0
Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema Wosia wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya upendo ndani ya familia” “Amoris laetitia” ni dira na mwongozo wa utume wa familia unaoliwezesha Kanisa kutoka na kuwaendea watoto wake wanaoogelea katika shida, magumu na changamoto za maisha, tayari kuwaonjesha faraja na upendo kwa njia ya Neno na Sakramenti zake.
Hiki ni kielelezo cha Kanisa ambalo malango yake yako wazi, tayari kuwapokea na kuwahudumia wale wote wanaokimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kwa njia ya toba na wongofu wa ndani! Wosia huu wa kitume unajikita katika mambo makuu manne yaani: “kupokea, kusindikiza, kung’amua na kushirikisha. Hiki ni kiini cha ujumbe wa matumaini kwa familia zote hata zile ambazo zinaogelea katika kinzani na misigano ya kifamilia. Familia ambazo zina madonda na machungu ya maisha, zote hizi zinaalikwa na Baba Mtakatifu Francisko kujizatiti na kutembea katika mwanga wa imani na matumaini na kamwe zisikate wala kukatishwa tamaa na changamoto zinazoendelea kuibuliwa katika ulimwengu mamboleo!
Kardinali Baldiserri ameyasema haya hivi karibuni katika kongamano la utume wa familia lililofanyika hivi karibuni huko Civitavecchia, nchini Italia. Ametumia fursa hii kupembua kwa kina na mapana hija iliyofanywa na Mababa wa Sinodi ya familia kwa kipindi cha miaka miwili pamoja na kusindikizwa na katekesi ya kina kuhusu utume wa familia kama zilivyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko. Huu ndio mwelekeo mpya wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa unaohimizwa na Baba Mtakatifu Francisko.
Huu ni mchakato wa majadiliano ya familia ya Mungu katika ukweli na uwazi, ili kufikia maamuzi ya pamoja kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo, ili kupata na hatimaye, kutekeleza utashi wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa maneno mengine, haya ndiyo mang’amuzi ya pamoja yanayopaswa kuliongoza Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Mang’amuzi ya pamoja yamewasaidia Mababa wa Sinodi kukabiliana na changamoto, vikwazo na fursa zilizojitokeza katika kuibua, kupanga na kutekeleza sera na mikakati ya utume wa familia ndani ya Kanisa. Ni mchakato ambao unafumbatwa katika maisha ya kila siku siku ya watu wa familia; wakati wa raha na shida; wakati wa mwanga wa matumaini na giza la maisha!
Familia za Kikristo zinapaswa kujikita katika Sakramenti ya Ndoa, lakini pale upendo ndani ya familia haulingani wala kulandana tena na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; hapo Kanisa halina budi kuingilia kati ili kusaidia kuganga na kuponya madonda na machungu ya wanandoa, ili kuwasaidia tena kuona njia na Mwanga wa Injili, kwa kutambua kwamba, neema na baraka ya Mungu inawaandama daima, ikiwa kama watakuwa na ujasiri wa kuipokea na kuiambata! Mafundisho tanzu ya Kanisa yameimarishwa kwa kuzingatia kanuni za jumla pamoja na kuangalia hali halisi ya kila kesi inayojitokeza. Hapa hakuna njia ya mkato!
Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, Furaha ya upendo ndani ya familia unajadili kwa kina na mapana changamoto kubwa kwa wanandoa waliotalakiana; ushiriki wao katika Sakramenti ya Upatanisho na uwezekano wa kuruhusiwa kupokea Ekaristi Takatifu baada ya mchakato wa kina wa mang’amuzi, toba na wongofu wa ndani, ili kufikia ukomavu katika maisha ya kiroho. Kuwapokea na kuwasindikiza wanandoa hawa ni dhana inayopaswa kuwa ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa ndoa na familia.
Mababa wa Sinodi katika sala, tafakari na mang’amuzi yao, walikazia kwa namna ya pekee maandalizi ya wanandoa watarajiwa pamoja na kuweka mikakati ya kuwasindikiza hatua kwa hatua baada ya kufunga Ndoa, ili kweli waweze kuimarika kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, tayari kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa Injili ya familia, ambayo kimsingi ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya sala na utakatifu wa maisha. Mikakati ya kichungaji inapaswa kutafsiri huruma na upendo wa Mungu unaojionesha kwa waja wake, hasa wadhambi na wanyonge, wanaojibidisha kukimbilia na kuambata huruma na upendo wake katika maisha yao!
Mama Kanisa anataka kuwaendelea wale wote wanaoogelea katika dhambi na ubaya wa moyo kwa jicho la huruma na upendo wa Mungu; kwa kumwangalia mtu mmoja mmoja. Huu ndio urithi mkubwa na endelevu katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu uliohitimishwa hivi karibuni! Sinodi ambayo kimsingi ni safari ya pamoja inayofanywa na familia ya Mungu ni mchakato unaopaswa kumwilishwa na waamini wote, ili kweli kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kama kielelezo cha imani tendaji, anasema Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anapopembua kwa kina na mapana Wosia wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, Furaha ya upendo ndani ya familia!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top