0

Askofu mkuu Thomas A. White aliyekuwa Balozi wa Vatican katika nchi mbali mbali duniani, amefariki dunia, Jumapili tarehe 7 Mei 2017. Askofu mkuu White alizaliwa tarehe 12 Agosti 1931, Jimboni Ossory, nchini Ireland. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 25 Februari 1956 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Baada ya miaka miwili ya maisha na utume wake wa Kikuhani, akajiunga na Taasisi ya Kanisa inayotoa mafunzo maalum ya kidiplomasia kwa wafanyakazi wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia.

Kunako mwaka 1960 akaanza utume wake katika masuala ya kidiplomasia na kutumwa Nairobi, nchini Kenya kama Katibu wa Ujumbe wa Kitume kutoka Afrika Mashariki. Kunako mwaka 1965 akahamishiwa nchini Guatemala; 1967 akapelekwa nchini Colombia na kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya hija ya kitume ya Mwenyeheri Paulo VI nchini Colombia kunako mwaka 1968. Kunako mwaka 1970 akatumwa kwenda nchini Uswiss na huko akawa ni Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, Uswiss.
Kunako mwaka 1974 akarejeshwa mjini Vatican kuendelea na utume wake kwenye Sekretarieti kuu kama Mkuu wa kitengo cha diplomasia mjini Vatican. Baadaye akatumwa nchini China. Kunako tarehe 27 Mei 1978 akateuliwa kuwa Askofu mkuu na kuwekwa wakfu tarehe 30 Julai 1978 na akatumwa nchini Rwanda, kama Balozi wa Vatican na kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa muda wa miaka mitano. Mwaka 1983 akateuliwa na Papa Yohane Paulo II kuwa Balozi wa Vatican nchini Ethiopia. Mwaka 1989 akateuliwa tena kuwa ni Balozi wa Vatican nchini New Zealand na Mwakilishi wa Kitume huko Oceania. Na kunako mwaka 1996 baada ya kazi na utume wa kutukuka akang’atuka kutoka madarakani na tarehe 7 Mei 2017, akapumzika kwenye usingizi wa amani, akiwa na tumaini la ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele!

Chapisha Maoni

 
Top