ya Mungu. Hili limekuwa ni tukio la neema kwa Kanisa zima, kwani waamini kadiri ya nafasi na uwezo wao wameweza kuadhimisha mambo msingi ya imani ya Kanisa Katoliki yaani: huruma, msamaha, upatanisho na upendo; mambo yanayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.



Kwa ufupi, Baba Mtakatifu katika mahojiano haya na Bwana Paolo Ruffini mkurugenzi wa  Tv2000 na Lucio Brunelli, mkurugenzi wa habari anagusia kwa kina na mapana maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma kama kipindi cha toba, wongofu wa ndani; neema na baraka kwa watu wa Mungu. Huruma ya Mungu inapaswa kuwa ni chachu ya mageuzi katika maisha na utume wa Kanisa; mahusiano kati ya watu binafsi na jamii ya watu katika ujumla wake. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna watu bado wanataliwa kwa kiasi kikubwa na uchu wa mali na madaraka, kiasi kwamba, fedha imegeuzwa kuwa ni kipimo cha utu na ufanisi wa maendeleo ya mwanadamu na kusahau kwamba, fedha inapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu na wala si kumgeuza mwanadamu kuwa ni mtumwa wa fedha, matokeo yake ni utu na heshima ya binadamu kuwekwa rehani!
Baba Mtakatifu katika mahojiano haya anapembua kwa kina na mapana kuhusu huruma ya Mungu na haki; adhabu ya kifo na Injili ya Uhai. Licha ya ratiba, shughuli na utume wake anasema, kila siku anamwomba Mtakatifu Thomas More amsaidie kuwa ni mtu wa furaha na tabasamu kwa wale wote anaokutanana nao, ili kuwatangazia na kuwashuhudia furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, chemchemi ya furaha na lango la huruma ya Baba wa milele!
Kimsingi, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, yamewawezesha waamini wengi zaidi kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya Neno na Sakramenti za Kanisa, maisha ambayo yamemwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji. Toba na wongofu wa ndani ili kuambata utakatifu wa maisha ni changamoto kutoka kwa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, iliyovaliwa juga na Mwenyeheri Paulo VI na Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wao.
Matokeo ya safari hii ya maisha ya kiroho ni kutangazwa kwa Mtakatifu Faustina Kowalska sanjari na kuanzishwa kwa Jumapili ya huruma ya Mungu, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukimbilia chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake ili kuondokana na ubinafsi na uchoyo; mambo msingi katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Mbegu ya huruma na upendo wa Mungu imepandwa mioyoni na akilini mwa waamini, sasa ni wakati wao kuhakikisha kwamba, wanazaa matunda ya toba na wongofu wa ndani, huku wakiendelea kuambata na kushuhudia huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao!
Ijumaa ya huruma ya Mungu anasema Baba Mtakatifu, imemwezesha kukutana na watu walionyanyaswa na kudhalilishwa utu wao kutokana na utumwa mamboleo, biashara haramu ya binadamu; ukosefu wa fursa za ajira pamoja utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu kama vile wahamiaji na wakimbizi. Amekutana na waamini waliosimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya familia na uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kukataa katu katu dhana ya utoaji mimba. Amekutana na kushuhudia wagonjwa waliokuwa kufani, lakini bado wana matumaini na imani kwa Baba mwenye huruma.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa ni Jumuiya ya waamini wanaomzunguka Kristo Yesu na wala si majengo. Kanisa linajengwa na waamini wanaosimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo, kama kielelezo makini cha imani tendaji! Adui mkubwa wa Kanisa ni pale uchu wa mali na madaraka vinapoingia kwa kupitia mlango wa nyuma. Maskini ni hazina, amana na utajiri wa Kanisa, hawa ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu. Matendo ya huruma ndicho kigezo kikuu ambacho Kristo Yesu atakitumia Siku ya Hukumu ya Mwisho. Waamini wawe makini dhidi ya uchu wa mali na madaraka mambo ambayo yanaweza kuhatarisha hata maisha yao ya kiroho na kujikuta wametumbukia katika kiburi na ubinafsi. Lakini, ikumbukwe kwamba, haya ni mapambano endelevu katika maisha ya kiroho! Hakuna kulala hadi kieleweke!
Baba Mtakatifu anakiri kwa kusema kwamba, yeye ni kati ya wadhambi wanaopaswa daima kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho! Kama binadamu, mwamini na kiongozi wa Kanisa anakabiliwa na vishawishi mbali mbali ambavyo anapaswa kuvishinda kwa kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake, kwa kujiaminisha mbele ya Mungu. Waamini wanapaswa kujifunga kibwebwe kupambana na vishawishi katika maisha yao ili kudumu katika imani, matumaini na mapendo. Kiti cha huruma ya Mungu, yaani Sakramenti ya Upatanisho ni faraja ya roho inayomwezesha mwamini kupyaisha maisha yake.
Baba Mtakatifu anasema, huruma, upendo na haki kwa wafungwa ni jambo ambalo analipatia kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake. Licha ya makosa na udhaifu wao wa kibinadamu, lakini bado wanabaki kuwa ni watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni watu wenye haki na wajibu wao mbele ya jamii. Hawa ni watu wanaopaswa kujengewa matumaini ili waweze kutubu na kuongoka na kuwa ni watu wapya wanaporejea kwenye jamii baada ya kutumikia vifungo vyao. Adhabu ya kifo inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu na kwa hakika imepitwa na wakati! Kuna njia mbali mbali zinazoweza kutumika kwa ajili ya kuwasaidia wafungwa kulinda na kudumisha utu wao kama binadamu! Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuendelea kuwatembelea na kuwasaidia wafungwa katika shida na mahangaiko yao, kamwe wasiwaache kumezwa katika utupu na upweke wa maisha! Jubilei ya wafungwa iwe ni chachu ya kuwathamini na kuwaenzi wafungwa ili waweze kutubu na kuongoka!
Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, katika maisha yake anapenda daima kuwa ni chombo na shuhuda wa furaha ya Injili kwa watu anaokutana nao katika hija ya maisha na utume wake. Mapadre wawasaidie waamini wao kuonja furaha ya kuwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Kuwavumilia wasumbufu ni sehemu ya matendo ya huruma: kiroho, lakini wanafiki ni adui wakubwa wa maendeleo ya watu: kiroho na kimwili. Ikumbukwe kwamba, huruma inakwenda sanjari na haki, lakini haki bila huruma ni hatari kubwa katika ustawi na maendeleo ya watu kiroho. Haki na huruma ni chanda na pete, kamwe haviwezi kutenganishwa, kama Yesu mwenyewe anavyoshuhudia katika Injili kwa kumsamehe Zakayo mtoza ushuru, Madgalena mtenda dhambi; na mwanamke Msamaria! Huruma ni jina jingine la Mungu!
Baba Mtakatifu anasema, huruma ya Mungu ni mwarobaini wa kupambana na utamaduni wa kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; utamaduni wa kifo unaomwangalia mtu kutokana na mchango wake katika uzalishaji na ukuaji wa uchumi; uchu wa mali na madaraka usiothamini utu wala heshima ya binadamu. Matokeo yake ni biashara haramu ya silaha ambazo zimekuwa ni chanzo kikuu cha maafa kwa watu na mali zao. Yesu Kristo kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mateso na Kifo chake amewafunuliwa walimwengu Uso wa huruma ya Baba wa milele! Umefika wakati wa kujifunga kibwebwe kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaojikita katika ubinafsi. Maisha ya mwanadamu hayana tena thamani mbele ya wafanyabiashara wa silaha duniani!
Baba Mtakatifu Francisko anasema tarehe 17 Desemba 2016 ataadhimisha kumbu kumbu ya miaka 80 tangu alipozaliwa. Anamshukuru Mungu kwa zawadi ya Uhai anayoendelea kuipamba kwa sala, tafakari ya Neno la Mungu na matendo ya huruma. Anapata muda wa kulala vyema, jambo ambalo anamshukuru sana Mwenyezi Mungu. Anazo changamoto za maisha ya uzee na afya mgogoro, lakini kwa sasa anamshukuru Mungu na kwamba, anajitahidi kutenda kadiri ya uwezo na umri wake, neema na baraka kutoka kwa Mungu. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawapongeza wadau mbali mbali wa vyombo vya habari wanaoendelea kuinjilisha, kwa njia ya ushuhuda wa maisha ya Kikristo na Kanisa. Anavishukuru vyombo vya mawasiliano ya jamii kwa kuendelea kuwa ni sauti ya wanyonge na maskini wanaohitaji msaada wa hali na mali. Gonjwa kubwa na la hatari kwa watu wa nyakati hizi ni kutowajali wengine anasema Baba Mtakatifu Francisko!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top