0

Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuridhia sheria mpya kuhusu taratibu za kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu anasema, zoezi hili ni kwa ajili ya mafao ya wengi linapaswa kuongozwa na kanuni za ukweli na uwazi; gharama nafuu katika mchakato wa kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu. Sheria hizi mpya zimepitishwa na Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kikao chake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, hapo tarehe 4 Machi 2016.

Sheria hizi baada ya kuchapishwa kwenye gazeti la L’Osservatore Romano zinaanza kutumika kama majaribio kwa kipindi cha miaka mitatu, “Ad Experimentum”. Sheria hizi mpya zinafuta sheria zilizokuwa zimepitishwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1983. Pamoja na mambo mengine, sheria hii inakazia umuhimu wa mchakato huu kuwa ni kwa ajili ya mafao ya wengi na kwamba, Vatican itasaidia kubeba gharama za mchakato huu utakapoingia hatua yake mjini Roma. Gharama hizi zinachangiwa pia na wahusika kwa kutoa mchango wao, ili kuhakikisha kwamba kwa namna yoyote ile mchakato haukwami kutokana na ukwasi au uhaba wa fedha za kuendeshea mchakato huo. Sheria hizi zinaweka bayana pia uwepo wa Mfuko wa mshikamano ambao umeanzishwa kwenye Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu.

Hii inatokana na ukweli kwamba, mchakato wa kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu unachukua muda mrefu na una gharama kubwa, kumbe, kanuni ya ukweli na uwazi ni muhimu kuzingatiwa kwa kuwahusisha Maaskofu wa Makanisa mahalia pamoja na wahamasishaji wa mchakato huu, ili yote yatendeke katika misingi ya ukweli na uwazi. Mhamasishaji mkuu ataunda mfuko kwa ajili ya kumtangaza mwamini kuwa mwenyeheri au mtakatifu. Mfuko huu utachangiwa na watu mbali mbali kwa nia ya kudumisha  ibada. Msimamizi wa mfuko huu anapaswa kuhakikisha kwamba, anazingatia kikamilifu nia ya wafadhili wa mfuko huu pamoja na kuhakikisha kwamba, hesabu zake zinatungwa kwa umakini mkubwa na kutolewa mapato na matumizi yake kila mwaka, hatimaye kupitishwa na nakala yake kutumwa kwa mhamasishaji mkuu wa mchakato.
Pale ambapo mhamasishaji mkuu anapenda kutumia sehemu ya fedha kutoka kwenye mchakato wa kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, atapaswa kwanza kabisa kupata kibali kutoka kwenye Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu. Nakala ya bajeti nzima inapaswa kupelekwa kwa viongozi wakuu wanaohusika katika kudhibiti matumzi ya Mfuko huu. Pale ambapo sheria na kanuni hizi zitakiukwa, Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu litahusika kutoa adhabu. Mfuko huu utakoma uwepo wake baada ya mchakato wa kumtangaza mwamini kuwa mwenyeheri au mtakatifu. Msimamizi wa Mfuko huu atapaswa kutoa hesabu zake ili kuhakikiwa na hatimaye kupitishwa. Kiasi kitakachokuwa kimesalia baada ya mchakato mzima, kitapelekwa kwenye Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu. Hapo mfuko utakoma.
Sheria hizi zinaonesha kwamba, kutakuwepo na Mfuko wa Mshikamano utakaoanzishwa na Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa watakatifu na wenye heri. Mfuko huu utakuwa unachangiwa na wafadhili binafsi au kutoka katika vyanzo vingine vitakavyobainishwa. Pale ambapo kutakuwepo na ukwasi katika kuendeleza mchakato wa kumtangaza mwamini kuwa mwenyeheri au mtakatifu, Mhamasishaji mkuu wa mchakato anaweza kuomba msaada kutoka katika mfuko huu, ikiwa kama hatua ya mchakato imefikia mjini Roma. Ombi hili litatumwa na kiongozi mhusika. Lakini kwanza kabisa lazima kuwepo na uhakiki wa kutosha kuhusu hali ya kiuchumi na kifedha na vizingiti vilivyopo na jinsi ambavyo msaada huu utaweza kusaidia kusongesha mbele mchakato. Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu litaamua kila kesi itakaowasilishwa na kuipatia majibu yake!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top