0
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Alhamisi, jioni tarehe 22 Desemba 2016 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kituo cha Mshikamano nchini Italia kilichoko mjini Roma na kuzindua “nyumba ya Sara” iliyojengwa kwa ajili ya kuwasaidia wanawake wanaokabiliana na nyanyaso za kijinsia kama ilivyotokea kwa Sara di Pietrantronio, msichana aliyekuwa na umri wa miaka 22 aliyeuwawa kikatili na mchumba wake, mwezi Mei, 2015. Tukio hili limehudhuriwa na viongozi wa Serikali na Kanisa mjini Roma.


Kardinali Parolin katika mahubiri yake amesema, uzinduzi wa jengo hili ni mwendelezo wa maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu kwa maskini na watu wanaoishi pembezoni mwa jamii, changamoto na mwaliko wa kutubu, kumwongokea na hatimaye, kujipatanisha na Mungu, mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko. Ni wakati wa kusikiliza kilio cha watu wasiokuwa na hatia; wanaonyanyaswa na kudhulumiwa mali, hadhi, utu, upendo hata wakati mwingine kupokwa maisha.
Kuendelea kubaki kwenye njia ya uovu ni chemchemi ya udanganyifu na machungu katika maisha. Mwenyezi Mungu yuko daima tayari kusikiliza na kunyoosha mkono wake kwa wale wanaokimbilia ili kuambata huruma yake. Huu ndio muda uliokubalika wa kuachana na matumizi haramu ya dawa za kulevya, rushwa na ngono ili kurejea tena katika njia ya wema iliyooneshwa na Kristo Yesu anayebeba udhaifu na unyonge wa mwanadamu; Yesu anayeshiriki furaha na cheche za matumaini mapya kwani hakuna anayetengwa na upendo wake!
Kardinali Parolin anawapongeza wanawake na wasichana hawa ambao wameamua kuachana na matendo yanayowatumbukiza katika majanga ya maisha pamoja na kuwashukuru Wasamaria wema wanaojisadaka kwa ajili ya kutoa huduma makini kwenye Kituo cha Mshikamano Italia, mwendelezo wa ndoto iliyoanzishwa na Muasisi wa Kituo hiki Don Mario Picchi aliyetiwa shime na Mwenyeheri Paulo VI na Mtakatifu Yohane Paulo II na kwamba, Baba Mtakatifu Francisko yuko pamoja nao katika huduma kwa maskini katika hali ya unyenyekevu, ushuhuda unaotolewa na Bikira Maria katika maisha yake.
Kardinali Parolin anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufungua malango ya matumaini kwa watu wenye shida na mahangaiko mbali mbali kama vile: wakimbizi na wahamiaji; watu wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao kama ilivyokuwa hata kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuwa mkimbizi au mhamiaji si kosa la jinai, bali ni mwaliko wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.
Hiki ni kipindi cha huruma ya Mungu inayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kwa kuwapatia fursa wadhambi kutubu na kumwongokea Mungu. Ni muda uliokubalika wa kuondokana na biashara pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya yanayoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu kwa kuwazamisha vijana wengi katika msongo wa mawazo na kukata tamaa, wakati huo huo wahusika wakiendelea “kula kuku kwa mrija” kwa fedha inayonuka damu ya watu wasiokuwa na hatia!
Kanisa litaendelea kusimama kidete kupinga biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya sanjari na kuwasaidia wahusika ili waweze kuanza kuandika tena kurasa za maisha yao! Dhuluma, nyanyaso na mauaji ya wanawake ni vitendo ambavyo kamwe haviwezi kukubalika katika jamii anasema Kardinali Pietro Parolin. Wote hawa wanakumbukwa na kuombewa na Baba Mtakatifu Francisko ambaye pia anawatakia heri na baraka wakati huu wa maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli na Mwaka Mpya 2017.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top