Mama Kanisa kuanzia tarehe 21 hadi 26 Agosti 2018 ataadhimisha Siku ya IX ya Familia Duniani, Jimbo kuu la Dublin nchini Ireland, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Injili ya familia, furaha ya ulimwengu”. Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua uzito wa tukio hili amemwandikia ujumbe Kardinali Kevin Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha akikumbusha juu ya maadhimisho ya Siku ya VIII ya Familia Duniani iliyoadhimishwa Jimbo kuu la Philadelphia, nchini Marekani na kwamba, maadhimisho haya kwa Mwaka 2018 yatafanyika Jimbo kuu la Dublin
Baba Mtakatifu anasema anapenda kutoa mwongozo makini ambao unapaswa kufuatwa kama sehemu ya tafakari ya Wosia wa Kitume, "Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Swali la msingi hapa ni kujiuliza ikiwa kama Injili inaendelea kuwa ni sababu ya furaha kwa ulimwengu? Je, Familia bado inaendelea kuwa ni Habari Njema kwa ulimwengu mamboleo? Baba Mtakatifu anakiri kwa kusema kwamba, ni kweli familia inaendelea kuwa ni sababu ya furaha na Habari Njema kwa walimwengu, kwani uhakika huu unafumbatwa katika mpango wa Mungu kwa mwanadamu; upendo ambao unapaswa kupewa jibu la “Ndiyo” na viumbe vyote kwani hiki ni kiini cha moyo wa binadamu.
Hii ni “Ndiyo” inayowaunganisha bwana na bibi tayari kushiriki katika mchakato wa kuhudumia uhai katika hatua zake zote! Hii ni “Ndiyo” ya Mungu inayodhihirisha ile dhamana yake kwa binadamu aliyejeruhiwa, anayetendewa vibaya na kutawaliwa na ukosefu wa upendo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Familia kimsingi ni “Ndiyo” ya upendo wa Mungu. Upendo ni chimbuko ambalo linaiwezesha familia kushuhudia sanjari na kuzalisha upendo wa Mungu duniani. Bila upendo huu, si rahisi sana kuweza kuishi kama watoto wa Mungu, watu wa ndoa, wazazi na kama ndugu.
Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuhimiza umuhimu wa familia kuishi kwa kujikita katika upendo kwa ajili ya upendo na ndani ya upendo wenyewe. Hii ina maana kwamba wanandoa wanapaswa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusameheana, kuvumiliana na kuheshimiana. Baba Mtakatifu anawaalika wanafamilia kumwilisha ndani mwao maneno makuu matatu: “Hodi, samahani na asante”. Mama Kanisa kila wakati anapata mang’amuzi ya udhaifu wa binadamu, ndiyo maana watu wote, familia pamoja na viongozi wa Kanisa wanapaswa kujenga unyenyekevu uliopyaishwa, unaotamani kufundwa vyema; kuelimishwa ili uweze kuelimisha; kusaidiwa ili uweze kusaidia; kusindikiza, kung’amua na kuwaingiza na kuwashirikisha watu wote wenye mapenzi mema.
Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, anaota ndoto ya kuona Kanisa lisilojitafuta lenyewe, bali Kanisa linalotoka kwenda kuwatafuta watu waliojeruhiwa; Kanisa lenye huruma linalotangaza na kushuhudia upendo wa Mungu ambao ni chemchemi ya huruma, unaowapyaisha watu, ili kweli familia za Kikristo ziweze kuwa ni madhabahu ya huruma na shuhuda wa huruma ya Mungu. Baada ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani, Dublin, itakuwa tena ni fursa ya kumwilisha mikakati hii katika uhalisia wa maisha ya watu!
Mafundisho ya Wosia “Furaha ya upendo ndani ya familia” yanapaswa kupewa msisitizo wa pekee, kwani Kanisa linatamani kuwaona wanandoa wakiwa daima katika hija ya maisha ya kiroho yanayomwilishwa katika ukweli wa maisha. Baba Mtakatifu anapenda kuishukuru familia ya Mungu Jimbo kuu la Dublin na Ireland katika ujumla wake kwa ukarimu na dhamana waliyotwisha na Mama Kanisa ya kuandaa maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani. Anawaombea ili Mwenyezi Mungu aweze kuwalipa tangu sasa kutokana na ukarimu wao pamoja na kuwakirimia neema za mbinguni. Familia Takatifu ya Nazareti, iwaongoze, iwasindikize na kuwabariki katika huduma na famili zote zinazohusika katika maandalizi ya tukio hili kubwa kimataifa huko Dublin, Ireland.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni