Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani imekuwa ni fursa ya kujenga na kuimarisha Uekumene wa damu na huduma; maisha ya kiroho na sala kwa kuvuka kinzani na misigano ya kihistoria tayari kujikita katika safari ya ujenzi wa umoja unaosimikwa katika matumaini. Ni muda wa kumshukuru Mungu kwa wema na ukarimu wake kwani kwa miaka kadhaa iliyopita dhana ya kuweza kuwaunganisha: Wakatoliki, Waluteri
na Wapentekosti katika sala ya pamoja lilikuwa ni jambo lisiloweza kufikirika.
na Wapentekosti katika sala ya pamoja lilikuwa ni jambo lisiloweza kufikirika.
Lakini mwaka 2016 limewezekana kabisa, matunda na kazi ya Roho Mtakatifu anayewawezesha waamini kuvuka kinzani na vizingiti na kugeuza mafarakano kuwa ni fursa ya kujenga na kudumisha umoja. Hati ijulikanayo kama “Kutoka katika kinzani kuelekea katika umoja” ilikuwa ni sehemu ya uzinduzi wa maandalizi ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani. Hizi ni shukrani zilizotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 31 machi 2017 alipokutana na kuzungumza na washiriki wa kongamano la majadiliano ya kiekumene lililokuwa linaongozwa na kauli mbiu “Luther Miaka 500 baadaye”. Kongamano hili limeandaliwa na Tume ya Kipapa ya Sayansi ya Historia.
Baba Mtakatifu anawapongeza wadau wote walioshiriki katika mchakato wa mwendelezo wa maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani, fursa makini ya kuweza kuangalia kwa pamoja matukio haya muhimu sana katika historia, maisha na utume wa Kanisa. Imekuwa ni nafasi ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu mchango wa Luther, upinzaji wake kuhusu Kanisa na mchango wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika ujenzi wa imani kati ya waamini wa Makanisa haya, ikikumbatwa kwamba, kwa miaka mingi Wakatoliki na Waluteri walikuwa wanaangaliana kwa “jino pembe”.
Upembuzi yakinifu na sadifu usiogubikwa na maamuzi mbele na kinzani za kisiasa, leo hii yanaliwezesha Kanisa kujadiliana, kung’amua na kuchukuliana yale mambo mzuri na muhimu yaliyojitokeza kwenye Mageuzi ya Kiluteri Duniani. Ni wakati muafaka wa kuachana na makosa, ukuzaji wa mambo, mapungufu ya kibinadamu kwa kutambua dhambi iliyopelekea kumeguka kwa Kanisa la Kristo! Baba Mtakatifu Francisko anakiri kabisa kwamba, si rahisi kuweza kurejea tena katika historia iliyopita, lakini miaka 50 ya majadiliano ya Kiekumene kati ya Wakatoliki na Waluteri inaonesha kwamba, kuna uwezekano wa kutakasa kumbu kumbu na kufanya marekebisho ya dhati, ili kuweza kuandika tena historia ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani, bila kurejea kwenye madonda yaliyopita wakati wa mageuzi kwani yanawafanya waamini kuwa taswira mbaya kati yao. Baba Mtakatifu anasema, Wakristo wote wanahamasishwa kuondokana na maamuzi mbele dhidi ya imani ya wengine wanaokiri na kuabudu kwa mtindo na lugha tofauti; tayari kusamehe makossa yaliyotendwa na wazee waliotangulia ili hatimaye, kumwomba Mwenyezi Mungu zawadi ya upatanisho na umoja.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni