Upendo usiomtambua Kristo kwamba amekuja katika mwili, akafanyika mwili, sio upendo ambao Mungu anawaamuru watu. Upendo wa namna hiyo ni upendo wa kidunia, wa kifalsafa, wa nadharia, upendo usio halisi, upendo laini laini. Upendo wa Mungu, ni upendo wa Neno aliyefanyika mwili. Anayefundisha upendo tofauti na huu, huyo atakuwa ni mpinga Kristo. Waamini wanapaswa kuishi na kuonesha upendo kama alivyofanya Kristo mwenyewe. Mafundisho haya ni sehemu ya mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Misa Takatifu, kwenye Kikanisa cha Mt. Martha, kilichoko mjini Vatican, siku ya Ijumaa, tarehe 11 Novemba 2016.
Kanisa ni jumuiya iliyo katika uwepo wa Kristo aliyefanyika mwili. Yeyote anayekwenda kinyume na fundisho la umwilisho hawezi kuwa na upendo wa kweli, upendo wa dhati, upendo kama wa Kristo. Walio kinyume na upendo uliofanyika mwili, huishia kuishi maisha ya nadharia, bila uhalisia ndani yao. Baadhi ya wanaoamini hivyo, hujikuta wanaishia kwenye maigizo ya huzuni, maigizo ya Mungu bila Kristo, Kristo bila Kanisa, na Kanisa bila watu. Baba Mtakatifu Francisko, anawaalika waamini kuomba pamoja naye, ili kujihadhari na upendo nadharia, bali wajaliwe kuwa na upendo wa kweli, upendo unaoshuhudia huruma ya Mungu. Waamini wajifunze kutoka kwa Mt. Laurent aliyesema: maskini ni hazina ya kanisa. Alisema hivyo sababu maskini ni mwili wa Kristo unaoteseka. Hivyo ni muhimu kuishi upendo na kujali maskini.
Na Padre Celestine Nyanda
Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni