0
Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini kwamba, maisha ya Kikristo ni mapambano endelevu dhidi ya vishawishi vinavyotaka kuwatumbukiza katika malimwengu kwa kuwaondoa katika njia sahihi inayowapeleka kwa Kristo Yesu. Ikumbukwe kwamba, Yesu amekuja hapa duniani ili kufutilia mbali nguvu ya giza na mauti pamoja na kumshikisha adabu shetani, baba wa maovu yote duniani.
Yesu katika maisha na utume wake, alifuatwa na makutano ya watu ili kusikiliza Neno la uzima lililokuwa linatolewa kwa mamlaka na kugusa hadi katika sakafu ya nyoyo za watu, kinyume kabisa cha Walimu wa sheria! Kuna baadhi ya watu walikwenda kumwona Yesu ili kujiridhisha wenyewe kuhusu wasi wasi uliokuwa umesheheni nyoyoni mwao na kudhani kwamba, Yesu alikuwa anakuja kuwapokonya nafasi za ajira! Lakini, watu wa kawaida walikuwa na kiu na hamu iliyokuwa inabubujika kutoka katika undani wao kwani walikuwa wanavutwa na Mungu Baba kumwendea Kristo Yesu, Mwanaye wa Pekee kwa njia ya Roho Mtakatifu ili aweze kuwafundisha Maneno ya uzima na kuwaponya na kuwaondolea dhambi zao.
Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 19 Januari 2017. Anaendelea kusema hawa ni watu waliokuwa wanagusa undani wa maisha na utume wa Kristo Yesu kiasi cha Yesu mwenyewe kuwaonea huruma na upendo kama kondoo wasiokuwa na mchungaji! Makundi ya kidadisi yaliyokuwa yananyemelea kuona matendo makuu ya Yesu, yalibaki yakipiga ukelele kwa kusema “Yesu ni Mwana wa Mungu”. Hii ndiyo hali halisi na ukweli kwa watu wanaomsogelea na kushibana na Yesu katika safari ya maisha yao hapa duniani!
Lakini hadi kufikia hatua, hii, kuna haja kwa Wakristo kujizatiti barabara dhidi ya nguvu za shetani, kwani maisha ya Kikristo ni mapambano endelevu dhidi ya nguvu za giza na shetani, hadi pale shetani atakaposhikishwa adabu na kuwekwa chini kama soli ya kiatu! Yesu amekuja ulimwenguni ili kupambana na shetani anayeendelea “kuwazingua”  waamini kutoka katika undani wa mioyo yao, lakini wakimtumainia Mungu atawasaidia kuwaelekeza mahali alipo Kristo Yesu. Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu anawataka waamini kusimama kidete kupambana na shetani ili kweli Kristo Yesu, aweze kupata ushindi katika maisha ya waamini. Mapambano haya yajikite katika huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; maisha ya sala, ibada na tafakari ya Neno la Mungu linalomwilisha katika uhalisia wa maisha ya watu! Haya ni mapambano yanayowawezesha waamini kuchagua njia njema inayowaelekeza watu kwa Kristo Yesu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.


Chapisha Maoni

 
Top