Mama Kanisa, Jumapili, tarehe 7 Mei 2017 anaadhimisha Siku ya 54 ya Kuombea Miito Duniani inayoongozwa na kauli mbiu “Tukisukumwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya utume”. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho haya anakumbusha kwamba, wito wa Kikristo ni
mwaliko wa kutoka katika ubinafsi, tayari kujizatiti kusikiliza kwa makini sauti ya Mwenyezi Mungu anayeita daima na kutambua umuhimu wa Jumuiya ya Kikristo kama mahali maalum pa kuibua, kukuza na kushuhudia wito. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu kwa mwaka huu 2017 anapenda kukazia mwelekeo wa Kimisionari katika wito wa Kikristo! Hawa ni wale ambao wamesikiliza sauti ya Mungu, wakajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumfuasa Kristo na kwamba, wanatambua ndani mwao kuwa wanayo dhamana na wajibu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa jirani zao kwa njia ya: Uinjilishaji na huduma ya upendo!
mwaliko wa kutoka katika ubinafsi, tayari kujizatiti kusikiliza kwa makini sauti ya Mwenyezi Mungu anayeita daima na kutambua umuhimu wa Jumuiya ya Kikristo kama mahali maalum pa kuibua, kukuza na kushuhudia wito. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu kwa mwaka huu 2017 anapenda kukazia mwelekeo wa Kimisionari katika wito wa Kikristo! Hawa ni wale ambao wamesikiliza sauti ya Mungu, wakajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumfuasa Kristo na kwamba, wanatambua ndani mwao kuwa wanayo dhamana na wajibu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa jirani zao kwa njia ya: Uinjilishaji na huduma ya upendo!
Ikumbukwe kwamba, wakristo wote ni wamissionari wa Injili waliopokea zawadi ya wito wa upendo wa Mungu si kwa ajili ya mafao binafsi, wala kujitafuta mwenyewe, bali upendo huu umewageuza kuwa ni chemchemi ya furaha, kiasi cha kujisikia kuwa wanapendwa na Mungu na kwamba furaha ya Injili inayojaza maisha ya Jumuiya ya wafuasi wa Kristo ni furaha ya kimissionari, kiini cha imani na nguzo ya mahusiano na Kristo Yesu anayewatuma wafuasi wake ulimwenguni kama Manabii wa Neno na Mashuhuda wa upendo wake.
Baba Mtakatifu katika ujumbe wake wa Siku ya Kuombea Miito Duniani anakaza kusema, hata katika udhaifu wa kibinadamu unaowafanya wakati mwingine kujisikia kukatishwa tamaa, lakini wanapaswa kusimama kidete, kutoka kifua mbele kumwelekea Mwenyezi Mungu bila kuruhusu kugalagazwa chini kwa kuwa watazamaji waliochoshwa na maisha pamoja na mazoea ambayo kimsingi yana shida zake, lakini hakuna nafasi hata chembe moja kwa ajili ya woga usiokuwa na mvuto wala mashiko! Ni Mungu mwenyewe anayekuja na kuwatakasa waja wake kutokana na dhambi zao, tayari kutoka ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama ilivyokuwa kwa Nabii Eliya!
Kila mtume mmissionari katika undani wa moyo wake, anasikia sauti ya Mungu ikimwita kupita kati ya watu kama ilivyokuwa kwa Yesu ili kuwaganga, kuwaponya na kuwabariki watu wa Mungu. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, kila Mkristo ni “Kristofa” yaani ni “mjumbe wa Kristo” anayempeleka Kristo kwa jirani zake. Hii ni dhamana ya pekee kwa wale wote waliojitoa na kujisadaka kama Wakleri na Watawa, wakaitikia kwa moyo wa ukarimi na upendo, “Mimi hapa”, wanahamasishwa na Mama Kanisa kutoka huko walikojifungia kwenye Sakristia na nyumba za kitawa tayari kwenda kutangaza na kushuhudia wema na huruma ya Mungu kwa watu wake. Kanisa linawahitaji Mapadre wenye imani na utulivu wa ndani baada ya kugundua hazina, wako na ari na moyo mkuu wa kutaka huruma na upendo wa Mungu uweze kufahamika na wengi.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Kuombea Miito Duniani anajitahidi kujibu maswali ya msingi kuhusu nani ni mmissionari na anapata wapi nguvu na ujasiri wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na anakita ujumbe huu katika mantiki ipi! Baba Mtakatifu anakaza kusema, Yesu baada ya kupakwa mafuta na Roho Mtakatifu alitumwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa Mataifa. Wamissionari wa Kristo Yesu wanashiriki utume wa Kristo kwa kupakwa mafuta na Roho Mtakatifu wanatumwa kwenda kuwahubiri maskini Habari Njema, kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao na vipofu kupata kuona tena na kuwaacha huru waliosetwa na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa! Huu ndio utume wa Wakristo waliopakwa mafuta na Roho Mtakatifu wanatumwa kwenda kwa jirani zao ili kutangaza Habari Njema na hatimaye, kuwa ni vyombo vya wokovu!
Baba Mtakatifu anasema, Yesu daima anatembea na wafuasi mitume wake bega kwa bega, ili kuweza kukabiliana na changamoto za maisha ya kila siku, kwa kuwa na nguvu na matumaini katika yeye anayewawezesha na kwamba, utume huu si jambo la kufirikika linaloelea katika ombwe, bali ni utume unaovuka mipaka ya uwezo na nguvu zao za kibinadamu! Yesu Mfufuka alisindikizana na wanafunzi wawili wa Emau, huo ukawa ni mwanzo wa “Liturujia ya Barabarani” inayotangulia Liturujia ya Neno na Ekaristi Takatifu, yaani Mkate uliomegwa na kutolewa kwa waamini kama chakula chao cha maisha ya kiroho, ili kuwakumbusha waamini kwamba, kila hatua ya maisha yao, Yesu yupo! Bandua bandika! Yesu yupo!
Wanafunzi wa Emau waliotikiswa sana na Kashfa ya Msalaba, walikuwa wanarejea nyumbani huku wakiwa wamebeba ndani mwao kashfa ya kushindwa na matumaini yaliyotoweka kama ndoto ya mchana. Furaha ya Injili ikamezwa na masikitiko na huzuni yao! Yesu Mfufuka anawatokea na kuanza kuandamana nao, anachukua fursa hii ili kuwashirikisha “cheche za mageuzi” katika maisha na kuanza kuwatia shime, kufungua akili na nyoyo zao; kuwatangazia Habari Njema na Kumega Mkate pamoja nao. Baba Mtakatifu anasisitiza kwamba, dhamana na wito wa kimissionari unaotekelezwa na Mkristo unabeba ndani mwake machungu, magumu na hata wakati mwingine hali ya kutoeleweka lakini anatambua kwamba, Yesu ana andamana, anatembea, anapumua na kufanya naye kazi. Anahisi uwepo wa Yesu aliye hai pamoja naye na kati kati ya kazi za kimissionari.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutambua kwamba, Yesu ndiye anayeiwezesha ile mbegu ya Neno iliyopandwa katika maisha ya watu kumea, kukua na kuzaa matunda yanayokusudiwa, yaani toba na wongofu wa ndani! Na wala si kwa kutumia madaraka, wongofu wa shuruti, misimamo mikali ya kidini na kiimani pasi na maridhiano. Injili ya Kristo ni mwaliko wa kuondokana na uchu wa fedha, mali na madaraka; hofu na wasi wasi wa kupita kiasi wa kutaka kulinda miundo mbinu ya Kanisa; kwa kumezwa mno na mwelekeo wa kutaka kushinda badala ya kujikita katika mwelekeo wa huduma. Mbegu ya Ufalme wa Mungu inakua polepole kutokana na kazi inayotendwa na Mwenyezi Mungu.
Kumbe, waamini kwanza kabisa wanapaswa kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu anayevuka matumaini ya kibinadamu na kuendelea kuwashangaza kutokana na ukarimu, kwa kufanya mbegu iliyopandwa kutoa matunda kinyume kabisa cha matarajio na udhaifu wa kibinadamu! Imani hii inayofumbatwa kwenye tunu za Kiinjili inawafungulia waamini kutambua uwepo wa Roho Mtakatifu msingi wa utume wa Kanisa, anayetenda katika hali ya ukimya. Utume na wito wa Kikristo unafumbatwa katika sala endelevu na tafakari ya kina ya Neno la Mungu; kwa kukuza na kudumisha uhusiano binafsi na Kristo Yesu kwa njia ya maadhimisho ya Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, mahali muafaka pa kukutana na Mwenyezi Mungu katika sala na ukimya!
Baba Mtakatifu anapenda kuwahimiza waamini kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya wito wa Kipadre na maisha ya kuwekwa wakfu. Watu wa Mungu wanapaswa kuongozwa na watumishi wa Mungu wanaoyamimina maisha yao kwa ajili huduma ya Injili, changamoto na mwaliko kwa waamini na vyama vyote vya kitume, kujizatiti katika sala ili kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kupeleka watenda kazi: wema, watakatifu na wachapakazi katika shamba lake. Wafanyakazi ambao wameshibana vyema na Injili, tayari kujisadaka kwa ajili ya Injili ya huruma na mapendo kwa jirani zao; kwa kukazia utu, furaha na upendo katika huduma. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 54 ya Kuombea Miito Duniani anapenda kuwaweka vijana wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mkombozi. Sala na maombezi yake yafungue nyoyo na utayari wa waamini kusema “Mimi hapa Bwana” wanaposikia sauti ya Mungu ikiwaita, tayari “kuchanja mbuga” kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo duniani kote kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni