Wapendwa Mahujaji, tumejumuika leo kuadhimisha siku maalum ya kwenda faraghani na kujitenga na pilika pilika za tume zetu za kila siku na masumbuko ya maisha yetu. Napenda kuwashukuruni kwa kutenga muda wenu wa kutosha kwa ajili ya zoezi hili muhimu la kiroho. Nawapongeza kwa uamuzi huu wa busara wa kukubali kuchukuliwa na Roho wa Bwana na kwa nguvu zake kupelekwa katika
jangwa la kiroho ili Roho azungumze na mioyo yetu na akili zetu katika Kituo hiki cha hija wakati wa Adhimisho la Sherehe ya Huruma ya Mungu tarehe 23 Aprili 2017.
Tunaanza kuzungumza kwa pamoja na Roho Mtakatifu kwa njia ya Misa hii Takatifu kwa heshima ya Mama Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Tunaiadhimisha kwa kusudi maalum kabisa - maana mwaka huu wa Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria watokee watoto wa Fatima ambao ni Yasinta Marto na Francis - watatangazwa watakatifu tarehe 13 Mei mwaka huu kule Fatima nchini Ureno na Baba Mtakatifu Francisko, wakati mchakato wa kumtangaza Sr. Lucia dos Santos (binamu wa Yasinta na Francis na mkubwa kati ya hao watatu, aliyeishi muda mrefu na kufariki dunia tarehe 13/2/2005) kuwa mwenye heri na hatimaye mtakatifu - umeanza hivi karibuni. Naamini kwa dhati kuwa safari ya haraka ya kufika mbinguni na kwa uhakika wa mia kwa mia ni safari ya kuvaa viatu viwili vya uhakika vitakavyotufikisha bila wasiwasi nyumbani kwa Baba wa Huruma. Viatu hivi ni - Ibada kwa Bikira Maria wa Fatima na Ibada ya Huruma ya Mungu. Ukivaa viatu hivi viwili, mwenzangu, utasafiri salama na haraka katika safari ya utakatifu na ufuasi wa Bwana na kuwa Mtume wa Huruma yake chini ya uongozi wa Mama Maria, Kiongozi amini wa kwenda mbinguni.
Tunapokuwa basi katika Adhimisho la Sherehe ya Huruma ya Mungu, tumwombe Mungu Roho Mtakatifu apende kutuonyesha nafsi ya Mama Bikira Maria, Kiumbe bora kabisa cha Mwenyezi Mungu, mtumishi bora wa Bwana, Mwalimu Mkuu katika shule ya Upendo wa Kristo, Mama yetu na Mwombezi wetu na Kiongozi amini wa kwenda mbinguni. Kwanza, tuone nafasi ya pekee ya Mama Bikira Maria katika safari yetu ya wokovu na katika vita vyetu vya kiroho hapa duniani.
I - Nafasi ya Bikira Maria katika mapambano ya maisha ya kiroho!
Bikira Maria ana nafasi ya pekee katika vita vya kiroho vinavyoendelea katika historia ya wokovu. Tena anayo nafasi hiyo tangu wakati ule wa anguko la Shetani. Mungu alipomuumba Lusiferi (Lusiferi – maana yake pambazuko au abebaye mwanga, nuru), alimshirikisha nguvu zake na uhuru wake. Lusiferi alikuwa miongoni mwa viumbe bora vya Mungu Muumba. Mungu alimjaza Lusiferi neema na baraka nyingi sana. Wakati Lusiferi na Malaika wengine wenzake walipokataa kumtii na kumtumikia Mungu wakisema ‘Non serviam!’ yaani ‘Sitatumikia!’, basi, Mungu alijibu uasi huo kwa Umwilisho wa Bwana wetu Yesu Kristo aliyezaliwa na Mwanamke kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Mungu alitufunulia kuwa anataka kutukomboa katika dhambi kwa njia ya kujinyenyenyekeza Yeye mwenyewe na kwa kutwaa hali iliyo duni kuliko ile ya Malaika – yaani kuwa mwanadamu.
Hivyo, kwa njia hiyo Lusiferi na pepo wabaya wenzake wakiwa viumbe tu vya Mungu nao wangepewa hali duni zaidi – kuwa chini ya Mwanamke na uzao wake. Jambo hili Lusiferi na wenzake hawakuweza kukubali na kuvumilia, hivyo wakaanza vita vikali sana dhidi ya Bikira Maria. Nabii Isaya anaeleza vizuri sana hali hii ya upinzani wa Lusiferi: “Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, ewe uliyewaangusha mataifa! Nawe ulisema moyoni mwako, ‘Nitapanda mpaka mbinguni, nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, nitafanana na Yeye Aliye juu’. Lakini utashushwa mpaka kuzimu, mpaka pande za mwisho za shimo” (Isa 14:12-15). Kiumbe wa Mungu mwenye fahari ya ajabu alitenda dhambi katika majivuno yake na kiburi!
Kitabu cha Ufunuo wa Yohane kinasimulia mapambano ambayo yalimwangusha Lusiferi (sasa akiitwa Shetani) na wenzake kutoka mbinguni hadi kuzimuni: “Kulikuwa na vita mbinguni: Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye” (Ufu 12:7-9). Sababu ya hasira ya Shetani ni Mwanamke aliyemzaa Mkombozi pamoja na vyungo vyote vya Mwili wa Kristo – yaani Kanisa Takatifu, ambalo pia ni uzao wa Mama Maria. “Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu” (Ufu 12:17).
Jibu la Mungu kwa kiburi ya Shetani ni nafsi ya Bikira Maria. Yeye ni kiumbe bora cha Mungu kilichotoka mikononi mwake. Maria ni nyota mpya ya asubuhi – si Lusiferi tena! Yeye ni “Sanduku la Agano” (taz. Ufu 11;19) linalombeba Bwana wa Agano Jipya ndani yake. Yeye ni ishara kubwa inayoonekana mbinguni: “Mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili” (Ap 12:1). Maria ni kiumbe bora, aliyekingiwa na dhambi ya asili, hivyo hakuwa kamwe chini ya utawala wa shetani na dhambi.
Jibu la Bikira Maria kwa Malaika Gabrieli lilikuwa ndilo hili: “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivosema” (Lk. 1:38). Maneno ya Bikira Maria yanapinga moja kwa moja msimamo wa Shetani aliyesema ‘sitatumikia!’ Na Wimbo wa Bikira Maria tunaosali kila siku kwenye Masifu ya Jioni unaeleza msimamo wa Bikira Maria ambao ni kinyume kabisa cha kiburi na majivuno ya Lusiferi. Maria anamsifu na kumuabudu Mungu. Unyenyekevu wake na hamu ya kumtumikia Mungu vinaonekana wazi. Maria, mjakazi wa Bwana, anampa uhai Mwana wa Adamu, Yesu Mteswa, ambaye kwa maisha yake nyenyekevu ya upendo na utii alimshinda Shetani kwenye mti wa Msalaba. Maria alishirikiana na Yesu katika kazi ya Ukombozi. Alisimama pale Msalabani, moyo wake ukiwa umechomwa upanga wa mateso (taz. Lk 2:35). Kila siku Maria alikuwa anarudia ahadi yake ya awali ya kumwambia Mungu ‘ndiyo!’ na hivyo alifaulu kabisa kuponda kichwa cha Shetani.
Mwana wa Bikira Maria na Mwili wake wa kifumbo, ambao ndio Kanisa Takatifu, wanaendelea na vita dhidi ya Shetani itakayokwisha kwa ushindi mkubwa wa Mungu siku ya mwisho. Hati za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano zinaeleza nafasi ya pekee ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya asili katika mapambano hayo kama ifuatavyo:
“Hatuwezi kushangaa ikiwa Mababa Watakatifu waliozoea kumwita Mama wa Mungu kuwa “Mtakatifu kabisa”, bila doa lolote la dhambi, kama aliyetengenezewa na Roho Mtakatifu na kufanywa kuwa kiumbe kipya. Hali amepambwa tangu nukta ya kwanza ya kutungwa kwake mamba kwa mng’aro wa utakatifu wa pekee kabisa, Bikira huyo wa Nazareti aliamkiwa na Malaika mhubiri, kwa amri ya Mungu, kuwa “amejaa neema”, naye akamjibu mjumbe wa mbinguni: ‘Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana, na iwe kwangu kama ulivyosema’” (Lk. 1:38)” (Mwanga wa Mataifa, 56).
“Mwishowe, Bikira asiye na doa, aliyekingiwa na kila doa la dhambi ya asili, akishamaliza mwendowa maisha yake duniani, aliinuliwa katika utukufu wa mbinguni pamoja na mwili wake na pamoja na roho yake; akatukuzwa na Bwana kama Malkia wa ulimwengu, ili afananishwe kikamilifu zaidi na Mwanawe aliye Bwana wa mabwana (taz. Ufu 19:16), na mshindi wa dhambi na mauti” (Mwanga wa Mataifa, 59). Kwa sababu Bikira Maria alikingiwa dhambi ya asili, basi, Shetani anashindwa mbele yake. Neema ya Mungu inamtawala kabisa Maria. Kwa sababu hiyo pia Mungu alimteua Maria kuwa silaha itakayomshinda kabisa Shetani na kutusaidia sisi pia katika mapambano dhidi ya Yule Mwovu.
Mungu anataka Kanisa la Mwanaye lifanane na Bikira Maria – tuwe bila dhambi na doa (taz. Waef 5:27). Mungu anataka kulivisha Kanisa lake vazi la utakatifu wa Maria. Yesu mwenyewe Msalabani alitueleza mpango huu wa Mungu alipotukabidhi Mama yake kuwa Mama yetu na alimkabidhi Mama sisi sote kama watoto wake. Tumpokee basi, Mama Bikira Maria na tuige mfano wa maisha yake tukiwa na ibada hai kwake na kujifunza fadhila zake. Hivyo tutahakikisha kuwa Mama Maria atakuwa nasi daima, nasi tutaweza kupokea msaada wake na kuutumia vema..
II - Kumfuasa Mama Bikira Maria katika maisha yetu ya ufuasi wa Bwana wetu Yesu Kristo: Ndugu zangu, ili Yesu aweze na apende kutupeleka mbinguni, hatuna budi kufuata mfano wa Mama Maria katika maisha yetu. Ningependa nifafanue maana ya kuwa mfuasi wa Bikira Maria au maana ya usemi wa „kuingia katika shule ya upendo wa Kristo ambapo Mwalimu wake Mkuu ni Mama Bikira Maria”. Kuna upande wa toba na malipizi, na kuna upande wa pili wa kuvaa vazi la Bikira Maria la ufanano naye.
Nianze kwa kueleza njia za kupoza Mateso ya Moyo Safi wa Maria uliozingirwa na miiba ya dhambi zetu na dharau za ulimwengu. Kisha, nitaeleza sifa za Mtoto mpendwa wa Maria. Kusudi, kila mmoja wetu akielewa hayo, aweze kumpendeza Mama Maria na kuiga mfano wa maisha yake na kuijenga Moyo wake Safi katika hisia za furaha. Kwanza, nieleze Mateso Saba ya Moyo Safi wa Maria. Mara nyingi tunaona picha au sanamu za Moyo Safi wa Maria ambazo zinaonyesha Moyo huo ukizungushiwa miiba au uliochomwa mapanga. Mababu wa Kanisa walieleza Mateso haya Makuu ya Moyo Safi wa Mama Maria kama ifuatavyo: Mateso saba ya Bikira Maria (panga saba za Mateso zilizopenya Moyo Safi wa Maria):
- Utabiri wa Nabii Simeoni
- Kukimbia Misri
- Kumtafuta Yesu siku tatu Yerusalemu
- Kukutana na Yesu wakati wa Njia yake ya Msalaba
- Kusimama na kudumu Kalvario pale Msalabani
- Kupokea Mwili wa Yesu ulioshushwa Msalabani
- Maziko ya Yesu.
Sote tutakubali kwamba Mateso hayo kweli yalikuwa ni makuu katika maisha ya Mama Maria. Sasa tufanyeje ili tuweze kupoza mateso hayo ya Mama na kumletea furaha ya kweli. Nadhani njia bora au ibada bora tulizo nazo katika Kanisa la Mwanaye zitakazokuwa kielelezo cha utayari wetu wa kumchukua Mama Maria nyumbani na kumpokea katika maisha yetu, kumuenzi na kumheshimu na kumpenda kwa moyo wa dhati na kwa njia hiyo kufanya malipizi ya mateso hayo ni hizi zifuatazo: ALAMA ZA KUMCHUKUA MAMA MARIA NYUMBANI (katika maisha yetu ya kiroho) – njia bora za kupoza Mateso ya Moyo Safi wa Maria (njia bora za kufanya malipizi):
- Ibada ya kujiweka wakfu kwa Mama Maria (ibada ya majitoleo kamili kwa utumwa wa kimapendo wa Mama Maria – Mt. Louis Maria Grignon de Montfort)
- Rozari Takatifu
- Medali ya kimuujiza
- Skapulari ya Bikira Maria wa Mlima wa Karmeli na masharti yake
- Novena ya Bikira Maria, Mama wa Msaada wa Daima
- Litania ya Bikira Maria
- Ibada ya Moyo Safi wa Maria (Jumamosi ya kwanza ya mwezi)
Katika njia hizi saba za kupoza Mateso ya Mama, ni zipi unazotumia, ni zipi zimeingia damuni mwako na rohoni mwako??? Wapendwa, Licha ya mateso hayo, Mama Maria mwenyewe alieleza kufuru zinazofanywa dhidi ya Moyo wake Safi katika ulimwengu huu, alipomtokea sista Lusia mnamo mwaka wa 1930. Sista Lusia alisema kwamba: „Nilipokuwa kanisani pamoja na Bwana wetu usiku wa 29-30 Mei 1930, na nilipoongea na Bwana wetu, kwa ghafla nilijihisi mimi mwenyewe kujawa na utakatifu uliokuwepo na, kama sikosei, haya ndiyo yaliyofunuliwa kwangu:
Binti yangu, kuna aina tano za makosa na kufuru yanayofanywa dhidi ya Moyo Safi wa Maria:
1) Kufuru dhidi ya imani kuwa Bikira Maria alitungwa mimba pasipo dhambi ya asili.
2) Kufuru dhidi ya Ubikira wake wa Daima.
3) Kufuru dhidi ya Umama wake wa Mungu, na kukataa wakati huo huo kumtambua kama Mama wa watu.
4) Kufuru za watu ambao hadharani wanapanda katika mioyo ya watoto kutojali, dharau, au hata chuki kwa Mama huyu Safi.
5) Makosa ya wale ambao wanaomdhihaki moja kwa moja katika sanamu zake takatifu.
"Hii, Binti yangu, ndiyo sababu kwa nini Moyo Safi wa Maria ulinisukuma Mimi kuomba ibada hii ndogo ya Malipizi ya dhambi..."
"Hii, Binti yangu, ndiyo sababu kwa nini Moyo Safi wa Maria ulinisukuma Mimi kuomba ibada hii ndogo ya Malipizi ya dhambi..."
Wapendwa, Kama ndivyo ilivyo, na kama ndivyo Mama anavyosikitika na kulalamika kwamba sisi tunamtendea hivyo, basi Ibada ya Moyo Safi wa Maria tunayoifanya kwa agizo lake – kila Jumamosi ya Kwanza ya Mwezi ni jambo la kimsingi katika maisha ya kila mmoja wetu. Masharti yake, mnavyofahamu, ni mepesi na kwa kweli, ibada ya Moyo Safi wa Maria ni njia ya mkato ya kwenda mbinguni. Masharti yenyewe ni kama ifuatavyo:
- Jumamosi ya Kwanza ya miezi mitano mfululizo
- Maungamo na Komunio ya Malipizi ya Jumamosi za Kwanza
- Kusali Rozari (matendo matano angalau)
- Tafakari ya dakika kumi na tano ya Mafumbo yote ya Rozari
- Nia ya sala ni kufanya malipizi
Ninaamini kuwa ibada hii aliyoiagiza Mama Maria mwenyewe itaota mizizi imara katika maisha yetu na kuzaa matunda ya kudumu.
III – Sifa za Mtoto halisi wa Bikira Maria
Wapendwa Mahujaji, Sasa nitaeleza Sifa za msingi za Mtoto Mpendwa wa Bikira Maria. Sifa hizo ni za Mama Bikira mwenyewe, hivyo yeyote anayetaka kuwa mfuasi mwaminifu wa Bwana wetu Yesu Kristo katika maisha yake, hana budi kuelewa kwamba Yesu alichukua tabia yake yote kwa Mama yake – maana Mt. Yosefu ni baba yake mlishi tu, na si wa kumzaa, hivyo Yesu tabia yake aliichukua kwa Mama yake Mzazi tu, Bikira Maria. Hivyo tukitaka kumfuata Yesu kikamilifu, hatuna budi kumtazama Mama yake na kuzifahamu, kuzielewa na kuziishi sifa zake alizozionyesha kwa namna ya pekee katika maisha yake mwenyewe. Sifa hizo kuu za Mama Bikira Maria na hasa za Moyo wake Safi ni hizi zifuatazo:
- Utii – Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe ulivyonena”
- Imani – „Heri yule aliyesadiki kwamba yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana” (hata pale msalabani)
- Unyenyekevu – „Baba yako na mimi” (anajiweka nyuma ya Mt. Yosefu)
- Umakini katika kutambua shida za wengine – „Hawana divai”
- Kujiaminisha kabisa katika Mapenzi ya Mungu – „Fanyeni lolote atakalowaambia Yesu”
Basi, tuweke mioyoni mwetu mafundisho haya, tuyatafakari kwa kina na kupitia kwa Moyo Safi wa Mama Maria, tumwombe Mungu Roho Mtakatifu ujasiri wa kuyaishi siku kwa siku katika maisha yetu kusudi Moyo Safi wa Maria ufarijike na ujengwe katika furaha ya kudumu, nasi tufike salama mbinguni tukifuata nyayo za Bwana katika shule ya upendo wake ambapo Mwalimu wake Mkuu ni Mama Bikira Maria mwenyewe.
Na Padre Wojciech Adam Koscielniak.
Kituo cha Hija Kiabakari, Jimbo Katoliki Musoma.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni