0
   Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli anasema, Mungu ni upendo na ni mwingi wa huruma na msamaha mambo ambayo yamefumbatwa kwa namna ya pekee katika Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Huu ni upendo unaoshuhudiwa katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwajali maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali za maisha.


Ni ushuhuda ambao ameonesha kwa kujali na kuthamini utu na heshima ya wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora Barani Ulaya kama ilivyojionesha wakati wa safari yake kwenye Visiwa vya Lesvos, nchini Ugiriki. Hawa ni watu wanaokufa maji kila kukicha kwenye bahari ya Mediterannia, kiasi kwamba, sauti ya kilio chao kwa sasa ni kero na usumbufu kwa Jumuiya ya Kimataifa! Lakini hawa ni watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu wanapaswa kuheshimiwa na kusaidiwa kwa hali na mali kama binadamu!
Patriaki Bartolomeo wa kwanza anayasema yote haya kwa kufanya tafakari ya kina mintarafu Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya upendo ndani ya familia” wosia ambao kimsingi unafumbata tunu msingi za Injili ya familia na maisha ya ndoa. Wakati viongozi hawa wawili walipotembelea kambi ya wakimbizi na wahamiaji huko Ugiriki, walikutana na nyuso za huzuni kutoka kwenye familia ambazo zimelazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na vita, kinzani na dhuluma mbali mbali changamoto kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanaunganisha uongozi na huduma kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wao na wala si vinginevyo!
Huduma na uongozi pia ni changamoto kwa waamini ili kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo kwa jirani zao. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume, Furaha ya upendo ndani ya familia anapembua kwa kina na mapana umuhimu wa upendo katika maisha na utume wa wanandoa na familia. Anagusia changamoto zinazowakabili wanandoa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia; malezi na makuzi ya watoto; talaka na changamoto ya ndoa za watu wa jinsia moja. Haya ni mambo yanayogusa undani wa utakatifu wa maisha ya mwanadamu na Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.
Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, katika miezi ya hivi karibuni, Wosia huu wa kitume umechambuliwa na kupepetwa kama mpunga ili kuangalia Mafundisho tanzu ya Kanisa, mchango wake katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji; mabadiliko yaliyojitokeza katika sheria za Kanisa na uelewa wake kwa wakati huu. Wakati huu, Mama Kanisa anapojiandaa kwa ajili ya kuadhimisha Fumbo la Umwilisho yaani Siku kuu ya Noeli, Neno wa Mungu alipofanyika mwili na kukaa kati ya watu wake katika mambo yote akawa sawa na binadamu isipokuwa hakutenda dhambi, ni wakati wa kutambua na kuenzi huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu na wala si kuangalia tu kanuni maadili na Sheria za Kanisa ambazo zimetungwa na binadamu wenyewe!
Ni kweli ulimwengu mamboleo una changamoto na matatizo yake mintarafu maisha ya ndoa na familia, lakini waamini wakumbuke kwamba, Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya: huruma, upendo na maisha! Mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume, “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Anafafanua kwa kina na mapana tasaufi ya maisha ya ndoa na familia katika ukweli na uwazi kwa kujikita katika huruma ya Mungu inayoganga na kuponya majeraha ya maisha ya mwanadamu. Kila mwanadamu anapendwa na kuthaminiwa na Mungu, kumbe, hakuna sababu msingi ya kumtenga mtu na huruma pamoja na upendo wa Mungu anakaza kusema Patriaki Bartolomeo wa kwanza.
Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anaendelea kuchambua Patriaki Bartolomeo wa kwanza, Baba Mtakatifu Francisko amebahatika kukutana na kuzungumza na familia za wakimbizi na wahamiaji, mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu. Papa Francisko anawaalika watu kujifunga kibwebwe ili kuwajibika kikamilifu kwa ajili ya wokovu wa roho zao wenyewe kwa kujikita katika Amri za Mungu, kanuni maadili na utu wema mambo yanayofumbatwa katika tasaufi ya maisha ya ndoa na familia.
Patriaki Bartolomeo wa kwanza anahitimisha tafakari yake kuhusu Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, Furaha ya upendo ndani ya familia kwa kusema udhaifu wa kibinadamu, usiwe ni kikwazo cha kusnindwa kumwilisha utimilifu wa huruma na umoja unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 

Chapisha Maoni

 
Top