Baba Mtakatifu Frsancisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Watoto Mashahidi waliouwawa kikatili na Mfalme Herode, iliyoadhimishwa na Mama Kanisa hapo tarehe 28 Desemba 2016 amewaandikia barua Maaskofu wote wa Kanisa Katoliki akiwataka wasimame kidete kulinda, kutetea na kudumisha maisha ya watoto dhidi ukatili wanaotendewa. Hapa kuna haja ya kuhakikisha kwamba, watoto hawatendewi tena ukatili, huu ni uamuzi wa kijasiri unaopaswa kutekeleza na Maaskofu sehemu mbali mbali za dunia!
Baba Mtakatifu anasema, Habari Njema ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo Mkombozi wa dunia inaonesha uwepo wa Mungu kati ya watu wake, chemchemi ya furaha na matumaini kwa waja wake. Liturujia ya Neno la Mungu katika kipindi cha Noeli, inawaingiza waamini katika kitovu cha Siku kuu ya Noeli, yaani Fumbo la Umwilisho, kiini cha furaha ya Wakristo. Kama ilivyokuwa kwa wachungaji kule kondeni, hata Wakristo katika ulimwengu mamboleo, wanahimizwa kuiendeleza furaha hii katika ukamilifu wake na kamwe wasiache furaha hii ipokwe kutoka kwao kwa kukosa matumaini na kudhani kwamba, mambo yote yanakwenda sawasawa!
Baba Mtakatifu anasikitika kusema, maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli kwa bahati mbaya yanaambatana pia na kilio hali inayopembuliwa kwa kina na mapana na Wainjili katika kipindi hiki cha Noeli. Kwa mtazamo wao makini, Noeli, hakikuwa ni kipindi cha kujificha kutoka katika ukweli wa mambo, changamoto na ukosefu wa haki kwa nyakati zile. Fumbo la kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu limekuwa pia ni sababu ya kilio na machungu kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale pale sauti iliposikika kutoka Rama, kilio na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake, asikubali kufarijiwa, kwa kuwa hawako!
Baba Mtakatifu anasema, hiki ni kilio cha akina mama wanao omboleza vifo vya watoto wao kutokana na upanga kama ule wa Mfalme Herode. Hiki ni kilio ambacho kinaendelea kusikika hata katika ulimwengu mamboleo na kamwe Maaskofu hawawezi kukinyamazia wala kukipatia kisogo! Huu ni ukweli usioweza kufumbiwa macho kwamba, kuna akina mama wanalia na kuwaombolezea watoto wao wasiokuwa na hatia! Huu ni mwaliko wa kufanya tafakari ya kina kuhusu Pango la Noeli sanjari na kujifunza kusikiliza kilio cha watoto wanaoendelea kuandika historia katika kurasa hizi chungu cha maisha yao.
Tafakari ya Pango la Noeli iwasaidie waamini kufanya rejea katika hali halisi ya maisha, ili kupata nguvu ya Habari Njema inayofumbatwa kwa Fumbo la kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu. Hakuna furaha ya kweli katika maisha ya Kikristo kwa kufumbia macho kilio, mateso na mahangaiko ya watoto wasiokuwa na hatia. Mtakatifu Yosefu aliitwa na Mwenyezi Mungu kulinda furaha ya wokovu dhidi ya ukatili mkubwa uliokuwa unatendeka kwa nyakati hizo. Huu ni mfano wa mtu mwaminifu, mtiifu na mwenye haki, aliyekuwa na uwezo wa kusikiliza sauti ya Mungu na kutekeleza dhamana na utume aliokabidhiwa na Baba wa milele! Akaisikiliza sauti hii kwa makini na kumwachia Mwenyezi Mungu nafasi ya kutekeleza utashi wake kwa kusoma alama za nyakati na kuyaangalia matukio ya wakati ule kwa jicho kavu!
Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hata viongozi wa Kanisa wanachangamotishwa kuwa kweli ni watu wenye uwezo wa kusikiliza sauti ya Mwenyezi Mungu ili kuguswa na uhalisia wa matukio yanayowazunguka na kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yosefu, kamwe wasikubali kupokwa furaha ya kweli! Wasimame kidete kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa akina Herode katika ulimwengu mamboleo. Wawe na ujasiri wa kukubali uhalisia wa mambo na kuufanyia kazi; ujasiri wa kuwalinda na kuwatunza watoto wasiokuwa na hatia! Unyofu wa watoto hawa unatupiliwa mbali kutokana na uzito wa kazi za suluba, utumwa mamboleo, biashara ya ngono, vita pamoja na uhamiaji wa nguvu unaoambatana na athari zake.
Baba Mtakatifu kwa uchungu anasema, watoto wengi wametumbukia kwenye mikono ya wahalifu na wafanyabiashara wa kimataifa wanaoendelea kupandikiza mbegu ya kifo ili kukidhi malengo na ubinafsi wao. Leo hii kutokana na vita, kuna watoto zaidi ya milioni 75 ambao wamenyimwa haki ya kupata elimu katika kipindi cha Mwaka 2015. Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 68% ya idadi ya watoto hawa wametumbukizwa katika biashara ya ngono duniani na kiasi cha watoto kilichobakia, kinafanyishwa kazi za suluba. Kuna kiasi kikubwa cha watoto wenye umri chini ya miaka 5 wanaofariki dunia kutokana utapiamlo wa kutisha.
Takwimu za Mwaka 2016 zinaonesha kwamba, watoto milioni 150 wamefanyishwa kazi za suluba kwa kuishi katika mazingira hatarishi! Takwimu za Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, zinaonesha kwamba kama hakutakuwepo na mabadiliko, ifikapo mwaka 2030 watoto zaidi ya milioni 167 watakuwa wanaishi katika hali ya umaskini wa kutupwa; watoto milioni 69 walioko chini ya umri wa miaka 5 watafariki dunia na wengine zaidi ya milioni 60 hawatapa nafasi ya kupata elimu ya msingi kati mwaka 2016 hadi mwaka 2030.
Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu Katoliki kusikiliza kilio cha Mama Kanisa anayesikitika sana na vitendo vya nyanyaso za kijinsia zilizofanywa dhidi ya watoto wadogo na Wakleri ndani ya Kanisa. Hii ni dhambi ambayo inaleta aibu kubwa kwa Kanisa! Hawa ni watu waliokuwa na dhamana ya kuwalinda na kuwahudumia watoto hao, lakini tamaa ya mwili, imewapelekea kiasi hata cha kuharibu utu na heshima ya watoto hawa, Kanisa linaomba msamaha kwa vitendo hivi. Maaskofu wanapaswa pia kusikitishwa na kuguswa na dhambi ya kutokutimiza wajibu na kuwahudumia waathirika wa nyanyaso za kijinsia; dhambi ya kuficha na kutokubali uwepo wa nyanyaso hizi pamoja na dhambi ya kutumia vibaya madaraka; Kanisa linalia sana na kuomba msamaha. Kumbe, kuna haja ya kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, vitendo vya haina hii havirudiwi tena, kwa kutumia kila njia ili kuhakikisha kwamba watoto wanalindwa kikamilifu na kwamba, kusiwepo hata kidogo na mtoto anayenyanyaswa kijinsia.
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukaza kwa kusema, furaha ya Kikristo inajikita katika uhalisia wa maisha ya watu; kwa kuitikia wito wa Mungu kama alivyofanya Mtakatifu Yosefu mtu wa haki kwa kuchukua na kuhifadhi zawadi ya unyofu na utakatifu wa maisha ya watoto wa nyakati hizi. Kipindi cha Noeli ni wakati wa kusimama kidete kulinda zawadi ya maisha, kwa kuipatia nafasi kuzaliwa, kukua na kuwapyaisha kama ilivyokuwa kwa wachungaji jasiri kule kondeni. Huu ni ujasiri unaowawezesha Maaskofu Katoliki kutambua hali halisi ya watoto katika ulimwengu mamboleo ili kujizatiti kwa kuwaundia mazingira bora yatakayolinda na kutetea utu na heshima yao kama watoto wa Mungu.
Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake kwa Maaskofu Katoliki duniani anasema, kamwe wasikubali watoto kupokwa furaha ya utoto wao! Hata wao wenyewe wasikubali kunyang’anywa furaha, bali wasimame kidete kuilinda na kuipatia nafasi ya kukua na kukomaa katika uaminifu mkubwa kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yosefu aliyeongozana na Bikira Maria, Mama mpole, ili kamwe wasiwe na mioyo migumu kama jiwe!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni