0
Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujizatiti kikamilifu kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na amani duniani na kwamba, migogoro mbali mbali inapatiwa ufumbuzi wa amani, ili kujenga na kudumisha umoja, udugu na urafiki kati ya watu kwa kuzingatia kanuni maadili, ulinzi na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko aliomtumia Mama Elayne Whyte Gòmez, Rais wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa unaojadili kuhusu upigaji rufuku wa silaha za nyuklia.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu umesomwa kwa niaba yake na Monsinyo Antoine Camilleri, Katibu mkuu Msaidizi wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa
Kimataifa mjini Vatican katika mkutano ulioanza tarehe 27 Machi na unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 31 Machi 2017. Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, dunia inaondokana na hofu ya silaha za kinyuklia kwa kutekeleza mkataba wa kimataifa unaopiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha ya kinyuklia. Mkakati huu wa muda mrefu ni muhimu sana kutokana na hali tete na kinzani mbali mbali zinazojitokeza kwenye Jumuiya ya Kimataifa kiasi cha kutishia ulinzi, usalama na amani duniani.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika kipindi cha Karne ya 21 kumekuwepo na matukio yanayohatarisha ulinzi, usalama na amani duniani kutokana na vitendo vya kigaidi, vita, ukosefu wa usalama kwenye mitandao ya kijamii, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na umaskini; mambo ambayo yanapaswa kushughulikiwa kikamilifu sanjari na udhibiti wa utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha za kinyuklia kwani matokeo ya matumizi ya silaha hizi yanaweza kuwa ni makubwa sana, yakutisha na tena bila ubaguzi kwa maisha ya binadamu na mazingira katika ujumla wake.
Sumu za taka zinazozalishwa kwenye utengenezaji wa silaha za kijeshi zinatishia sana usalama wa maisha ya watu, rasilimali hii ingeweza kutumika kwa busara kusaidia kukuza amani na maendeleo endelevu ya binadamu sanjari na kupambana na baa la njaa, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuondokana na falsafa ya woga na kuanza kudumisha mchakato wa kuaminiana ili kuimarisha: ulinzi, usalama na amani duniani. Tabia ya mataifa makubwa kutaka kupimana nguvu inatishia amani na usalama duniani.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, amani inapaswa kujengwa kwenye haki, maendeleo endelevu ya binadamu; kwa kuheshimu na kuthamini haki msingi za binadamu; kwa kuunga mkono taasisi zinazoendeleza amani; kwa kuwekeza katika elimu na afya; kwa njia ya majadiliano na mshikamano. Kutokana na changamoto hizi kuna haja ya kuvuka na kwenda mbali zaidi na hofu ya mashambulizi ya silaha za kinyuklia, kwa kudumisha amani na utulivu na hivyo kuondokana na mtazamo finyu wa usalama wa kimataifa.
Upigaji rufuku wa silaha za kinyuklia ni changamoto ya kimaadili na dhamana ya kiutu kwa kukazia kanuni maadili zinazoendeleza amani duniani; ushirikiano katika ulinzi na usalama na kuondokana na falsafa ya woga usiokuwa na mvuto wala mashiko, hali inayopelekea baadhi ya mataifa kutengwa, jambo ambalo linashika kasi sana katika mijadala mingi ya kimataifa. Kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na dunia isiyokuwa na vitisho vya mashambulizi ya kinyuklia ikiwa kama binadamu ataheshimu ekolojia endelevu, kwani mustakabali wa binadamu anasema Baba Mtakatifu unaohitaji: majadiliano na ushirikiano ili kuweza kuwa na dunia isiyokuwa na vitisho vya nyuklia, kwa kujenga msingi wa kuaminiana.
Jambo hili linawezekana kwa njia ya majadiliano ya kweli yanayopania mafao ya wengi na wala si kwa ajili ya kulinda masilahi ya baadhi ya watu. Majadiliano haya hayana budi kuwahusisha wadau mbali mbali na kamwe kusiwepo na ubaguzi unaoweza kutumiwa na baadhi ya watu kuwa “kichaka cha kufichia masilahi yao”. Binadamu anao uwezo wa kushirikiana katika ujenzi wa nyumba ya wote kwa kutumia vyema: uhuru, akili na teknolojia pamoja na kuweka yote haya kwa ajili ya maendeleo endelevu ya binadamu na kijamii katika ujumla wake. Mkutano huu unaojikita hasa katika kanui na maadili ni safari inayoweza kuondoa hofu ya mashambulizi ya silaha za kinyuklia, mchakato huu ni mgumu, lakini unawezekana kabisa. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka wajumbe kudumisha kanuni maadili ya amani sanjari na  ushirikiano wa usalama kimataifa; mambo yanayohitajiwa na wengi kwa sasa!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top