0
Baba Mtakatifu Francisko ameianza Siku yake ya Pili ya hija ya kitume nchini Misri, Jumamosi tarehe 29 Aprili 2017 kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Jeshi la Anga iliyohudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka Misri. Katika mahubiri yake, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Pasaka, Baba Mtakatifu amekazia mambo makuu matatu: Kifo, Ufufuko na Maisha; mambo ambayo wafuasi wa Emau walikuwa wakijadiliana njiani baada ya mateso na kifo cha Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu wao. Ni watu waliokuwa wamechanganyikiwa kutokana na Kashfa na upuuzi wa Msalaba, ulio
zika matumaini yao yote.
Wanafunzi hawa walijenga matumaini yao kwa Yesu ambaye amekufa na kushindwa vibaya, kiasi kwamba amezikwa pamoja na matumaini yao yote! Yesu, Mwalimu na Mkombozi aliyewafufua wafu na kuponya wagonjwa akashindwa kujiokoa mwenyewe hadi kuishia kwenye Kashfa ya Msalaba. Walishindwa kuamini ilikuaje Mwenyezi Mungu akashindwa kumwokoa Yesu kutoka kwenye ukatili mkubwa wa kifo. Msalaba wa Kristo ulikuwa ni Msalaba wa mawazo yao kuhusu Mungu; Kifo cha Kristo kilikuwa ni kifo cha yule waliyedhani pengine ni Mungu. Wanafunzi hawa ndio waliokufa na kuzikwa kaburini kutokana na kushindwa kwao kufahamu Fumbo la Msalaba.
Baba Mtakatifu anafafanua kwa kusema, hivi ndivyo inavyojitokeza kwa mwamini kujikuta hajitambui  kwa kushindwa kuvuka wazo lake kuhusu Mwenyezi Mungu, mungu ambaye ameumbwa kwa sura na mfano wa binadamu. Ni mara ngapi waamini wanakatishwa tamaa kwa kukataa kuamini kwamba, ukuu na nguvu ya Mungu havijioneshi kwa nguvu, vitisho na mamlaka, bali katika upendo, msamaha na maisha tele! Wanafunzi walimtambua Yesu kwa kuumega mkate, katika kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, changamoto na mwaliko wa kuvunjilia mbali mambo yote yanayofisha macho yao na hivyo kuufanya moyo wao kushindwa kuvunjilia mbali mawazo mgando na maamuzi mbele, kwa hakika watashindwa kuufahamu Uso wa Mungu!
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema kwamba,  katika usiku wa giza nene, hali ya kuchanganyikiwa na kukatisha tamaa, Yesu anajitokeza na kuanza kuandamana nao, ili waweze kumgundua kwamba yeye ni njia, ukweli na uzima, Yesu Mfufuka anatumia fursa hii kugeuza hali yao ya kukata tamaa kuwa ni chemchemi ya maisha na yale matumaini ya kibinadamu yanapotoweka kama ndoto ya mchana, matumaini ya Kimungu yanachukua nafasi ya kuanza kung’aa, kwani kile ambacho hakiwezekani kwa binadamu, kinawezekana mbele ya Mungu.
Pale mwanadamu anapogusa sakafu ya kushindwa na udhaifu wake ni pale anapoanza kuzama katika mawazo ya kufikiria na kudhani kwamba yeye ni bora kuliko wengine na anaweza kujitegemea na kujitosheleza mwenyewe; na kwamba, ni sehemu muhimu sana ya ulimwengu, hapo ndipo Mwenyezi Mungu anapomnyooshea mkono wake kiasi cha kugeuza usiku wa giza kuwa ni mapambazuko angavu na cheche za furaha zinaanza kuchanua, kifo chake kinageuka kuwa ni ufufuko na kuanza kuchapa miguu tena kurejea Yerusalemu, yaani kurejea tena katika chemchemi ya maisha na kutambua ushindi wa Msalaba.
Wafuasi wa Emau baada ya kukutana, kuzungumza na kutembea na Yesu Kristo Mfufuka, wanarejea wakiwa wamesheheni furaha, imani na matumaini kedekede, tayari kushuhudia imani yao kwa Kristo Mfufuka aliyewafufua kutoka katika makaburi yao ya kutoamini na kujikatia tamaa. Kwa kukutana na Kristo Mfufuka wakapata nafasi ya kufafanuliwa utimilifu wa Maandiko Matakatifu, Sheria na Unabii na hatimaye, kufahamu kwa kina maana ya Kashfa ya Msalaba. Kwa mang’amuzi ya Fumbo la Msalaba wakaweza kufikia ukweli wa Ufufuko kiini cha matumaini mapya. Ili kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu kuna haja kwa waamini kusubilisha mawazo yao yanayomwonesha mungu kuwa ni muweza wa yote na mwenye nguvu!
Wafuasi wa Emau kwa kukutana na Kristo Mfufuka wanapata mabadiliko makubwa katika maisha. Lakini ikumbukwe kwamba ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu si imani iliyozaliwa ndani ya Kanisa, lakini Kanisa limezaliwa katika imani kwa Kristo Mfufuka anayeendelea kuwafunda wafuasi wake kumwamini hata kama bado hawajamwona. Kanisa halina budi kuendelea kutambua, kuamini na kumsadiki Kristo Mfufuka anayeliuhisha Kanisa kwa njia ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa, tayari kumtangaza na kumshuhidia Kristo Mfufuka kama walivyofanya wanafunzi wa Emau, kwa kujikita katika Ibada na uchaji kwa Mungu, upendo na mshikamano kwa jirani; imani inayomwilishwa katika matendo kwani Mwenyezi Mungu anaangalia moyo wa mtu na kukataa unafiki!
Baba Mtakatifu anakaza kusema, imani ya kweli ni ile inayomwilishwa katika matendo ya huruma na upendo kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya wengine bila ubaguzi. Imani ya kweli inawasaidia waamini kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu na wala si kama adui wa kufutiliwa mbali kutoka katika uso wa dunia. Kwa hakika, imani ya kweli inamwilisha katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu na kwamba, imani inakua na kuchanua katika unyenyekevu. Imani inapaswa kumwilishwa katika matendo, tayari kurejea tena katika maisha kwa furaha, ujasiri na imani thabiti, bila kusita kumfungulia Kristo malango ya maisha yao ili aweze kuwakirimia mwelekeo mpya wa maisha. Upendo unaomwilishwa katika maisha ni amana ya mwamini!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top