0
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 24 Mei 2017 majira ya saa 2:30 asubuhi kwa saa za Ulaya, anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye baadaye pia atakutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican atakayekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican. Habari zaidi kutoka Washington DC., Marekani
zinasema kwamba, Rais Trump, Alhamisi tarehe 4 Mei 2017 ametangaza rasmi kwamba, ziara yake ya kwanza kama Rais wa Marekani ataifanya kwenye Falme za Kiarabu, ili kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini; kusimama kidete kupambana na vitendo ya kigaidi, misimamo mikali ya kidini pamoja na kudumisha amani sehemu mbali mbali za dunia. Rais Trump anasema, anataka kukutana na viongozi wa dini ya Kiislam nchini Saudi Arabia, mahali patakatifu kwa waamini wa dini ya Kiislam ili kukazia haki na amani sanjari na kuwajengea vijana matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.
Rais Trump katika sera na mikakati yake ya mambo ya nchi za nje anataka kushirikiana zaidi na Israeli, ili kusukuma mbele mchakato wa amani na maridhiano kati ya Israeli na Palestina. Anapania kuimarisha urafiki na wadau mbali mbali huko Mashariki ya Kati ili kupambana na vitendo vya kigaidi na hatimaye, kurejesha tena amani, utulivu na usalama huko Mashariki ya kati. Rais Trump, Alhamisi amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza kwa faragha na Makardinali wa Kanisa Katoliki kutoka Marekani. Changamoto ya wakimbizi na wahamiaji; umuhimu wa kulinda, kutunza na kudumisha  utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; umuhimu wa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana ili kufahamiana na hatimaye kushikamana katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni kati ya changamoto kubwa ambazo pengine, Rais Trump na Baba Mtakatifu Francisko watazijadili watakapokutana mjini Vatican. Hatima ya Wakristo huko Mashariki ya Kati ni changamoto pevu katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu!
Kimsingi, Baba Mtakatifu anakazia majadiliano katika ukweli na uwazi sanjari na juhudi za kidiplomasia katika kutafuta suluhu ya kudumu kwa changamoto na matatizo yanayoendelea kufuka moto na hivyo kutishia misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu sehemu mbali mbali za dunia. Rais Trump atakuwa nchini Italia ili kuhudhuria mkutano wa G7.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top