Mdo. 2:14, 22 – 28
Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu.
Yesu wa Nazareti, mtu aliyedhihirishwa kwenu na Mungu kwa miujiza na ajabu na ishara, ambazo Mungu alizifanya kwa mkono wake kati yenu, kama ninyi wenyewe mnavyojua; mtu huyu alipotolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa, na kwa kujua kwake tangu zamani, ninyi mkasulibisha kwa mikono ya watu wabaya, mkamwua; ambaye Mungu alimfufua, akaufungua uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana ashikwe nao. Maana Daudi ataja habari zake.
Nalimwona Bwana mbele yangu sikuzote, Kwa kuwa yuko upande wa mkono wangu wa kuume, nisitikisike.
Kwa hiyo moyo wangu ukapendezewa, ulimi wangu ukafurahi; Tena mwili wangu nao utakaa katika matumaini. Kwa maana hutaiacha roho yangu katika kuzimu; Wala hutamtoa Mtakatifu wako aone uharibifu. Umenijulisha njia za uzima; Utanijaza furaha kwa uso wako.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 16:1 – 2, 5, 7 – 11 (K) 11
(K) Utanijulisha njia ya uzima.
Mungu unihifadhi mimi,
Kwa maana nakukimbilia Wewe.
Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu;
Bwana ndiye fungu la posho langu, na la kikombe changu;
Wewe unaishika kura yangu. (K)
Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri,
Naam, mtima wangu umenifundisha usiku.
Nimemweka Bwana mbele yangu daima,
Kwa kuwa yako kuumeni kwangu, sitaondoshwa. (K)
Kwa hiyo moyo wangu unafurahi,
Nao utukufu wangu unashangilia,
Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini.
Maana hutaiachaia kuzimu nafsi yangu.
Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu. (K)
Utanijulisha njia ya uzima;
Mbele za uso wako ziko furaha tele;
Na katika mkono wako wa kuume mna mema ya milele. (K)
SOMO 2
1Pet. 1:17 – 21
Ikiwa mnamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni. Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwanakondoo asiye na ila, asiye na waa, ya Kristo. Naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa mwisho wa zamani kwa ajili yenu; ambao kwa yeye mmekuwa wenye kumwamini Mungu, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata Imani yenu na tumaini lenu liwe kwa Mungu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Lk. 24:32
Aleluya, aleluya,
Bwana Yesu, utufunulie maandiko; uwashe mioyo yetu unaposema nasi.
Aleluya.
INJILI
Lk. 24:13 – 35
Siku ile watu wawili miongoni mwa wafuasi wa Yesu walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili. nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia. Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao. Macho yao yakafumbwa wasimtambue. Akawaambia, Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso zao.
Akajibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia, Je! Wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi? Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote; tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha. Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu yalipotendeka mambo hayo; tena, wanawake kadha wa kadha wa kwetu walitushitusha, waliokwenda kaburini asubuhi na mapema, wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai. Na wengine waliokuwa pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale wanawake walivyosema, ila yeye hawakumwona.
Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii! Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake? Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe.
Wakakikaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, naye alifanya kama anataka kuendelea mbele. Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao. Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao. Wakaambiana, Je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia maandiko?
Wakaondoka saa ile ile, wakarejea Yerusalemu, wakawakuta wale kumi na mmoja wamekutanika, wao na wale waliokuwa pamoja nao, wakisema, Bwana amefufuka kweli kweli, naye amemtokea Simoni, nao waliwapa habari ya mambo yale ya njiani, na jinsi alivyotambulikana nao katika kuumega mkate.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
KUFAULU KATIKA JARIBIO LA IMANI!
“KUFUFUKA NA KRISTO”
Tafakari ya Pasaka
Ijumaa, Aprili 28, 2017,
Juma la 2 la Pasaka
Mdo 5:34-42
Zab 27: 1,4,13-14
Yn 6:1-15
KUFAULU KATIKA JARIBIO LA IMANI!
Mungu daima anatambua anachopenda kufanya. Daima yeye ana mpango mkamilifu wa maisha yetu. Leo katika Injili, Yesu anafanya muujiza wa kuwalisha watu kwa mkate na samaki. Yesu alitambua kwamba ataongeza mkate na samaki ili kuwalisha watu zaidi ya elfu tano. Lakini kabla ya kufanya hili, anamjaribu Philipo. Hivyo hivyo Yesu anatujaribu wakati mwingine. Je, hafanyi hivyo?
Majaribio haya sio kwamba Yesu anapenda kutuuliza tu au kufanya mchezo Fulani na sisi. Bali, anatupa nafasi ya kudhihirisha imani yetu kwake. Jaribio lililopo kwenye Injili lilikuwa ni kumfanya Philipo atumie Imani zaidi kuliko kufikiri kwa kawaida pekee. Philipo aliitwa ili kudhihirisha imani kwamba Mwana wa Mungu yupo pamoja nao pale. Lakini alishindwa jaribio. Alinyoosha mkono kwa ile hali ya kutokuwezekana. Lakini katika hali nyingine ni kama Andrea alikuja kuokoa. Anasema kuna kijana hapa ana mkate na visamaki vichache. Lakini yeye pia alikuwa na Imani kidogo, aliongeza kusema “lakini vya faa nini kwa umati huu mkubwa namna hii?”.
Chembe hii dogo ya imani ya Andrea, ilitosha kwa Yesu kuamuru watu waketi makundi makundi na hivyo kufanya ule muujiza. Inaonekana kwamba Andrea alikuwa na ufahamu kidogo kwamba ilikuwa muhimu kutaja visamaki hivi na mkate. Yesu anavichukua kutoka katika mikono ya Andrea na kuwajali watu.
Mara nyingi tunajikuta katika hali ngumu na hatujui tufanye nini. Tunapaswa kujitahidi kuwa na imani kidogo ili Yesu aweze kuwa na kitu cha kutenda katika maisha yetu. Tunaweza tusiwe na ufahamu wa nini anaenda kufanya, lakini ni lazima kuwa na ufahamu hata kidogo kwamba Mungu ndiye anaye tuongoza sisi. Kama tutaweza hata kukuza Imani hii kidogo sisi pia tutashinda majaribio.
Sala: Bwana, nisaidie niweze kuwa na Imani kamili ya mpango wako ambao unapenda kuufanya katika maisha yangu. Nisaidie niweze kufahamu kwamba wewe unaongoza na kuyalinda maisha yangu hata pale ninapo ona maisha yanayumba. Katika hali hizo, ninaomba Imani ninayo onesha iwe zawadi kwako ili uweze kuitumia kwa utukufu wako. Yesu, nakuamini wewe. Amina
MASOMO YA MISA, APRILI 28, 2017
MASOMO YA MISA, APRILI 28, 2017
IJUMAA, JUMA LA 2 LA PASAKA
SOMO 1
Mdo 5:34-42
Lakini mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamalieli, mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza, akaamuru mitume wawekwe nje kitambo kidogo, akawaambia, Enyi waume wa Israeli, jihadharini jinsi mtakavyowatenda watu hawa. Kwa sababu kabla ya siku hizi aliondoka Theuda, akijidai ya kuwa yeye ni mtu mkuu, watu wapata mia nne wakashikamana naye; naye aliuawa na wote waliomsadiki wakatawanyika wakawa si kitu. Baada ya mtu huyo aliondoka Yuda Mgalilaya, siku zile za kuandikiwa orodha, akawavuta watu kadha wa kadha nyuma yake, naye pia akapotea na wote waliomsadiki wakatawanyika. Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu, itavunjwa, lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu. Wakakubali maneno yake; nao walipowaita mitume, wakawapiga, wakawaamuru wasinene kwa jina lake Yesu; kisha wakawaacha waende zao. Nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo. Na kila siku, ndani ya hekalu na nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema za Yesu kwamba ni Kristo.
Neno la Bwana… Tumshukuru Bwana.
WIMBO WA KATIKATI
Zab 27:1, 4, 13-14
(K)Neno moja nimelitaka kwa Bwana, Nikae nyumbani mwa Bwana.
Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani? (K)
Neno Moja nimelitaka kwa Bwana,
Nalo ndilo nitakalolitafuta,
Nikae nyumbani mwa Bwana
Siku zote za maisha yangu,
Niutazame uzuri wa Bwana,
Na kutafakari hekaluni mwake. (K)
Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)
SHANGILIO
Kol. 3:1
Aleluya, aleluya.
Mkiwa mmefufuliwa na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.
Aleluya.
INJILI
Yn 6:1-15
Baada ya hayo Yesu alikwenda zake ng'ambo ya Bahari ya Galilaya, nayo ndiyo ya Tiberia. Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa. Naye Yesu akakwea mlimani, akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. Na Pasaka, sikukuu ya Wayahudi, ilikuwa karibu. Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake, alimwambia Filipo, Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula? Na hilo alilinena ili kumjaribu; kwa maana alijua mwenyewe atakalotenda. Filipo akamjibu, Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo tu. Wanafunzi wake mmojawapo, Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, Yupo hapa mtoto, yuna mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa? Yesu akasema, Waketisheni watu. Na mahali pale palikuwa na majani tele. Basi watu waume wakaketi, wapata elfu tano jumla yao. Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka. Nao waliposhiba, aliwaambia wanafunzi wake, Kusanyeni vipande vilivyobaki, kisipotee cho chote. Basi wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili, vipande vya mikate mitano ya shayiri vilivyowabakia wale waliokula. Basi watu wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni. Kisha Yesu, hali akitambua ya kuwa walitaka kuja kumshika ili wamfanye mfalme, akajitenga, akaenda tena mlimani yeye peke yake.
Neno la Bwana
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni