Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake wakati wa Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, siku ya jumanne, tarehe 15 Novemba 2016, amewaalika waamini kuchukua tahadhari kuepuka kuwa watu vuguvugu. Kristo anawaonya, anawarekebisha na anawaamsha kila mara ili wasije kuwa vuguvugu. Hivyo ni muhimu kwa waamini kuepuka hatari hiyo na kufanya jitihada za kubaki motomoto katika imani.
Wapo baadhi wanaojiona kuwa na amani na utulivu kwa kujidanganya kwamba hawana hitaji lolote, wala hawamtendei yeyote ubaya, kiuhalisia ni utulivu danganyifu, sababu katika kujidanganya huko, Mungu hayupo mahali hapo, Mungu hayupo kati yao. Utulivu wa namna hii unawafanya waamini hawa kujiona matajiri, lakini wanakosa utajiri wa kweli ulio ndani ya Kristo, utajiri unaoendana na maisha ya msalaba, na mawimbi ya hapa na pale katika hija ya imani. Huu ndio utajiri wa kweli ndani ya Kristo.
Kristo anatambua hatari ya kuanguka katika uvuguvugu wa imani, kwa sababu hiyo anawakumbusha waamini kila wakati, anawaamsha kiimani, amesimama mlangoni akibisha hodi ili kuwaamsha, ili kujialika katika maisha yao, ili kuwafariji, ili kuwarekebisha. Baba Mtakatifu Francisko anasema ni jukumu la kila mwamini mbatizwa kujifunza kuchanganua sauti ya Kristo anapogonga hodi, kutambua anagonga hodi ili kujialika maishani mwao, ili kuwarekebisha, ili kuwafariji, au kuwashusha kutoka katika mahangaiko yao fulani au kutoka katika udanganyifu wa uvuguvugu.
Na Padre Celestine Nyanda
Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni