Nyumba za Ibada si majukwaa ya malumbano ya kisiasa wala kampeni. Kuibuka tena kwa saratani ya rushwa na ufisadi nchini Kenya ni hali inayotishia amani na usalama wananchi. Kanisa linawashukuru wale wote wanaoendelea kujizatiti katika kuboresha mfumo wa elimu nchini Kenya na kwamba, wananchi washikamane ili kupambana na vitendo vya kigaidi vinavyohatarisha maisha na mafungamano ya kijamii nchini Kenya na kwamba, haki, amani, usalama na maridhiano ni mambo msingi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Sudan ya Kusini! Haya ni mambo msingi yaliyoandikwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika Waraka wao wa kichungaji kwa ajili ya familia ya Mungu nchini humo inayokabiliwa na changamoto katika medani mbali mbali za maisha. Wananchi wote wanawajibika kushikamana ili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa.
Safari ya wananchi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 ijikite katika misingi ya haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, ili kamwe wanasiasa wasiwatumbukize tena wananchi kwenye machafuko ya kisiasa na kijamii kama ilivyojitokeza kunako mwaka 2007- 2008 hadi leo athari zake bado zinajionesha kwenye jamii. Wasi wasi na hofu ya uchaguzi inaendelea kutanda nchini Kenya kutokana na ukabila, udini na migogoro kati ya wakulima na wafugaji. Kuna kinzani kati ya wafuasi wa chama tawala na vyama vya upinzani, zote hizi ni dalili za uchu wa madaraka, mambo yanayoweza kulitumbukiza taifa katika machafuko ya kisiasa na kijamii.
Maaskofu Katoliki Kenya wanalaani kwa nguvu zote vitendo vyote vya uvunjifu wa amani na kuitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti ili kurekebisha hali hizi. Wananchi wanakumbushwa kwamba, uchaguzi unakuja na kutoweka na kamwe wasikubali kutumiwa na wanasiasa uchwara kwa ajili ya mafao yao binafsi, bali wananchi wajikite katika misingi ya haki, amani na utulivu, ili kufanikisha mchakato mzima wa uchaguzi mkuu kwa mwaka 2017. Taasisi na wadau wote wanaohusika na mchakato wa uchaguzi mkuu wahakikishe kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao katika misingi ya ukweli, uwazi na mafao ya wengi, ili kuwa na uchaguzi huru na wa haki! Maaskofu wanaendelea kusema kwamba, malumbano, kinzani na mapigano kati ya viongozi ni jambo la aibu la wala halina mafao kwa ustawi na maendeleo ya wengi na badala yake linakwamisha mchakato wa maendeleo endelevu nchini Kenya.
Viongozi wameelemewa mno na ubinafsi kwa kujipatia misahahara minono, kwa kujikita katika udugu na ukabila pamoja na kuweka sahihi mikataba mibovu ili kulinda masilahi binafsi badala ya kuangalia mafao ya wananchi wote wa Kenya. Ni viongozi wenye uchu wa mali na madaraka na wala jukwaa la siasa si kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu nchini Kenya. Maaskofu wanawataka viongozi na wale wote wanaowania nafasi mbali mbali za uongozi kuhakikisha kwamba, wanajikita katika ukweli, uaminifu, kanuni maadili na utu wema; wanakuwa ni vyombo na wajenzi wa haki na amani; watu wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Kenya!
Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawataka wananchi wote kuachana na udini, ukabila au mahali anapotoka mtu kama kigezo muhimu cha kupewa kura; kwani mwelekeo wa namna hii ni hatari sana katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki,amani, maridhiano na mafungamano ya kijamii. Malumbano ya kisiasa na lugha chafu ni mambo ambayo hayana tija wala mashiko kwa wakati huu, badala yake viongozi wa namna hii, wajielekeze zaidi katika kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano.
Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawataka viongozi wa Kanisa kutojihusisha na masuala ya kampeni za uchaguzi, bali wawe ni alama ya umoja na mshikamano na kwamba, nyumba za ibada zisiwe ni majukwaa ya malumbano na kampeni za kisiasa. Kanisa linasikitika kuona tena kwamba, saratani ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma imeibuka kwa nguvu na kasi ya ajabu sana. Umefika wakati kwa wananchi, serikali na wadau mbali mbali kusimama kidete kupambana kufa na kupona na saratani ya rushwa na ufisadi; kwa kuwakamata na kuwashughulikia wakwepa kodi, ili Kenya iweze kushamiri na kustawi kwa maendeleo.
Viongozi wa Kanisa wanapenda kushiriki kikamilifu katika mapambano haya, ili watuhumiwa waweze kufikishwa kwenye vyombo vya haki na sheria iweze kushika mkondo wake. Kanisa linawashukuru na kuwapongeza wadau mbali mbali wanaoendelea kuboresha sekta ya elimu nchini Kenya kwa kuhakikisha kwamba, mitihani inafanyika katika misingi ya ukweli na uwazi, ili kuwafunda vijana wa kizazi kipya watakaowajibika katika mchakato wa ustawi na maendeleo ya nchi yao. Ubora wa elimu unaojikita katika tunu bora za maisha ya kiafrika, kiroho, kiutu na kimaadili ni muhimu sana kwa maendeleo ya taifa.
Ulinzi na usalama ni dhamana ya wananchi wote wa Kenya, hivyo wanapaswa kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, wanatokomeza vitendo vyote vya kigaidi vinavyoendelea kuhatarisha usalama wa maisha ya watu na mali zao. Ikumbukwe kwamba, vitendo vya kigaidi haviwezi kamwe kuleta suluhu ya matatizo na changamoto zinazowakabili wananchi na badala yake, vinataka kuwagawa wananchi wa Kenya kwa misingi ya udini; yaani: Wakristo na Waislam. Wananchi wakumbuke kwamba, kuna mambo mengi yanayowaunganisha kama Wakenya kuliko yale yanawaowagawa na kuwagombanisha. Viongozi wa Kanisa pia wanataka kuona haki, amani na maridhiano vinatawala nchini Sudan ya Kusini, dhamana ambayo imekuwa ikitekelezwa na Serikali ya Kenya.
Mwishoni, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasema kwamba, Ulinzi na usalama; ustawi na maendeleo ya wananchi wa Kenya viko mikononi mwa wananchi wenyewe. Kwa pamoja wanaweza kujenga nchi yao kwa kujikita katika utawala wa sheria, kanuni maadili na utu wema, ili kujenga na kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni