0
Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa washiriki wa mkutano wa majadiliano ya kidini kimataifa mintarafu amani ulioandaliwa na Chuo kikuu cha Al-Azhar cha Cairo nchini Misri, Ijumaa, tarehe 28 Aprili 2018 ameipongeza kwa namna ya pekee, Misri kuwa ni nchi ambayo ina tamaduni na hekima za kale pamoja na maagano! Ni nchi ambayo imezalisha wasomi wengi duniani na hapa ndipo panapopaswa kuwa ni chimbuko la amani, inayojikita katika majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya, mintarafu asili ya binadamu, wazi na inayojenga na kudumisha mafungamano ya kijamii
Elimu inapaswa kuwa ni hekima ya maisha inayomwez
esha mtu kujiondoa katika ubinafsi wake katika hali ya unyenyekevu ili kujikita katika majadiliano ya kina na endelevu. Ni ekima inayomwezesha mtu kukutana na kushirikiana na wengine katika hija ya maisha kwa kutambua kwamba, ubaya huzaa ubaya na vita huzaa maafa na majanga kwa binadamu. Elimu inapaswa kutoa kipambele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu sanjari na kujikita katika maadili yanayoondoa hofu na wasi wasi isiyokuwa na mashiko kwa kutumia njia ambazo zimewekwa na Mwenyezi Mungu.
Baba Mtakatifu anasema, majadiliano ya kidini yanawawezesha waamini kutembea kwa pamoja ili kukutana na tamaduni mbali mbali zinazosaidia pia kusukuma mbele mchakato wa maendeleo. Huu ndio mfano hai unaotolewa na Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini kwa kushirikiana na Kamati ya Msikiti wa Al Azhar ili kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini yanayofumbatwa katika: utambulisho, ujasiri wa kuheshimiana na kuthaminiana, daima kukiwa na nia njema kama kielelezo cha utu wema, ukweli, ili kujenga ushirikiano na wala si ushindani! Elimu inapaswa kuwa wazi, inayojikita katika heshima; majadiliano ya kweli yanatambua haki msingi na uhuru wa kuabudu, ili kuweza kuwa ni vyombo na wajenzi wa tamaduni za watu kukutana na wala si kupigana.
Vijana wanapaswa kufundwa kuhusu umuhimu wa kuondokana na ubaya kwa kujikita katika wema; vijana watambue historia yao, ili kushirikiana na wengine ili kuondoa hewa chafu ya kinzani ni mipasuko ya kijamii na badala yake kujenga udugu. Hii ni changamoto ambayo waamini wa dini mbali mbali wanahamasishwa kushiriki kuchangia kwa kutambua kwamba, wote wanaishi chini ya jua la huruma ya Mungu, mweza wa yote, anayewapatia jeuri ya kuitana ndugu. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kwa ajili ya kuombea kuchipuka kwa utamaduni wa amani na watu kukutana nchini Misri, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Francisko alipokutana na Sultani Malik al Kamil.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, Misri ni nchi ambayo imebahatika kuwa na maagano ya watu kutoka katika dini mbali mbali wanaotegemeana na kutajirishana katika huduma kwa Jumuiya ya Kimataifa, kwa ajili ya mafao ya wengi. Mlima Sinai unawakumbusha waamini Agano ambalo Mwenyezi Mungu alifanya na watu wake, kumbe dini si jambo la binafsi ni sehemu muhimu sana ya binadamu na jamii katika ujumla wake, changamoto hapa ni kutofautisha kati ya dini na siasa ambayo wakati mwingine inataka kumeza mambo ya kidini kwa ajili ya mafao yake binafsi. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yawasaidie watu kutambua wito wao kama binadamu na uwepo wa Mungu katika maisha yao na kwamba, dini si tatizo bali ni sehemu ya suluhu ya matatizo yanayomwandama mwanadamu, kwa kuthamini uwepo wa Mungu ili kujenga mji wa binadamu.
Amri kumi za Mungu zilizotolewa pale Mlimani Sinai zinakataza kutoa uhai wa binadamu, kwani maisha ni matakatifu na kwamba, utu na heshima ya binadamu pamoja na haki zake msingi, vinapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote kwa sababu Mwenyezi Mungu ni Mtakatifu na Jina lake ni takatifu na ni Mungu wa amani na amani ni takatifu na wala hakuna vita vitakatifu na kwamba, kutumia jina la Mungu kufanya mauaji ni kumkufuru Mungu na jina lake takatifu. 
Misri ambayo ni nchi ya maagano, waamini wote kwa mara nyingine tena wasimame kidete na  kukataa katu katu vita, tabia ya kulipiza kisasi kwa kisingizio cha dini au kwa jina la Mwenyezi Mungu na kwamba, hakuna uhusiano wowote kati ya: vita na imani; kati ya kuamini na kuwachukia wengine. Kwa pamoja wasimame imata kukuza na kudumisha utu, heshima na utakatifu wa maisha ya binadamu dhidi dhuluma: kimwili, kijamii, kielimu au kisaikolojia, Imani ya kweli inabubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, imani inaweza kukua na kukomaa kwa njia ya upendo kwa Mungu na jirani.
Dini inapaswa kukuza na kudumisha amani duniani, kwa kusali na kuombeana; kwa kukutana na kujadiliana; katika hali ya utulivu, ushirikiano na urafiki, kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ambaye kimsingi ni upendo. Dunia inawahitaji wajenzi wa amani na wala si wachochezi wa vita na mafarakano; wazima moto wa vita na wala si wachochezi wanaotaka kuona dunia ikiwaka moto!; dunia inawahitaji watangazaji wa upatanisho na wala si waharibifu. Jamii inapaswa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa amani duniani katika ukweli na uwazi na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake ili kutambua sababu zinazopelekea kusua sua kwa amani ili hatimaye, kuzitafutia suluhu ya kudumu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Misri kwa msaada wa Mwenyezi Mungu itaweza kutekeleza tena dhamana yake ya utamaduni na maagano, ili kukuza na kudumisha mchakato wa amani ndani na nje ya Misri!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top