0
Mama Kanisa katika kipindi cha Pasaka anaadhimisha, anatangaza na kushuhudia matumaini, furaha, upendo na mshikamano miongoni mwa wafuasi wa Kristo mambo msingi yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Hii ni changamoto kwa wafuasi wote wa Kristo kushikamana katika Uekumene wa huduma kwa ajili ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Lengo ni kuhakikisha kwamba,
furaha na matumaini ya Kristo Mfufuka katika kipindi hiki cha Pasaka yanawafikia na kuwaambata watu wengi zaidi
Hii ni sehemu ya ujumbe wa Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa la Kianglikani. Anakumbusha kwamba, mwaka 2017, Pasaka imeadhimishwa na Wakristo wote siku moja, yaani hapo tarehe 16 Aprili 2017. Tukio hili la kihistoria litajirudia tena kunako mwaka 2025. Kipindi cha Pasaka cha mwaka huu, iwe ni fursa makini ya kujikita katika uekumene wa sala na maisha ya kiroho; uekumene wa damu, lakini zaidi uekumene wa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali.
Wakristo kutoka katika mataifa, lugha, jamaa na tamaduni mbali mbali kwa pamoja, mwaka huu wamemwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwani Kristo Yesu amefufuka kweli kweli! Yesu alipokuwa hapa duniani aliwafundisha wanafunzi wake kumwomba Baba yake wa mbinguni, ili kweli Ufalme wake uje na kusimikwa duniani na kwamba, mapenzi yake yatimizwe duniani kama ilivyo mbinguni! Huu ni Ufalme wa haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati hasa miongoni mwa maskini.
Askofu mkuu Justin Welby anawaalika Wakristo kwa namna ya pekee, kuungana pamoja naye tangu baada ya Siku kuu ya Bwana kupaa mbinguni na kurejea kwa Baba yake wa mbingu hadi Pentekoste, kwa sala maalum; kwani kalenda ya maadhimisho yote haya inawaruhusu Wakristo kushikamana kwa dhati, na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Ni kipindi maalum kwa ajili ya kuwaombea walimwengu sanjari na kuendeleza mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Anakumbusha kwamba, Kanisa linaadhimisha Pasaka ya Bwana, mwanzo mpya wa kazi ya uumbaji na mwaliko wa maisha ya uzima wa milele kama anavyokaza kusema Mtakatifu Augustino, Askofu na mwalimu wa Kanisa. Jumapili, siku ambayo Kanisa linaadhimisha ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu, ni kielelezo makini cha ushindi wa Kristo dhidi ya dhambi na mauti, mwanzo wa mchakato mpya wa kuyaendea maisha ya uzima wa milele.
Askofu mkuu Justin Welby anasema, hata kama kalenda ya maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa inatofautiana kutoka Kanisa moja kwenda Kanisa jingine, lakini jambo la maana hapa ni kushikamana katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu miongoni mwa watu wa Mataifa. Kanisa linatangaza na kushuhudia kwamba, Kristo Yesu, aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kadiri ya Maandiko Matakatifu. Hii ni imani inayowaunganisha Wakristo wote, tayari kutoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu ni changamoto endelevu inayopaswa kuvaliwa njuga na Wakriosto wote si tu wakati wa kipindi cha Pasaka, bali kama sehemu ya vinasaba na utambulisho wao wa Kikristo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top