0
Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yamefungwa rasmi, lakini lango la huruma ya Mungu na katekesi makini kwa waamini ili waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu bado inaendelea! Kuwashauri wenye shaka na kuwafundisha wajinga ni kati ya matendo ya huruma: kiroho yanayoambatana na kushibana katika uhalisia wa maisha ya kawaida, ndani ya familia na jamii katika ujumla wake.


Kuwafundisha wajinga ni dhamana inayotekelezwa kimsingi na taasisi mbali mbali na inaratibiwa vyema, ili kuweza kufikia malengo yanayokusudiwa. Lakini hata leo hii, bado kuna mamillioni ya watoto ambao hawajabahatika kupata fursa ya kwenda shule ili kupata elimu bora itakayowajengea matumaini kwa siku za usoni. Ukosefu wa elimu makini unaathari zake pia hata kwa utu na heshima ya binadamu, kwani watu wasiokuwa na elimu wanaweza kutumbukizwa kwa urahisi katika nyanyaso na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo!
Hii ni sehemu ya Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 23 Novemba 2016 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Paulo VI ulioko mjini Vatican. Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika huduma kwenye sekta ya elimu kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, ili kuwarejeshea tena watu utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mtakatifu Justin ndiye aliyejenga shule ya kwanza kabisa mjini Roma kunako sehemu ya pili ya Karne ya pili, ili kuwafundisha watu Maandiko Matakatifu hadi wakati wa Mtakatifu Giuseppe Calasanzio aliyefungua shule za msingi bila malipo sehemu mbali mbali Barani Ulaya. Baadaye inafuatia litania ya watakatifu waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya elimu kwa vijana wa kizazi kipya, hasa miongoni mwa maskini kwa kutambua kwamba, elimu ilikuwa ni njia pekee ya kuweza kuvuka umaskini na ubaguzi wa aina mbali mbali.
Hawa ni watu waliotambua umuhimu wa matendo ya huruma kiasi cha kuyamwilisha na kuwa ni sehemu ya maisha yaliyoichachua Jamii na hatimaye kuweza kubadilika. Kwa kutumia miundo mbinu na rasilimali kidogo waliyokuwa nayo kwa wakati huo, wakafanikiwa kuwarejeshea watu wengi utu na heshima yao. Mfumo huu wa elimu ulilenga pia kuwapatia vijana fursa za kazi na matokeo yake ni kuanzishwa kwa shule nyingi za ufundi ili kuwapatia vijana ujuzi, maarifa na stadi za kazi pamoja na kuwafunda tunu msingi za maisha kiutu na Kikristo!. Utoaji wa elimu ni kielelezo cha mfumo makini wa Uinjilishaji.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, pale ambapo elimu inaendelea kuboreka zaidi watu wanakuwa na uhakika wa maisha na fahamu mbali mbali ambazo zinahitajika na wote katika maisha. Elimu bora inawafundisha watu mbinu makini za kukabiliana na changamoto za maisha; kwa kuonesha mashaka, kuuliza maswali na kuthamini matokeo yaliyofikiwa ili kuwa na uelewa mpana zaidi. Kuwashauri wenye mashaka ni msaada unaotolewa kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo; watu wenye hofu, wasi wasi na mashaka; mambo yanayomkandamiza mtu katika udhaifu na unyonge. Mashaka katika imani ni chachu muhimu sana ya kutaka kumfahamu Mungu, Kristo na Fumbo la Upendo wake katika maisha ya binadamu! Waamini wawe na ujasiri wa kuuliza maswali kuhusiana na imani yao, ili waweze kuifahamu kwa undani zaidi na hatimaye, kuvuka mashaka.
Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, ili kuondokana na mashaka ya kiimani, kuna haja ya kusoma na kulitafakari Neno la Mungu ili kutambua kile ambacho Mwenyezi Mungu anapenda kuwafundisha watu wake. Katekesi ni muhtasari wa: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Maisha ya Sala yanayotangazwa na kushuhudiwa katika  maisha ya mwamini na Jumuiya ya waamini katika ujumla wake, changamoto ni kumwilisha Imani hii katika matendo hususan katika huduma kwa jirani, lakini zaidi maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mashaka huweza kuondolewa na imani kusadifu kutokana uwepo wa Mwenyezi Mungu na Ukweli wa Kiinjili na upendo unaoishi ndani ya mioyo yao bila mastahili yao, ili kuwashirikisha wengine.
Baba Mtakatifu Francisko anasema: kuwashauri wenye shaka na kuwafundisha wajinga ni sehemu ya maisha ya kila siku na kwamba, kila mwamini anaweza kujitahidi kumwilisha sehemu hii ya Maandiko Matakatifu katika maisha yake, kwani Mwenyezi Mungu katika hekima yake amewaficha mambo haya watu wenye hekima na akili, akawafunulia watoto wachanga. Lakini fundisho kubwa zaidi ni kwamba, upendo wa Mungu unaweza kufukuzia mbali mashaka. Huu ni upendo pasi na makuu na umetolewa kwa daima jambo linalowawajibisha waamini ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa jirani zao.
Mwishoni mwa katekesi yake, Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa limefunga rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, lakini moyo wa huruma ya Mungu bado uko wazi na utaendelea kuwamiminia neema, mwaliko wa kuwa na nyoyo wazi pamoja na kuendelea kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha. Mang’amuzi ya upendo na msamaha wa Mungu wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni chachu ya upendo kwa Mungu na jirani!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

    Chapisha Maoni

     
    Top