0
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kitume “Dhamana ya Afrika” “Africae munus” anasema, Kanisa Barani Afrika linapaswa kuwa ni chemchemi ya upatanisho, haki na amani; masuala ambayo kimsingi yanagusa medani za kisiasa, lakini Kanisa pia linatambua wajibu wake katika mchakato mzima wa haki inayofumbata ukweli ili kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika amani, upendo na mshikamano wa kitaifa. Upendo unapaswa kuheshimu uadilifu na haki. Kanisa linatambua kwamba ni mhudumu wa ukweli na kwamba, huduma hii, italiweka huru.


Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu  Katoliki Kenya kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, imeamua kuunga mkono juhudi za Serikali ya Kenya katika kupambana na saratani ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma. Tume hii imeandika kitabu ambacho kimewasilishwa hivi karibuni kwa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika mapambano dhidi ya rushwa pamoja na hatua muhimu zinazopaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha kwamba, saratani ya rushwa inapatia mwarobaini ili kung’oa mizizi yake ambao kwa sasa inahatarisha amani, ustawi na mafungamano ya kijamii.
Kitabu hiki, kinaitaka familia ya Mungu nchini Kenya, kujikita katika kanuni maadili na utu wema mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayojikita katika misingi ya haki, amani, utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kukua na kukomaa kwa rushwa nchini Kenya ni matokeo ya kumong’onyoka kwa misingi bora ya maadili na utu wema na badala yake watu wameelemewa mno na malimwengu, ubinafsi, uchu wa mali na madaraka. Kumbe, umefika wakati kwa familia ya Mungu nchini Kenya, kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Tunu hizi msingi zimwilishwe katika maisha ya watu binafsi, wanafanyakazi wa umma n ahata katika sekta binafsi, kwani jamii isiyokuwa na maadili hiyo ni sawa na daladala iliyokatika usukani! Hatari kwa haki, amani, ustawi na mafao ya wengi!
Kitabu hiki ni matokeo ya shutuma nyingi kuhusiana na rushwa pamoja na ubadhirifu wa mali ya umma nchini Kenya. Kuna baadhi ya maafisa wa serikali na mashirika ya umma walikuwa wanajichote vigunia vya fedha za umma kwa mafao binafsi. Ni watu ambao wamesahau kwamba, fedha hii ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi na wala si kwa ajili ya kutunisha mifuko wa wajanja wachache. Wito wa Rais Uhuru Kenyatta kwa wananchi wote kujifunga kibwebwe ili kupambana na saratani ya rushwa ni wajibu fungamanishi wa kijamii, unaowahusisha wananchi wote pasi na ubaguzi.
Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linamshauri Rais Kenyatta kuhakikisha kwamba, anakula sahani moja na wala rushwa na mafisadi wa Kenya, ili wale wote wanaotuhumiwa, wasimamishwe kazi, uchunguzi ufanyike, ili haki iweze kutendeka na sheria ichukue mkondo wake. Viongozi walioteuliwa na Rais katika mapambano dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma wanapaswa kutekeleza wajibu wao kikamilifu kwani rushwa si tu kosa la jinai bali pia ni kielelezo cha kumong’onyoka kwa maadili na utu wema! 
Rushwa anasema Rais Kenyatta inatishia amani na usalama wa Kenya. Bwana Philip Kinisu, Kamishina wa kupambana na rushwa Kenya anasema theluthi tatu ya bajeti ya Serikali inapotea kutokana na rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma. Malipo hewa kwa wafanyakazi hewa pamoja na bei kubwa ya manunuzi ya vitu vya serikali ni kati ya dalili za kumong’onyoka kwa kwa maadili, sheria, kanuni na taratibu za kazi, mambo ambayo kamwe hayawezi kuendelea kufumbiwa macho wakati umma wa wananchi wa Kenya unaendelea kuteseka! Kitabu hiki kiliwasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta na Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya aliyekuwa ameandamana na Maaskofu pamoja na viongozi wakuu wa Tume ya Haki na Amani Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya.
Na Rose Achiego na kuhaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 

Chapisha Maoni

 
Top