Mama Kanisa tarehe 2 Februari 2017 anaadhimisha Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni, sanjari na Siku ya 21 ya Watawa Duniani iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II ili kuwaombea, kuwaenzi na kushikamana na watawa katika maisha na utume wao! Sr. Nicla Spezzati, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume anasema, watawa wote wameitwa kwa majina ili kumtumikia Mwenyezi Mungu na jirani zao.
Maadhimisho ya Siku ya Watawa Duniani kwa Mwaka 2017 bado yamefumbata kumbu kumbu hai ya maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ambapo waamini walikumbushwa kwa mara nyingine tena kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma! Katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, watawa kwa namna ya pekee kabisa, walikumbushwa kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa ya kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini!
Mwanga wa matukio yote haya anasema Sr. Nicla Spezzati unaendelea kuwasindikiza watawa katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa na kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaimarisha katika wito wao, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa waja wake. Matukio haya ni fursa makini ya kuendelea kutafakari, kufanya kumbu kumbu, kutubu na kuomwongokea Mungu pamoja na kujiwekea malengo ya kuwa watu wema na watakatifu zaidi, ili kuweza kuyachachua malimwengu kwa ushuhuda wenye mvuto na mashiko!
Katika maisha ya kitawa kuna matatizo na changamoto zake! Leo hii Mashirika mengi ya kitawa yana watawa wenye umri mkubwa na kwamba, idadi ya vijana wanaowania kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, inaendelea kupungua siku kwa siku hasa katika nchi za Ulaya na Amerika. Changamoto za utamadunisho na umwilisho wa karama za Mashirika bado ni pevu na kwamba, kuna madonda makubwa ya maisha ya kitawa na kazi za kitume yanayopaswa kugangwa na kuponywa kwa neema na baraka za Mungu, daima kwa watawa kuwa waaminifu kwa maisha, wito na karama zao, kwa kutambua kwamba, wameitwa kwa majina kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia ukuu wa Mungu kati ya watu wake.
Watawa waoneshe na kushuhudia ukarimu wa kimissionari, sadaka na majitoleo ya dhati kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa njia ya huduma makini katika elimu, afya, ustawi na maendeleo ya jamii. Wawe ni watu wa sala na tafakari ya kina, ili kuweza kujichotea nguvu katika maisha na utume wao kwa familia ya Mungu inayowazunguka. Wawe tayari kujisadaka hata kama itawabidi kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, yalisaidie Kanisa kung’ara kwa utakatifu wa maisha!
Sr. Nicla Spezzati anakaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko anawataka watawa kusoma alama za nyakati, tayari kutoka katika ubinafsi wao ili kuzingatia na kuambata mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa. Lengo ni kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Mwanga wa Injili ya Kristo duniani. Mang’umizi ya taalimungu ya Kanisa yasaidie kumwilisha mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa kwa kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi; katika huduma makini kwa maskini; kwa kukuza na kudumisha mahusiano ya kimissionari na kitume.
Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia una changamoto zake zinazojikita katika ubinafsi, kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema; lakini pia kuna mwamko wa watu kupenda mambo matakatifu na kwamba, Jumuiya ina kuwa ni mahali pa ushuhuda wa kinabii, umoja, upendo na udugu unaopata chimbuko lake katika Sakramenti za Kanisa. Kinzani na mipasuko ya maisha ya kijumuiya zisiwe ni kikwazo cha kusonga mbele, bali fursa ya kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya huduma, upendo na uaminifu. Watawa wawe ni mashuhuda wa huruma, upendo na matumaini ya watu wa Mungu; kwa kuwajibika barabara. Watambue kwamba, wao ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa wanaotumwa kutangaza furaha ya Injili!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni