0
Askofu Titus Joseph Mdoe wa Jimbo Katoliki la Mtwara, amewahimiza Waamini wote Jimboni humo kushiriki kikamilifu katika mazoezi mbalimbali ya kiroho ikiwemo sala wakati Kanisa la Tanzania  linaadhimisha Jubilei ya miaka 100 (1917-2017) tangu  kupatikana kwa Mapadre wa kwanza Wazalendo! Wito huo aliutoa kwenye Ibada Misa takatifu kwa ajili ya kutoa Daraja ya Upadre kwa Mashemasi wawili; Damas Msisiri, OSB na Deusdedit Msao, OSB  wa Shirika la Mtakatifu Benedikto Nyumba ya Ndanda (Abasia/Abbey) Jimboni humo zilizofanyika mwishoni mwa mwaka 2016 katika Kanisa la Abasia hiyo.
Alisema, Maaskofu Katoliki nchini Tanzania watatoa mwongozo wa jinsi ya kuiadhimisha Jubilei hiyo ambayo itafikia kilele chake hapo mwaka 2017. “Nawaalikeni nyote tuingie katika maadhimisho hayo kwa sala tukimshukuru Mungu kwa miaka 100 ya hao mapadre wa kwanza sanjari na miaka 150 tangu Uinjilishaji wa Tanzania Bara uanze kule Bagamoyo.” Mapadre wa kwanza wazawa wa Tanzania wanaotimiza miaka 100 ni Padre Angelo Mwirabure wa Jimbo la Geita, Padre Oscar Kyakaraba wa Bukoba, Padre Celestine Kipanda wa Jimbo la Bunda pamoja na Padre Wilibard Mupapi wa Jimbo la Bukoba.
Akizungumzia kupatikana kwa mapadre hao wawili kwa mpigo Askofu Mdoe alisema, ni zawadi kutoka kwa Mungu kwa ajili ya Wanashirika hilo, lakini si kwa Shirika tu bali ni kwa Kanisa lote Jimboni, kwa kuwa hivi sasa wapo mapadre mbalimbali wa Shirika hilo la Mtakatifu Benedikto ambao wanahudumia Parokia za Jimbo  Katoliki la Mtwara. Alitumia fursa hiyo kuwahimiza mapadre hao kuwa na imani thabiti kwa Mungu, waondoe hofu na wakumbuke kuwa Taifa lote la Mungu lipo pamoja nao. “Muwe na imani katika Utume wenu na mtambue kuwa Taifa lote la Mungu  lipo pamoja nanyi, linawaombea ninyi na lipo tayari kuwasaidia kwa hali na mali,mnachodaiwa ni kutekeleza majukumu yenu ya Kipadre”, alisema Askofu Mdoe.
Naye Abate wa Nyumba ya Watawa wa Ndanda Padre Placido Mtunguja alianza kumshukuru Mungu kwa kuwajalia Mapadre pacha, huku akikumbuka pia kwamba mwezi Julai mwaka 2015 Mashemasi watatu kwa mpigo walipewa Daraja ya Upadre katika Kanisa hilo. Baada ya shukrani hizo aliendelea kulifungua furushi lake lililojaa shukrani kwa Maabate Wastaafu wa Ndanda, Abate wa Nyumba ya Peramiho, Watawa wote wa kike na wa kiume, umati wa Mapadre kutoka majimbo ya Lindi, Mbinga, Mtwara, Songea, Tunduru-Masasi pamoja na wageni mbalimbali wakiwemo Viongozi wa Serikali na vyama vya kisiasa.
Alimshukuru pia Askofu Mdoe kwa kukubali kuja kuwapadrisha Watawa hao.Aidha Abate Mtunguja alilazimika kuwashukuru wazazi wa vijana hao ambao waliwalea na kuwaruhusu wauitikie wito wao wa Utawa na hatmaye Upadre, sanjari na Walezi mbalimbali walioshiriki katika kuwalea hadi kufikia hatua ya kuwa mapadre. Kwa niaba ya wazazi wa mapadre hao wapya,Mwalimu mstaafu Joseph Masawe ambaye ni Baba mzazi wa Padre Deusdedit OSB aliwashukuru na kuwapongeza Viongozi wa Shirika la Kitawa, kwa jitihada zao katika kuendeleza malezi bora waliyoyaanza kwa vijana wao wakiwa huko nyumbani,na kuwataka wasirudi nyuma katika utume wao kusudi wapatikane Mapadre wengine.Khatimaye aliwausia mapadre hao kuzingatia malezi bora waliyoyapata ili wawe watumishi badala ya kupenda kutumikiwa.
Akiongea kwa niaba ya mwenzake, Padre Damian Msisiri OSB, alitoa shukrani kwa wote wakiwemo Askofu, Wakuu wa Shirika lake,Wanajumuiya yao, Walezi, Mapadre, Masista na wageni wote ambao walihudhuria tukio hilo la kihistoria katika maisha yao. Aliwahimiza kumshukuru Mungu kwa kila jambo, na kuongeza kuwa bila Mungu jitihada zetu mbalimbali zinazofanyika,na hata raslimali zenu tulizonazo hazitaleta tija bila baraka kutoka kwa Mungu. Akahitimisha kushukuru kwa zawadi mbalimbali walizopewa ambazo ni ukumbusho mkubwa kwa tukio hilo.
Kupatikana kwa Mapadre hao pacha kumeliongezea Shirika hilo idadi ya Mapadre wazalendo kutoka mapadre 15 mwaka 2015 hadi kufikia Mapadre 20 mwaka 2016. Akiongelea kuhusu ongezeko la Mapadre wazalendo kwenye Shirika la Watawa wa Mtakatifu Benedikto Ndanda, Mhasibu wa Halmashauri Walei Parokia ya Ndanda, Bi Cecilia Mmavele alitoa maoni kwa kueleza kuwa kadiri ya ongezeko hilo, baada ya muda mfupi, idadi ya mapadre kwenye majimbo ya Lindi, Mtwara na Tunduru-Masasi haitafua dafu kwa idadi ya mapadre itakayokuwepo katika Shirika hilo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka Shirika hilo, ongezeko la mapadre hao pacha kunalifanya Shirika hilo liwe na Mapadre 35, wakiwemo Wazalendo 20 na Wamisionari 15; huku kukiwa na waseminari watatu wanaosoma masomo ya Taalimungu kwenye Seminari kuu huko Morogoro,na wengine wawili wakihudhuria masomo ya Falsafa kwenye Seminari ya Spiritan iliyoko Jimbo kuu la Arusha
Na  Padre Anthony Chilumba.
Jimbo Katoliki Mtwara.

Chapisha Maoni

 
Top