Hivi ndivyo walivyoshuhudia Professa Francesco Miano na mkewe Giuseppina De Simone wakati wa kuzindua Wosia wa kitume wa Furaha ya upendo ndani ya familia. Wao wameshuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kama wanandoa Wakristo. Wanasema, Wosia huu unawaelekeza waamini kuzingatia mambo msingi katika maisha ya ndoa na familia katika lugha rahisi na inayoweza kufahamika na wengi. Wosia huu ni muhimu kwa wasomi, wafanyakazi, wataalam wa shughuli za kichungaji, lakini una umuhimu wa pekee sana kwa wanandoa wanaoshiriki kikamilifu katika kazi ya uumbaji kadiri ya mpango wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa, ili kujenga na kudumisha familia ya binadamu!
Professa Francesco na mkewe katika ushuhuda wao, wamejikita zaidi katika elimu na majiundo makini kwa watoto ndani ya familia. Hapa Baba Mtakatifu anawasindikiza wanandoa kutambua, kuonja na kushuhudia Injili ya familia inayosimikwa katika upendo wa dhati unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake kwa nyakati na mazingira mbali mbali. Wosia huu ni hazina na amana ya Kanisa kwa ajili ya familia, mwaliko na changamoto ya kutafakari kwa kina na mapana dhamana ya maisha ya ndoa na familia, ili kutambua uwepo endelevu wa Mwenyezi Mungu katika maisha na historia.
Baba Mtakatifu anazungumzia maisha ya kawaida kabisa ndani ya familia kwa kushirikisha uzoefu na mang’amuzi yake kama Mchungaji mkuu wa Kanisa. Huu ni muhtasari wa changamoto aliyoitoa kwa Mababa wa Sinodi wa kusikiliza kwa makini kilio cha familia ya binadamu, ili kujenga na kuimarisha familia kama Kanisa dogo la nyumbani, shule ya haki, utakatifu,ukarimu, upendo na maisha. Huu ndio mwelekeo mpya unaotolewa na Baba Mtakatifu kwa kuhakikisha kwamba, Kanisa linaambatana na waamini katika hija ya maisha yao ya kila siku, ili kuwaonesha dira na mwongozo wa kufuata katika kumwilisha Furaha ya upendo ndani ya familia.
Professa Francesco na mkewe ambao wameshiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi mbili za Maaskofu wanasema, maisha ya ndoa na familia ni safari inayojikita katika ukweli na uwazi; uaminifu na upendo wa dhati; mwaliko na changamoto ya kuwa na mwelekeo mpana zaidi pasi na kukata tama ya maisha pale wanandoa wanapokumbana na changamoto au kukumbwa na giza la maisha! Haya ni mambo ya kawaida, yanayopaswa kutafutiwa ufumbuzi kwa njia ya mwanga wa Injili ya furaha; huruma, upendo na msamaha wa kweli Wanandoa waendelee kuwa na ndoto nzuri zaidi za maisha, wawe tayari kumshukuru Mungu kwa wema na ukarimu wake; pamoja na ujasiri wa kuomba msamaha na huurma yake, pale wanapoteleza kuanguka katika udhaifu wao.
Wanandoa wawe ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo unaobubujika kutoka katika undani wa mioyo yao! Waamini wawe na ujasiri wa kutangaza na kushuhudia Furaha ya upendo ndani ya familia hasa katika ulimwengu mamboleo ambao umesheheni na kinzani, mipasuko na vita na magumu ya maisha! Furaha ya upendo iwaimarishe wanandoa wanaoteseka na kusumbuka kutokana na sababu mbali mbali za maisha; iwasaidie kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu.
Wanandoa waimarishe utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; wajenge mazoea ya kusikilizana kwa umakini mkubwa kile kinachotoka katika sakafu ya mioyo yao; waoneshe na kushuhudia ukomavu katika mahusiano ya ndani, daima wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa utajiri unaofumbatwa katika maisha yao ya ndoa na familia. Bila majadiliano ya kweli, familia zinashupaa na kusambaratika na hatimaye kupotea katika sura ya dunia kama umande wa asubuhi.
Wanandoa waoneshane upendo wa dhati pasi na unafiki, kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema pasi na dharau wala kubezana, kwani wote ni wamoja katika njia ya utakatifu wa maisha. Upendo hauna shaka katika mageuzi, upendo unaelimisha na kudumisha mahusiano ya ndani, ili daima upendo huu uweze kupyaishwa, vinginevyo, utaota kutu na kuzaa manung’uniko. Professa Francesco na mkewe wanampongeza Baba Mtakatifu kwa kuchambua kwa kina na mapana nafasi ya Baba na Mama katika wosia wake, bila kuwasahau wazee na majirani. Baba Mtakatifu anaonesha mwelekeo sahihi katika dhana ya kuwa mzazi, mtoto, ndugu au mzee, au wakwe!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni