Hii ndiyo changamoto wanayokabiliana nayo akina mama sehemu mbali mbali za dunia; ni wanawake wenye ujasiri hadi dakika ya mwisho katika maisha yao! Hawa ni wanawake wanaofanya maamuzi magumu kwa kukubali kupokea ndani mwao historia ya maisha mapya ya binadamu ambaye anatarajiwa kuzaliwa. Ndiyo ya Bikira Maria ni litania ya utii itakayosindikiza maisha yake kama Mama! Injili inamwonesha Bikira Maria kuwa ni Mama mwenye kimya kikuu, wakati mwingine hakutambua kile kilichokuwa kinatendeka kuzunguka maisha yake, lakini ni mwanamke wa shoka aliyetafakari kwa kina kila neno na matukio yaliyogusa maisha yake!
Hii ni sehemu ya mwendelezo wa Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko juu ya matumaini ya Kiksro aliyoitoa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumatano, tarehe 10 Mei 2017. Saikolojia ya Bikira Maria inaonesha kwamba, hakuwa ni mwanamke aliyekuwa anakata tamaa mapema pale alipokuwa anakumbana na vizingiti katika maisha yake; hakuonesha upinzani na matumizi ya nguvu alipokumbana na changamoto za maisha. Ni mwanamke alikita maisha yake katika utamaduni wa kusikiliza kwa makini na akajitahidi kujenga uhusiano wa dhati kati ya kusikiliza na matumaini, amana anayowashirikisha pia waamini wa nyakati hizi.
Baba Mtakatifu anasema, hii ni amana iliyosheheni kurasa zenye furaha, lakini pia kwa upande mwingine kurasa hizi zilijaa mahangaiko yake ndani aliyokumbana nayo katika hija ya maisha yake hapa duniani, hadi pale alipodiriki kusimama chini ya Msalaba na kumwona Mwanaye wa pekee akipigiliwa misumari na hatimaye kufa Msalabani. Bikira Maria akasimama kimya na kumwangalia Mwanaye mpendwa akionesha utii wa hali ya juu kwa Baba yake wa mbinguni. Alionesha ujasiri wa hali ya juu hata pale mitume na marafiki zake Yesu walipokuwa wamesambaratika kutokana na woga na wasi wasi kuhusu hatima ya maisha yao! Akasimama chini ya Msalaba na kushuhudia ukatili wa hali ya juu aliotendewa Mwanaye wa pekee, mtu asiye kuwa na hatia akikata roho Msalabani.
Uchungu wa mateso ya Mwanaye ukapenya moyoni mwa Bikira Maria, lakini akaonesha ujasiri wa kusimama chini ya Msalaba, neno pekee ambalo Wainjili wanalitumia kumwonesha Bikira Maria bila kuongeza wala kupunguza jambo lolote lile kuhusu mateso na mahangaiko yake ya ndani! Bikira Maria alisimama pale chini ya Msalaba na kuteseka pamoja na Mwanaye Yesu Kristo! Alikuwa anatembea kwenye usiku wa giza nene, lakini aliendelea kuwa mwaminifu, akawasha mshumaa wa matumaini bila ya kutambua mustakabali wa maisha ya Mwanaye mpendwa Yesu Kristo ambao ungewafungulia wanadamu! Alikuwa pale chini ya Msalaba ili kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yake kama Mtumishi wa Bwana na kuendelea kuteseka pamoja na Mwanaye mpendwa.
Bikira Maria ni mfano wa wanawake wajasiri wanaosimama kidete kushuhudia mateso na mahangaiko ya watoto wao kutokana na sababu mbali mbali. Ndiyo maana Bikira Maria tangu mwanzo wa Kanisa anaitwa “Mama wa matumaini” katika Jumuiya ile ambayo ilikuwa imetikiswa na kuguswa; baadhi yao wakatimua mbio na kumwacha peke; wengine wakamsaliti na kushikwa na wasiwasi na woga. Lakini, Bikira Maria alikuwepo kama kawaida yake kana kwamba, hakuna jambo kubwa ambalo lilikuwa limetukia; akawa ni shuhuda wa mwanga wa Fumbo la Ufufuko na matumaini kwa Wafuasi wa Kristo.
Kutokana na ujasiri huu anasema Baba Mtakatifu, Kanisa linamwita Bikira Maria kuwa ni Mama wa matumaini na kamwe Wakristo siyo watoto pweke na yatima, bali wanaye Bikira Maria, Mama wa Mungu anayewafundisha kutumaini na kuwa na saburi katika maisha; kufumbata imani katika Fumbo la maisha ya Mungu hata pale giza totoro linapowafunika macho; wanapoelemewa na dhambi pamoja na changamoto za dunia! Bikira Maria amekuwa ni cheche za matumaini kwa wale waliokata tamaa kwa kuwatia shime kusimama na kusonga mbele kwani Bikira Maria ni Mama wa imani, matumaini na mapendo!
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuungana naye katika sala wakati wa hija yake ya kitume kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, nchini Ureno, kuanzia tarehe 12 – 13 Mei 2017. Baba Mtakatifu anakwenda huko ili kumkabidhi Bikira Maria wa Fatima mahitaji ya walimwengu na kuomba baraka za mbinguni. Hii ni hija ya matumaini na amani! Anawaalika waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili, waaminifu kwa Msalaba na Injili ya Kristo. Amekazia umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya ujenzi wa haki, amani, maridhiano, ustawi na mafao ya wengi!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni